Na NJUMAI NGOTA,
Ruvuma
MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa leo kuhutubia mkutano mkubwa wa hadhara eneo la Mbamba Bay katika Wilaya ya Nyasa, mkoani Ruvuma, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kuomba ridhaa ya wananchi kumpigia kura katika Uchaguzi Mkuu.
Dk. Samia atawasili leo katika Uwanja wa Ndege wa Songea ambako atapokewa na viongozi wa CCM na wananchi wa mkoa huo wakiongozwa na Mgombea Mwenza wa Urais, Dk. Emmanuel Nchimbi.
Kauli hiyo ilitolewa mjini Songea na Mwenyekiti wa CCM mkoani Ruvuma, Oddo Mwisho, muda mfupi baada ya Dk. Nchimbi kukagua Uwanja wa VETA uliopo Msamala utakaofanyika mkutano mkubwa wa hadhara kesho.
“Ndugu zangu wananchi wa Mkoa wa Ruvuma, napenda kuwajulisha kwamba, ziara ya Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, imeshatimia na kesho (leo) atawasili Uwanja wa Ndege wa Songea.
“Kwa hiyo ndugu zangu wananchi akishafika katika Uwanja wa Ndege atapokewa na viongozi na wananchi wa mkoa mzima wa Ruvuma wakiongozwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi,” alisema.
Mwenyekiti huyo alisema baada ya kupokewa na viongozi wa Chama na wananchi, Dk. Samia ataanza ziara wilayani Nyasa kutafuta kura za wananchi.
Mwisho alisema akiwa njiani kwenda Nyasa, Dk. Samia atapita wilayani Mbinga, ambako atafanya mkutano wa hadhara katika Mji wa Mbinga.
“Kwa hiyo tunatoa wito wananchi wa Wilaya ya Mbinga kukusanyika katika eneo la barabara ya DAE Company Limited, ambako atazungumza na wananchi,” alisema.
Alieleza baada ya mkutano huo, mgombea huyo wa urais atakwenda Mbamba Bay, ambako atafanya mkutano mkubwa wa kuomba kura na ridhaa ya wananchi kumchagua Oktoba 29, mwaka huu.
Alisema baada ya mkutano huo, Dk. Samia atarejea Songea mjini ambako kesho atafanya mkutano mwingine katika viwanja vya VETA.
“Kwa hiyo ndugu wananchi wa Songea mjini, wananchi wa Wilaya ya Songea Vijijini, Madaba na viunga vyake, tunawaomba sana kutoka Peramiho, Madaba tukusanyike viwanja vya Veta Septemba 22 kuanzia saa 1 asubuhi tayari kwa mkutano huo,” alisema.
Kwa mujibu wa Mwisho, baada ya kumaliza mkutano huo Songea Mjini, Dk. Samia atakwenda wilayani Namtumbo kwa mkutano mwingine wa hadhara na wananchi wa eneo hilo.
“Tunategemea umati wa wananchi wa Namtumbo kumpokea na kumsikiliza mgombea wetu wa urais,” alisema.
Mwenyekiti huyo alisema kesho alasiri, mgombea huyo atakwenda wilayani Tunduru ambako atafanya mkutano na wananchi wa Tunduru Kaskazini na Kusini.
Alisema baada ya ziara hiyo, Septemba 23, Rais Dk. Samia atakwenda mkoani Mtwara ambako atafanya mkutano Tarafa ya Nakapanya.
“Asubuhi hiyo ya tarehe 23, atafanya mkutano kuanzia saa mbili asubuhi na tunawaomba wananchi wa kata zote zinazojumuisha Tarafa ya Nakapanya wakusanyike katika viwanja vya Nakapanya mjini,” alisema.
Aliongeza mkoa huo wamejipanga kikamilifu kuhakikisha mapokezi ya kihistoria kwa mgombea huyo.
Awali, viongozi wa mkoa wa Ruvuma wakiongozwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Leyla Ngozi na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Jackson Msomi walitembelea wilaya zote za mkoa huo kuangalia hali ya maandalizi.