Na AMINA KASHEBA
WAWAKILISHI watatu wa nchi katika michuano ya kimataifa, leo wanashuka dimbani katika viwanja tofauti kuwania nafasi ya kucheza hatua ya pili ya mtoano.
Wawakilishi hao ni Yanga ya Dar es Salaam na Mlandege ya Zanzibar zinazoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) pamoja na Singida Black Stars kutoka Singida iliyopo katika Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC).
Katika ratiba hiyo, Yanga itarudiana na Wiliete de Benguela ya Angola katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam (Saa 11:00 jioni) wakati Mlandege ikicheza na Ethiopian Coffee ya Ethiopia katika Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja (Saa 10:15 jioni).
Yanga itaingia katika mtanange huo ikiwa na mtaji wa mabao 3-0 wakati Mlandege ikiwa imefungwa mabao 2-0 katika mechi ya kwanza.
Katika CAFCC, Singida Black Stars itachuana na Rayon Sports saa 1:00 usiku katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam huku ikiwa na mtaji wa bao 1-0 iliyoupata ugenini nchini Rwanda.
Akizungumza maandalizi ya mchezo wa leo, Kocha wa Yanga, Romain Folz, alisema amejipanga vizuri kupata ushindi ambao utaisogeza mbele miamba hiyo katika hatua ijayo.
"Mchezo utakuwa mgumu lakini wachezaji wangu wamejipanga kuhakikisha tunapata ushindi ambao utatuweka katika nafasi nzuri katika michuano," alisema.
Kocha huyo alisema ana imani na kikosi chake kutokana na kila mchezaji wake kuwa bora, hivyo anawaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi katika mchezo huo.
Kocha Mkuu wa Wiliete, Bruno Ferry alisema mchezo huo utakuwa mgumu lakini wamejipanga vizuri kupata matokeo ambayo yatawaweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele.
"Tuna uwezo wa kucheza vizuri zaidi ya mechi ya kwanza, tumeshatambua makosa yetu hivyo tutapambana kuhakikisha tunapaata matokeo," alisema.
Wakati huo huo , Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe aliwataka mashabiki waklabu hiyo kujitokeza kwa wingi katika mchezo huo muhimu licha ya kupata ushindi mkubwa katika mechi ya kwanza.
Katika mchezo huo viingilio vitakuwa ni sh. 3,000 katika eneo la mzunguko, VIP C sh. 10,000, VIP B sh. 20,000 na VIP A itakuwa sh. 30,000.