Na MWANDISHI WETU
MKUU wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob John Mkunda amempongeza Sajini Alphonce Simbu kwa ushindi wa medali ya dhahabu katika Mashindano ya Mbio za Marathon ya Dunia Kilomita 42, zilizofanyika Tokyo Japan.
Pia, Jenerali Mkunda amempandisha cheo mwanariadha huyo kutoka Sajini kuwa Sajinitaji.
Jenerali Mkunda alitoa pongezi hizo ofisini kwake Upanga Jijini Dar es Salaam, kuwa ushindi huo wa Simbu ni kwa Watanzania wote.
“Ushindi huu ni kwa Watanzania wote na na Afrika kwa ujumla na kwamba michezo ni sehemu ya kazi jeshini, hivyo Sajinitaji Alphonce Simbu amefanya kazi nzuri,” alisema.
Jenerali Mkunda alitoa rai kwa maofisa na askari wote jeshini kuiga mfano wa Sajinitaji Simbu kwa kufanya kazi kwa bidii na kuleta mafanikio katika kila idara jeshini.