Na MUSSA YUSUPH,
LINDI
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema mkakati wa serikali yake pindi atakapopata ridhaa ya kuliongoza Taifa ni kukifanya kilimo kiwe cha kibiashara.
Dk. Samia aliyasema hayo katika mkutano wa kampeni uliofanyika Jimbo la Ndanda mkoani Mtwara, ambapo alisema lengo la serikali ni kukuza kilimo kiwe cha kibiashara.
Alisema hatua hiyo itawawezesha wakulima kunufaika kupitia shughuli zao za kilimo.
“Kupitia pembejeo za ruzuku kwa kweli mmetenda haki na uzalishaji umekua, sasa tutaendelea kutoa ruzuku kwenye pembejeo na pia kuwawezesha kuendelea kuzalisha zaidi kwa sababu lengo letu ni kufanya kilimo biashara,” alisema.
Pia, aliwaahidi wananchi kwamba serikali itaunganisha Ndanda na Mji wa Masasi kwa barabara ya lami.
“Ahadi yangu ni kwamba tutaboresha barabara kwa kiwango cha lami na changarawe ndani ya Jimbo la Ndanda na zile za kuifungua Ndanda. Lengo letu ni kuinganisha Ndanda na Mji wa Masasi ili mazao yasafirishwe kwa haraka sana,” alieleza.
Dk. Samia alitumia fursa hiyo kuwapongeza wananchi wa Ndanda kwa kuzalisha mazao ya chakula na biashara kwa wingi.
Alisema katika sekta ya elimu, ataendelea kutoa elimu bila malipo lakini pia elimu jumuishi ili watoto wenye mahitaji maalumu waweze kupata elimu.
“Natambua kwamba hapa Ndanda kuna shule maalumu, niwaahidi tunaenda kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji ikiwemo kujenga karakana ili vijana watoke na ujuzi,” alisisitiza.
Kwa upande wa maji, Dk. Samia alisema miaka mitano iliyopita serikali yake ilitoa sh. bilioni 13 na kutekeleza miradi ya maji 63.
Akiwa Jimbo la Mtama, Dk. Samia alitoa wito kwa wananchi pindi watakapovuna mazao yao watunze akiba ya fedha kujiunga bima ya afya kwa wote.