Na MUSSA YUSUPH,
Nyasa
MGOMBEA Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema wananchi katika mikoa 11 aliyofanya mikutano ya kampeni wametoa salamu watampigia kura za kishindo mgombea Urais kupitia CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, mwaka huu.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni za urais uliofanyika Mbamba Bay, wilayani Nyasa mkoani Ruvuma, Dk. Nchimbi alimshukuru Dk. Samia kwa usimamizi madhubuti wa rasilimali fedha zinazotumika kuleta miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini bila upendeleo.
“Katika kuzunguka kuomba kura ulinigawia maeneo ya kupita kama msaidizi wako, ambapo nilipita mikoa 11. Naomba nikupe salamu, mikoa hiyo imenituma nikwambie utashinda wewe Dk. Samia na CCM.
“Wamenituma nikwambie, wabunge wa CCM watashinda kwa kishindo, madiwani wa CCM watashinda kwa kishindo na kipenzi chao Dk. Samia atashinda kwa kishindo,” alisisitiza Dk. Nchimbi huku akishangiliwa na wananchi waliofurika katika mkutano huo.
Dk. Nchimbi alimshukuru Dk. Samia kwa kumpendekeza kuwa mgombea mwenza wa urais na kuahidi kumsaidia kwa uaminifu.
“Heshima hii siyo yangu pekee ni heshima kwa mkoa wote wa Ruvuma, tunakushukuru sana. Nitumie nafasi hii kukuhakikishia kwa mila zetu mkoa wa Ruvuma imani huzaa imani, nitakusaidia kwa uwezo na uaminifu wangu wote kuhakikisha unatekeleza ilani ya CCM kama ulivyokusudia. Pia unafikia maono yako ya kulikomboa taifa letu kutoka hali duni kuwa hali bora zaidi.
“Nitakuwa msaidizi wako mwaminifu na kwa nguvu zangu zote. Kwa niaba ya ndugu zetu wa Ruvuma tunakushukuru sana kwa maendeleo makubwa uliyoyafanya siyo kwa Ruvuma tu, bali Tanzania nzima, uwezo wako wa kutafuta rasilimali na kusimamia mgawanyiko wake kuhakikisha kila pembe ya nchi yetu inapata rasilimali bila ubaguzi.
Dk. Nchimbi alisema mgombea urais wa CCM amefanya vizuri kiasi wanachama wanatembea kifua mbele kukinadi Chama baada ya kuaminiwa na Watanzania, ambapo kila kona ahadi inayotolewa ni ushindi wa kishindo.
“Wana-CCM wote, wananchi wa Mkoa wa Ruvuma tutahakikisha tunapiga kura za heshima kwa rais wetu ambazo zitampatia nguvu kuendelea kututumikia na kuwaonesha dunia nzima tuna imani na mapenzi naye,” alisema.
Dk. Nchimbi aliwaomba wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kumpiga kura Dk. Samia, wabunge na madiwani wanaotokana na CCM.




