Na MUSSA YUSUPH,
Arusha
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema katika miaka mitano ijayo, serikali itaendelea kuimarisha maslahi ya walimu.
Pia, amesisitiza atandelea kujenga mabweni, kuongeza vifaa vya kufundishia na kujifunza kwa wenye ulemavu.
Amesisitiza kuwa, hakuna yeyote atakayeachwa katika mageuzi yanayofanyika katika sekta ya elimu nchini, kwani mkakati wa serikali ni kukuza kiwango cha elimu nchini.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni za Uchaguzi Mkuu katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Dk. Samia, amesema serikali itaendelea kutekeleza mpango wa kutoa elimu bila ada.
“Serikali itaendelea kujenga miundombinu ya elimu kwa kuhakikisha maslahi ya walimu, nyumba za walimu, vifaa vya kufundisha na kufundishia vinapatikana kukuza elimu nchini. “Kama mnavyojua, tumebadilisha mitaala ya elimu, nasi tunajipanga kuendana na mabadiliko ya mitaala.
“Hata kwa wale wenye mahitaji maalum serikali imejipanga vizuri, elimu yao sasa haina shida kuna mabweni kwa ajili yao na vifaa vya kusomea tumejiandaa navyo. Kwa hiyo kama tulivyoelekezwa na maazimio ya kimataifa ya malengo ya milenia hasiachwe mtu nyuma, nasi Tanzania hatutaki kumuacha nyuma katika elimu, afya, upatikanaji maji safi, umeme na kote hatutaki kumuacha mtu nyuma,” amesisitiza.
Kwa upande wa elimu mkoani Arusha, alisema serikali imetumia sh. bilioni 267 katika sekta ya elimu mkoani hapo fedha ambazo zimetumika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.
Pia, amesema serikali imejenga vyuo vya ufundi stadi (VETA) kila wilaya lengo kuwawezesha vijana waweze kupata ajira au kujiajiri.
“Lengo la vyuo vya ufundi ni kuwaandaa vijana waweze kujajiri na kuajirika. Nimetaja miradi mikubwa inayopita huku (Arusha) kuna reli inakuja inataka mafundi umeme na kuunganisha vyuma ili reli ikija ikute vijana wameshasomeshwa,” ameeleza.
UJENZI WA BARABARA
Katika mkutano huo uliofurika maelfu ya wananchi, Dk. Samia alisema serikali itakamilisha miradi yote ya barabara inayoendelea na ile mipya ambayo imeahidiwa katika ilani ya uchaguzi.
Alitaja miongoni mwa barabara hizo ni Malula – Ngarenanyuki ambayo imetengewa sh. bilioni 30 na barabara ya Tengeru – Mbuguni – Mererani yenye urefu wa kilometa 24 ambayo upembuzi yakinifu umekamilika.
Vilevile, alisema barabara nyingine ni Mto wa mbu – Selela yenye urefu wa kilometa 23 ambapo mkataba upo mbioni kusainiwa ili mkandarasi anze kazi huku barabara ya Selela – Engaruka yenye urefu wa kilometa 27 tayari upembuzi yakinifu umekamilika.
“Barabara ya Engaruka – Ngaresero (kilometa 24) usanifu umekamilika, kazi inayosubiriwa ni kutangaza zabuni apatikane mkandarasi aanze kujenga. Kwa upande wa Karatu kuna ujenzi wa lami kilometa 10.
Aliongeza: “Nafahamu mahitaji ya maboresho ya barabara za ndani ya Jiji la Arusha ambapo jiji hilo limejumuishwa katika mradi wa TACTIC ambapo jumla ya kilometa 10.2 zitajengwa kwa kiwango cha lami. Oljoro kilometa 4.7, Engosheraton kilometa 4.8, Olasiti kilometa 4 ambazo zitajengwa ili Jiji la arusha lipate hadhi yake hasa ukizingatia watalii zaidi wanakuja, reli ya kisasa itakuja hivyo lazima jiji hili liwe na mtandao wa barabara za lami.”
Akizungumzia upatikanaji huduma za afya, alisema huduma hizo zimeimarika zaidi kwani hospitali ya mkoa huo imefungwa vifaa vya kisasa vikiwemo vipimo vyenye uwezo wa kupima saratani ya matiti.
Alibainisha kuwa mgonjwa atakayepatikana kupata maradhi hayo hatolazimika kwenda Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam bali atatibiwa katika Hospitali ya KCMC.
“Tumejenga bunker (nyumba maalum) ya mionzi na inatibu kama wanavyotibiwa Ocean Road. Kwa hiyo wakazi wa Kanda ya Kaskazini hongereni sana,” alisema Dk. Samia.
SEKTA YA MADINI
Dk. Samia alisema serikali imeendelea kuweka msisitizo kuimarisha sekta ya madini kwa kuweka lengo la ifikapo mwaka 2025 mchango wa madini katika pato la taifa ufikie asilimia 10.
“Tulifikia lengo kabla ya kufika 2025. Niwajulishe kwamba lengo lililofikiwa ni asilimia 10.1 ya pato la taifa kwa mwaka jana ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya kipindi tulichojiwekea. Tumeanza kuyatumia madini kuimarisha uwezo wetu wa kujitegemea kiuchumi, tumeanza kuweka akiba yetu ya dhahabu ndani ya benki kuu na akiba imekuwa mwezi hadi mwezi na ndiyo maana shilingi yetu imeendelea kuwa madhubuti.
Pia, alisema serikali imechukua hatua kuhakikisha Tanzania inanufaika zaidi kupitia madini ya Tanzanite kwa kuweka kituo cha uuzaji pamoja madini hayo eneo la Mirarani.
Vilevile, alisema serikali imeanzisha minada ya vito ambapo mnada wa kwanza ulifanyika Mirerani na mnada wa pili ulifanyika mkoani Arusha ambayo imeitangaza vyema katika biashara ya vito.
Alisema endapo akipewa ridhaa ya kuliongoza taifa, serikali yake itahamasisha zaidi shughuli za uongezaji thamani madini ili manufaa zaidi yapatikane ikiwemo ajira kwa vijana.
Kadhalika, alisema kupitia Kituo cha Jiolojia Tanzania (GST) serikali itaongeza kasi ya utoaji mafunzo kuhusu uongezaji thamani madini kwa viwango vinavyokubalika kimataifa.
“Nchi yetu tumepima madini yote yanayochimbwa nchi nzima ni eneo la asilimia 16 ndilo limepimwa, tuna lengo miaka mitano ijayo kupima tena asilimia 18 hadi 20 ya nchi kubaini madini tuliyonayo na tuwaalike wataalamu waje tuone namna ya kuchimba madini hayo ili kukuza ajira kwa vijana,” alibainisha.
Kwa upande wake, Mgombea Ubunge Jimbo la Arusha Mjini, Paulo Makonda, alimuomba Dk. Samia kuendeleza mikakati ya kufufua viwanda na kuboresha miundombinu ya barabara jijini Arusha.
Alisema Arusha inahitaji kurejea katika hadhi ya Jiji la viwanda huku akiiomba serikali kufufua kiwanda cha General Tire ili vijana wa Arusha wapate ajira kupitia uzalishaji wa matairi.
“Vijana wa Arusha ni wachapakazi. Tunaomba tufufue General Tire ili tairi zitengenezwe tena hapa nyumbani, hilo ni ombi kubwa la wananchi wa Arusha. Mama Samia umetuwezesha Arusha, miradi iliyokwama muda mrefu umeisimamia, leo tuna ujenzi wa standi mpya na soko jipya kupitia maelekezo yako. hizi zote ni kura zako,” alisema Makonda.
Naye, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Ubungo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, alisema Watanzania wanapaswa kumchagua tena mgombea urais wa CCM, Dk. Samia kwa kuwa ameonyesha uwezo mkubwa wa kulinda amani na mshikamano wa Taifa.
“Kigezo cha kwanza cha kiongozi ni kulinda amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa, maana hayo ndiyo msingi wa maendeleo. Katika miaka minne na nusu hakuna shaka kwamba Rais Samia ameweza kulinda na kudumisha umoja wa Taifa letu,” alieleza.
Aliongeza kuwa Rais Dk. Samia amesaidia wananchi kwa kudhibiti bei za bidhaa za msingi ikiwemo mchele, mahindi na maharage ambazo zimebaki katika viwango vya kawaida kwa kipindi cha miaka minne mfululizo.
“Wakati mafuta yalipopanda bei duniani hadi kufikia sh. 4,000 kwa lita, Rais Samia alitoa ruzuku ya sh. bilioni 100 kuhakikisha bei inabaki pale pale. Hakuna Rais mwingine aliyefanya hivyo Afrika,” alisema.