Na MUSSA YUSUPH,
Ruvuma
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amewahakikishia wakulima nchini, serikali katika miaka mitano ijayo itaimarisha masoko na kutafuta bei nzuri kwa mazao yao, wanufaike kupitia jasho lao.
Pia, amesema serikali inakusudia kujenga reli ya kisasa (SGR) kutoka Mbamba Bay hadi Mtwara yenye urefu wa kilometa 1,000 itakayopita maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mazao.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mbamba Bay, wilayani Nyasa, mkoani Ruvuma, Dk. Samia alisema serikali inafanya jitihada kutafuta bei nzuri ya mazao.
“Kahawa kwa mfano mpaka mwaka 2022 walikuwa wakiuza shilingi 4,500 lakini hadi jana (juzi) inauzwa shilingi 12,500 hiyo ni bei ya kahawa kwa kilo. “Tutaendelea kuhangaika kutafuta bei nzuri za mazao. Mahindi, wakipita walanguzi mnawauzia kwa shilingi 450 hadi 500, lakini vituo vyetu vya NFRA (Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula) vinanunua kilo kwa shilingi 700 kwa hiyo niwaomba subirini NFRA mje muuze.
“Pamoja na jitihada hizo, tumekusudia kuimarisha mfumo wa stakabadhi ghalani, masoko ya mazao ya biashara na tutaanzisha vituo vya ukodishaji zana za kilimo,” alisema.
Kuhusu ajira, alisema kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM (2025-2030) serikali imekusudia kujenga viwanda vya kuongeza thamani ya mazao kila wilaya.
Alibainisha serikali itaanza na wilaya zenye uzalishaji mkubwa, ambapo Nyasa utafungwa mtambo wa kukaushia samaki eneo la Mbamba Bay.
Pia, serikali itafunga mtambo wa kukoboa kahawa kuongeza thamani hatua ambayo itachangia ongezeko la ajira kwa vijana.
Dk. Samia alisema serikali inakusudia kujenga soko kubwa la kimataifa Mbamba Bay ambalo litakuza mapato na kuongeza fursa kwa wananchi na kuhudumia nchi za Malawi na Msumbiji.
“Hata wanaovua dagaa wataweza kupata wateja wengi na bei nzuri,” alisisitiza.
Akizungumzia uvuvi, Dk. Samia alisema serikali imejipanga kuongeza ufugaji samaki katika vizimba kuongeza uzalishaji na fursa kwa wananchi na
kutoa vifaa vya kisasa vya uvuvi, ikiwemo kukodisha boti za uvuvi na kupata boti ya uokozi Ziwa Nyasa.
Dk. Samia alisema serikali imetekeleza ilani kwa mafanikio makubwa ndiyo sababu CCM imekuwa na ujasiri kurudi tena kwa wananchi kuinadi ilani mpya.
Alieleza ilani hiyo itakwenda kutekeleza mambo ambayo yataleta maendeleo na uimarishaji taifa na kustawisha hali za wananchi.
Dk. Samia alisema alipofika katika wilaya hiyo aliweka jiwe la msingi kwa ujenzi wa Bandari ya Mbambabay, ambayo utekelezaji wake unaendelea vizuri.
“Ile ndoto ya muda mrefu ya wananchi wa Nyasa kuwa na bandari ya uhakika inaelekea kutimia mapema mwakani. Vilevile, mtakumbuka nilizindua barabara ya Mbinga-Mbamba Bay yenye urefu wa kilometa 66 ambayo ni kiunganishi kati ya Bandari ya Mtwara na Bandari ya Mbamba Bay.
“Tulikamilisha ujenzi wa bandari ya Ndumbi ambayo tayari imekamilika na inaendelea kufanya kazi pia imeongeza uwezo wa kuhudumia shehena kutoka tani 40,000 hadi tani 100,000 kwa mwaka,” alisema.
Dk. Samia alisema idadi ya abiria waliosafirishwa kupitia bandari hiyo imetoka wastani wa watu 45,000 hadi 100,000 kwa mwaka.
Pamoja na bandari hiyo, alisema serikali inatekeleza mradi mkubwa ambao tafiti zimeshakamilika wa ujenzi wa reli yenye urefu wa kilometa 1,000 itakayopita maeneo yenye utajiri mkubwa wa nafaka.
Vilevile, alisema itaunganisha maeneo ya kiuchumi ya Liganga na Mchuchuma yenye utajiri mkubwa wa chuma na makaa ya mawe.
“Tupo kwenye mazungumzo tuweze kujenga reli hii ya kisasa kwa viwango vya kimataifa kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay. Hayo ndiyo tunayoyafikiria kwa Wilaya ya Nyasa.
“Ni wazi reli hii tukiijenga itaambatana na manufaa makubwa ya kiuchumi kwa ukanda wa kusini. Nani kama CCM?” aliuliza.
Dk. Samia alisema serikali haijazisahau sekta za kijamii wilayani hapo, kwani mafanikio makubwa yameshuhudiwa akitolea mfano sekta ya afya maboresho yamefanyika katika hospitali ya wilaya, vituo vitatu vya afya na kujenga kipya kimoja.
Kadhalika, alibainisha serikali imejenga zahanati mpya tisa, imeajiri watumishi wa afya 316 na imani ya serikali ni kuongeza watumishi kadri fursa za ajira zinapojitokeza.
Mgombea huyo urais kupitia CCM alisema katika sekta ya elimu, wilaya hiyo imenufaika kupitia ujenzi wa shule mpya 12 ambazo sita za msingi na sita za sekondari pamoja na chuo cha ufundi stadi.
Alisema lengo la chuo hicho ni kuchochea ajira kupitia ujuzi watakaopata vijana ambao wataanzisha viwanda.
Kuhusu nishati, alieleza umeme umefikishwa vijiji vyote vya Wilaya ya Nyasa, vitongoji 153 huku bado kazi ya kusambaza nishati hiyo katika vitongoji 423 ikiendelea.
“Ninafahamu Nyasa kuna changamoto ya umeme kuwa mdogo, tutajenga kituo cha kupokea na kupoza umeme kipokee umeme kutoka Songea, uingie Nyasa kisha usambazwe. Hiyo inakwenda kuondoa tatizo la umeme na kuvutia wawekezaji kuja Nyasa,” alisema.
Dk. Samia alisema serikali imeendelea kuwekeza katika miundombinu ikiwemo ujenzi wa Daraja la Mto Luhuhu linalounganisha Ruvuma na Njombe.
Kadhalika, alieleza serikali itaendeleza ujenzi wa barabara kuu ya Kidatu-Ifakara-Malinyi-Londo hadi Lumecha yenye urefu wa kilometa 512 ambayo inaunganisha Ruvuma na Morogoro.
“Tayari tumekamilisha kilometa 61 na imani yangu tunakwenda kukamilisha sehemu iliyobakia,” aliongeza.
Alibainisha mpango wa ujenzi Daraja Mitomoni katika Mto Ruvuma kuunganisha Nyasa na Songea.
Awali, akihutubia maelfu ya wananchi wilayani Mbinga, Dk. Samia alisema serikali yake itahakikisha mkulima anapata bei nzuri kupitia mazao yake anayozalisha shambani.
“Niwaahidi serikali yenu itaendelea kutoa ruzuku kwa pembejeo, mbolea na pembejeo zingine. Kwa wafugaji pia tutaendelea kutoa ruzuku ya chanjo na huduma za ugani.
“Nimekuja kwa ujasiri mkubwa kwa sababu miaka mitano iliyopita tumeweza na mitano inayokuja kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu tutaweza. Katika afya, elimu, umeme na maji tunakwenda kukamilisha miradi yote,” alisema.
Alisema changamoto ya umeme katika vijiji imepatiwa ufumbuzi na hivi sasa juhudi hizo zimeelekezwa ngazi ya vitongoji ambavyo tayari nusu vimeunganishiwa nishati hiyo nchini na miaka mitano ijayo kazi hiyo itakuwa imeshahitimishwa.
Dk. Samia alisema upatikanaji wa maji unakaribia asilimia 90 hata hivyo ipo baadhi ya mikoa iko nyuma, lakini serikali imejikita kukamilisha miradi ya maji katika maeneo hayo.
Alisema katika miaka mitano ijayo miradi ya ujenzi wa barabara itaendelea kukamilishwa.
“Kuna barabara ambazo tumezitaja katika Ilani ya uchaguzi 2025-2030 ambazo zinakwenda kujengwa. Zipo barabara zitakazojengwa kwa lami na kiwango cha changarawe zipitike mwaka mzima, iwe jua au mvua.
“Pia tutaendelea kujenga madaraja yanayokatisha mawasiliano baina ya pande mbalimbali na kwa Wilaya ya Mbinga tutakwenda kujenga daraja la maalumu la Mto Lumeme.
Alisisitiza: “Hakuna miradi ghali kama ya ujenzi wa barabara, kwani kilometa moja ya barabara ni ujenzi wa vituo viwili vya afya, ndiyo maana hatuendi kwa kasi sana ila tukipunguza mzigo wa ujenzi wa afya, shule na maji tutakwenda haraka zaidi katika kujenga barabara.”
KATIBU MKUU
Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Asha-Rose Migiro, aliwaomba Watanzania kuchagua wagombea wanaotokana na CCM.
“Dk. Samia anahitaji mafiga matatu (kura za urais, wabunge na madiwani) hivyo namwombea kura yeye, wabunge na madiwani wote wa CCM,” alisema.
Naye, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho, alisema wamepanga vikosi vya ushindi kuhakikisha Chama kinapata ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, mwaka huu.
Mratibu wa Kampeni za CCM mikoa ya kusini (Lindi, Mtwara na Ruvuma) Leila Ngozi, alimshukuru Dk. Samia kwa kutekeleza miradi mingi katika mikoa hiyo.




