MUSSA YUSUPH
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema kama CCM ikipewa ridhaa ya kuliongoza taifa, serikali yake imejipanga kujenga mtandao wa gesi kutoka Kinyerezi hadi Chalinze mkoani Pwani.
Amesema mtandao huo wa nishati ya gesi, utakuwa na matoleo kuelekea maeneo ya uwekezaji ya TAMCO, Zegereni, Kwala na Bagamoyo, kwa sasa mkandarasi mshauri, anaendelea kufanya tathmini ya njia ya kupitisha bomba hilo.
Dk. Samia, aliyasema hayo alipohutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa kampeni za Uchaguzi Mkuu katika uwanja wa Sabasaba mjini Kibaha mkoani Pwani.
Aliongeza kuwa ujio wa gesi utazidi kuvutia uwekezaji mkoani Pwani kwani viwanda vitaendeshwa kwa gharama nafuu zaidi na bidhaa zitakazozalishwa zitapungua bei.
Dk. Samia, alisema miongoni mwa ahadi katika ilani ya CCM ni kuchukua hatua kupunguza gharama za vifaa vya ujenzi nchini, kuwezesha wananchi wa kipato cha chini, kujenga nyumba bora za kisasa kwa gharama nafuu.
Alibainisha kuwa, mwelekeo wa serikali ni kuendeleza mpango wa ujenzi makazi bora kwa bei nafuu.
Vilevile, alisema serikali yake, itaendelea kuboresha makazi mijini kwa kuhakikisha makazi, nyumba na majengo yote yanarasimishwa kwa kupimwa, kupangwa na kumilikishwa.
Kuhusu miradi ya maji, alisema serikali imeendelea kutoa fedha katika mkoa huo, kuhakikisha miradi mbalimbali ya maji inakamilishwa
“Katika kukabiliana na changamoto ya maji tulileta sh. bilioni 187.3 katika mkoa huu. Alibainisha kuwa, miradi hiyo, imeanza kutekelezwa itakayohudumia kata 53 za Wilaya ya Rufiji, Kibiti, Mkuranga na Kisarawe.
Pia, alisema mradi wa maji Kwala, utanufaisha maeneo ya Kwala, Bandari Kavu na maeneo ya viwanda.
Alisema mradi wa maji Pangani, utatatua changamoto ya maji Kata ya Pangani na maeneo ya Msufini, Lulanzi na TAMCO.
Mbali na miradi hiyo, alisema miradi mingine midogo yenye kuhusisha upanuzi wa mtandao wa maji kutoka Mlandizi, Bokomlegela, Janga, Mtongani na Kawawa itatekelezwa.
Alisema serikali itajenga mradi wa maji katika eneo la viwanda wenye gharama ya sh. bilioni 10.9, ambao utanufaisha maeneo tofauti ya mkoa huo.