Na NJUMAI NGOTA,
Ludewa
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimetangaza neema ya ujenzi, ukarabati na uimarishaji wa barabara katika Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, mkoani Njombe, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa miaka mitano ijayo wa kuondoa kero ya miundombinu kwa wananchi wa eneo hilo, iwapo kitashinda Uchaguzi Mkuu.
Ahadi hiyo imetolewa katika viwanja vya Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa na Mgombea Mwenza wa urais kwa tiketi ya CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi, katika mkutano wa hadhara wa kampeni za Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.
Amesema katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama ya mwaka 2025-2030, haijaiacha Ludewa nyuma.
Ametaja barabara ambazo zimetajwa katika Ilani hiyo ni pamoja na Mkoma Ng’ombe – Mchuchuma itajengwa kilometa saba kiwango cha zege, ujenzi wa daraja la Kiwe na barabara ya Kiwe – Lipande, daraja la Igugu ambalo lipo Mto Ruhuhu, barabara ya Ludewa – Igumi- Ruhuhu na daraja la Mawe katika barabara ya Ilera-Msungu.
Pia, amesema wamedhamiria kukarabati na kuimarisha barabara ya Manyanya-Mwembahesa yenye urefu wa kilometa tisa, Lifuma-Mbwira (19), Mawengi-Makonde (28), Lusitu-Madilu- Ligalawa (32), Kigasi- Amani (63), Ludewa-Songa Mbele (4.8) na Amani- Ibumi (43).
“Tunatarajia kutengeneza makalavati ya zege, ujenzi wa barabara za lami katika eneo la Posta Mdoe, Ludewa mjini, Lugalawa mjini, Mavanga na matengenezo ya changarawe kati ya Ludewa na Igumu,” amesema.
Kwa mujibu wa Dk. Nchimbi, barabara ya mwambao wa Ziwa Nyasa zitapewa kipaumbele kikubwa kwa kuwa ni za kiusalama na kichocheo kikubwa cha uchumi wa Ludewa.
KILIMO
Amesema sekta ya kilimo itakuwa miongoni mwa maeneo yatakayopewa msukumo mkubwa zaidi hasa kwa kuhakikisha wakulima wa kahawa na korosho wanapata zana bora za kuchakata mazao yao.
Amesema serikali ya CCM imekusudia kupeleka mashine tano za kuchakata kahawa na tano za kubangua korosho kwa wakulima wa Ludewa, hatua itakayoongeza thamani ya mazao hayo kabla ya kuingia sokoni.
Amesema pamoja na mashine hizo, serikali inakusudia kujenga maghala sita ya kuhifadhi nafaka na utaratibu wa mbegu na mbolea ya ruzuku utaimarishwa zaidi kuongeza tija kwa mkulima.
UMWAGILIAJI
Aliahidi kupanua mabonde matatu ya umwagiliaji katika Wilaya ya Ludewa kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, mradi unaolenga kufungua ajira mpya kwa vijana kupitia kilimo cha kisasa kinachotegemea umwagiliaji.
AFYA
Kuhusu afya, alisema katika kipindi cha miaka mitano ijayo, wamejipanga kuiendeleza Hospitali ya Wilaya ya Ludewa kwa kuongeza majengo, vifaatiba, wataalamu wa afya na kujenga vituo vya afya 14 na zahanati nne.
ELIMU
Kuhusu sekta ya elimu, Dk. Nchimbi alisema wameahidi kujenga shule tano za msingi na madarasa 344 kupunguza msongamano wa wanafunzi.
Aidha, wamedhamiria kujenga maabara 12 kwa masomo ya sayansi pamoja na mabweni 14 kwa wanafunzi wa kike.
MAJI
Alisema serikali ijayo, imedhamiria kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji hadi kufikia asilimia 90 kwa vijijini na asilimia 95 kwa mijini.
Alisema miradi mikubwa ya maji inaendelea na mipya itaanzishwa katika kata 17 ambazo hazina mtandao wa maji kwa hivi sasa.
NISHATI
Alisema umeme umefika katika vijiji vyote vya Ludewa na wakapewa ridhaa watapeleka huduma hiyo katika vitongoji 125 vilivyosalia.
UVUVI
Upande wa sekta ya uvuvi, mgombea mwenza huyo alisema katika wilaya hiyo, wanakusudia kujenga vizimba 50 vya kufugia samaki na kuongeza boti ya doria katika Ziwa Nyasa.
Naye, mgombea ubunge wa Ludewa kwa tiketi ya CCM, Joseph Kamonga, alisema serikali ilipeleka zaidi ya sh. bilioni 318 katika Wilaya ya Ludewa kwa miradi ya maendeleo.
Alisema kati ya fedha hizo, zaidi ya sh. bilioni 68.5 zilitumika katika sekta ya elimu, ikiwemo ujenzi wa shule saba za sekondari, Chuo cha Ufundi (Njombe Technical School) na chuo cha VETA kilichogharimu sh. bilioni saba.
Alisema katika sekta ya afya walipokea zaidi ya sh. bilioni 27.7 ambapo vituo vya afya vinne na zahanati 22 zimejengwa huku tano zikiwa katika hatua za ujenzi.
Kwa upande wa barabara, Kamonga alisema Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imewekeza zaidi ya sh. bilioni 180 kwa ujenzi wa barabara ya zege kuanzia Hitoni hadi Lusitu.
Pia, alitoa shukrani kwa serikali kuingiza miradi muhimu ya miundombinu ya barabara katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2025-2030 ikiwemo barabara ya Njombe-Manda na Mkiu-Liganga- Madaba.
Alisema kukamilika barabara hizo kutakuwa ukombozi mkubwa kwa wananchi wa Ludewa.
Pia, aliishukuru serikali kwa kulipa fidia ya sh. bilioni 19 kwa wananchi wa maeneo ya Liganga na Mchuchuma na kuingiza reli ya kutoka Mtwara-Mbamba Bay-Liganga-Mchuchuma katika Ilani ya 2025-2030.