MUSSA YUSUPH
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi, itatekeleza ujenzi wa barabara ya haraka kutoka Kibaha – Chalinze – Morogoro na utafanyika kwa awamu.
Dk. Samia aliyasema hayo, alipohutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa kampeni za Uchaguzi Mkuu katika Uwanja wa Sabasaba mjini Kibaha mkoani Pwani na kusema kuwa, anatambua mahitaji ya miundombinu hiyo kwa sababu ya msongamano wa magari katika barabara ya Morogoro kutokana na wembamba wa barabara hiyo.
Alisema kwa kushirikisha sekta binafsi kupitia ubia na serikali, utatekelezwa ujenzi wa barabara ya haraka kutoka Kibaha – Chalinze – Morogoro itakayojengwa kwa awamu.
Alieleza kuwa, barabara hiyo, ina tija kubwa kiuchumi, hivyo kupitia njia ya PPP, fedha za serikali ziende katika miradi mingine ya huduma za jamii.
“Tutaijenga barabara ya Bagamoyo – Mlandizi – Manelomango yenye urefu wa kilometa 100 kwa awamu ya kwanza, tumeingia makubaliano na mkandarasi kujenga kilometa 23 kuanzia Mlandizi hadi Stesheni ya SGR Ruvu,”alisema.
Alieleza kuwa, tayari usanifu unaendelea kwa upanuzi wa barabara kutoka Mailimoja hadi Picha ya Ndege, iwe na njia sita za magari na mbili za mwendokasi.
Vilevile, alisema serikali itaboresha mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 71, uboreshaji barabara kilometa 17 katika mji huo.
“Tumeanza ujenzi wa barabara ya TAMCO Kibaha hadi Mapinga Bagamoyo, ambayo kilometa zote 23 zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi na mwakani, tutakamilisha ujenzi huu,” alisisitiza.
Dk. Samia, alisema serikali imeanza ujenzi wa barabara ya Utete – Nyamwage, ambayo itazidi kufungua mkoa huo.
Aliahidi katika miaka mitano ijayo, serikali itakamilisha barabara ya Dar es Salaam – Kibiti – Mingoyo yenye urefu wa kilometa 487.
Katika jitihada za kuboresha mazingira ya biashara kwa wafanyabiashara na wawekezaji, alisema serikali itajenga soko la kisasa eneo la Lolindo kwa gharama ya sh. bilioni 18.
“Tutandeleza ujenzi wa stendi Kibaha vijijini na tutaangalia uwezekano wa stendi ya kusini,” alisema.
Dk. Samia alisema kazi kubwa imefanyika kuimarisha ushirika na kuwa, sasa vyama hivyo vimeimarika vyema.