Na MUSSA YUSUPH,
Moshi
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, ametangaza kuwa, serikali ipo katika hatua za mwisho kuanza utekelezaji mradi wa kihistoria wa Liganga na Mchuchuma.
Amesema utekelezaji mradi huo, utakaohusisha uchimbaji madini ya chuma na makaa ya mawe, utachochea zaidi ukuaji wa sekta ya viwanda kwa upatikanaji malighafi za kutosha.
Dk. Samia, amesema ataingia katika rekodi ya kuwa Rais wa kwanza kutekeleza ndoto hiyo ya muda mrefu, ataiweka Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa kinara Afrika kwa uzalishaji chuma.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Mashujaa wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro, Dk. Samia, amesema mradi huo, utaongeza kasi ya maendeleo ya viwanda.
“Hili tunalisema kwa uhakika kwa sababu, tayari tupo katika mazungumzo ya mwisho kabisa kuanza kazi mgodi wetu wa Mchuchuma na Liganga. Mgodi wenye chuma nyingi na makaa ya mawe mengi.
“Tupo katika hatua za mwisho mgodi ule ndiyo utakaolisha viwanda vingine kama cha Kilimanjaro Tools,” alisisitiza Dk. Samia huku akishangiliwa na maelfu ya wananchi waliofurika katika mkutano huo.
MKAKATI KUONGEZA WATALII
Akizungumzia sekta ya utalii, Dk. Samia, alisema mpango uliopo ni Tanzania kufikisha idadi ya watalii milioni nane.
“Wote sisi ni mashahidi. Kwa utalii, tumefungua fursa kubwa kwa vijana, tumeongeza hoteli, mapato, idadi ya waongoza watalii,”alisema.
Alisema serikali imeongeza idadi ya watalii kama ilivyolengwa katika ilani ya uchaguzi ifikie milioni tano kwa watalii wa ndani na nje.
Alibainisha kuwa, baada ya mafanikio hayo, lengo la sasa ni kufikisha idadi ya watalii milioni nane kwa mwaka.
UTEKELEZAJI MIRADI
Dk. Samia, alisema serikali imefanya uboreshaji mkubwa katika Hospitali ya Mawenzi, ambapo alikwenda kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la kinamama na watoto.
Alibainisha kuwa, jengo hilo ambalo limeshakamilika, limeanza kutoa huduma kwa wananchi.
Alisisitiza kuwa, uwepo wa jengo hilo, umewezesha idadi ya kinamama kuongezeka kupata huduma ya kujifungua katika hospitali.
“Idadi ya kinamama wanaokwenda hospitali, imeongeza kutoka 260,486 hadi 328,502. Kwa kiasi kikubwa tumepunguza vifo vya kinamama wakati wa kujifungua na hizi jitihada zitaendelea ili twende vizuri.
“Zaidi hospitali yetu ya rufaa ina huduma za wagonjwa mahututi, watoto njiti na kusafisha figo huduma ambazo awali hazikuwepo katika mkoa huo,” alisisitiza.
Pia, alieleza katika hospitali hiyo, kuna vifaa vya kisasa ambavyo ni CT Scan na X- Ray inayomfuata mgonjwa badala ya mgonjwa kupanga foleni kusibiri huduma hiyo.
Alieleza kuwa, kuna huduma za MRI ambazo zinapima magonjwa ya ndani hivyo mkoa huo umejitosheleza kwa huduma za afya.
Vilevile, alisema kwa kushirikiana na hospitali za kidini ikiwemo KCMC, serikali imefanikisha kujenga jengo la mionzi litakalotoa tiba ya maradhi ya saratani.
“Kwa sasa mtu wa Kilimanjaro hana haja kwenda Ocean Road Dar es Salaam. Matibabu ni hapahapa Kilimanjaro,” alieleza.
Dk. Samia alisema katika miaka mitano ijayo, serikali yake itaendeleza utoaji huduma hizo na kukamilisha uboreshaji wa hospitali za Moshi, Mwanga na Rombo.
Alisema upatikanaji dawa katika mkoa huo, umefikia asilimia zaidi ya 80 huku dawa muhimu ambazo lazima ziwepo hospitalini zinapatikana.
MAJI
Kuhusu upatikanaji maji, alisema katika Wilaya ya Hai, serikali imekamilisha mradi wa maji kutoka Uroki – Bomang’ombe – Kikafu kwa gharama ya sh. bilioni 3.3.
Kwa upande wa Rombo, alisema serikali inatekeleza mradi wa sh. bilioni 9.8 kutoa maji Ziwa Chala kwenda Rombo.
Kuhusu wilayani Siha, alibainisha kuwa, serikali inatekeleza mradi wa sh. bilioni 14 kupeleka maji vijiji vinane.
ELIMU
Akizungumzia elimu, alisema serikali itajenga kampasi ya Chuo cha Biashara CBE wilayani Hai, ambacho kitatoa fursa ya mafunzo ya elimu na kuimarisha uchumi wa eneo hilo.
Pia, alisema tayari serikali imetenga fedha kujenga kilometa 17 za barabara kupitia programu za TACTIC ambayo nayo itatekelezwa katika wilaya hiyo.
MOSHI VIJIJINI
Kuhusu Moshi Vijijini, alieleza kuwa, serikali itakamilisha barabara za Moshi International School – Kibosho kati – Kwa Raphael yenye urefu wa kilometa 13.
Kadhalika, alisema barabara ya Kidia – Udizini yenye urefu wa Kilometa 10, barabara ya Mambo leo – Shimbwe yenye urefu wa kilometa 10.3 na barabara ya Rau – Madukani – Mamboleo – Materuni (Kilometa 10).
JIMBONI VUNJO
Kwa jimbo la Vunjo, alisema serikali itakamilisha barabara ya Mbofa yenye urefu wa kilometa 10 ambayo inategemewa na wananchi katika hospitali ya Kilema, chuo cha Mandaka na lango la watalii wanaoshuka Mlima Kilimanjaro.
“Kuna barabara ya kipekee ya Uchira – Kisomati yenye urefu wa kilometa 10.8 ambacho kilichotofautisha mradi huu na mwingine ni wananchi walianza kujenga kwa nguvu zao baadaye serikali tukaingia,” alieleza.
Alisema serikali itakamilisha ujenzi wa barabara ya Holili – Tarakea yenye kilometa 53 ambayo ni ya kimkakati katika kukuza biashara mpakani.
Kuhusu viwanda, alisema awali mji wa Moshi ulikuwa na viwanda vingi vya kimkakati ambavyo baada ya ubinafsishaji vingi vilishindwa kuendelea.
Hivyo, alisema atahakikisha viwanda vinafanyakazi kwa kuwatafuta waendeshaji wengine vikiwemo vyama vya ushirika.
Pia, alisema serikali imefufua kiwanda cha Kilimanjaro Machine Tools kilichosimama kwa zaidi ya miaka 30 ambapo tayari kinatoa huduma kutengeneza vifaa vya viwanda.
PROFESA KITILA MKUMBO
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Ubungo Jijini Dar es Salaam, Profesa Kitila Mkumbo, alimtaja Dk. Samia kuwa ni kiongozi mwanamageuzi.
Profesa Kitila ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, alisema kwa uwezo wa Dk. Samia, wananchi wa mkoa huo, wana kila sababu ya kumchagua Oktoba 29, mwaka huu.
Alitaja sababu nne za kumpa kura za kishindo Dk. Samia kuwa ni kutumia falsafa ya 4R, kuifungua nchi, kufungua utalii na kukuza uchumi.
WAGOMBEA UBUNGE
Mgombea Ubunge Jimbo la Rombo, Profesa Adolf Mkenda, alieleza kuwa miradi ya kimkakati imefanyika katika jimbo hilo.
Alisema Dk. Samia ametoa sh. bilioni 8.6 za kutekeleza mradi wa maji kutoka Ziwa chala ambao utasambaza maji katika vijiji zaidi ya 30.
Naye, mgombea Ubunge Jimbo la Vunjo, Enock Koola, alisema jimbo hilo limepokea zaidi ya sh. bilioni 50 kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.
Hata hivyo, Koola aliomba ujenzi barabara ya Chekereni – Kahe – Mabodini huku akitilia msisitizo utekelezaji wa miradi ya maji.
Mgombea Ubunge Moshi Mjini, Ibrahim Shayo, alisema wananchi wa jimbo hilo, watakwenda kumpigia kura za kishindo Dk. Samia.
Alieleza kuwa, zaidi ya sh. bilioni 238 zimetumika katika afya, miundombinu na elimu kupitia ujenzi wa shule za msingi na sekondari.
Mgombea Ubunge Viti Maalum, Ester Maleko, alisema kwa kazi kubwa iliyofanyika katika sekta ya afya, vifo vya kinamama na watoto wachanga vimepungua.