Na NASRA KITANA
BAADA ya kuondolewa katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, Kocha wa Simba, Steve Barker amesema sababu ya kupoteza bao 1-0 katika mchezo dhidi ya Azam FC ni kuwachelewa kambini kwa wachezaji wake, mashabiki wameonekana kuchukizwa na kiwango cha kikosi hicho.
Simba, ilikubali kufungwa bao 1-0 dhidi ya Azam, katika mchezo wa nusu fainali uliofanyika Uwanja wa Amaan Complex, Zanzibar.
Aliwataja baadhi ya wachezaji waliochelewa kuingia kambini kujiandaa na Kombe la Mapinduzi ni Jean Ahoua, Elie Mpanzu na Jonathan Sowah.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Kocha Barker alisema kuwa mbali na hilo wachezaji wake walitengeneza nafasi lakini walishindwa kuzitumia ipasavyo kupachika mabao.
Alisema kuwa lengo lao lilikuwa ni kupata matokeo mazuri na kutinga fainali ya michuano hiyo msimu huu, lakini ilishindikana.
Alisema anakwenda kukisuka vyema kikosi chake kwa maandalizi ya michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL).
Kocha huyo alisema kuwa siku chache alizokaa na kikosi chake ameona nini anatakiwa kuanza nacho ili aweze kukijenga na kuwa bora kwa ajili ya mashindano yajayo.
“Tumepoteza lakini sababu kubwa ni baadhi ya wachezaji kushindwa kuingia kambini kwa wakati kipindi cha kufanya maandalizi.
“Pia tulitengeneza nafasi lakini tulishindwa kuzitumia ipasavyo kupachika mabao wavuni, tunakwenda kujipanga upya kuhakikisha tunafanya vyema katika michuano ya Ligi na CAFCL,” alisema.
Naye Kocha wa Azam FC, Florent Ibenge alisema kuwa haikuwa rahisi kuifunga Simba, hivyo anawapongeza vijana wake kwa kazi kubwa waliyoifanya.
Alisema kuwa licha ya kukutana na ugumu katika mchezo huo lakini walibaki katika malengo yao ambayo wameyatimiza na hivi sasa watapambana kubeba taji.
“Ilikuwa mechi ngumu, kwani haikuwa rahisi kupata ushindi mbele ya Simba lakini niwapongeze wachezaji wangu kwa kazi kubwa waliyoifanya hadi kufikia malengo ya kutinga fainali ya mashindano haya,” alisema Ibenge.
Wakati kocha wa Simba akijitetea, mashabiki wa klabu hiyo wamesisitiza kwamba hawajaridhishwa na kiwango cha wachezaji wao.
Shabiki aliyejitambulisha kwa jina la Dokta Moo alisema kuwa, amechukizwa na kipigo walichokipata kutoka Azam FC kwani wamefungwa na wachezaji vijana wa U20.
Alisema kuwa katika kikosi cha Azam wachezaji wachache walitoka kikosi cha kikubwa huku kikijumuisha wengi wa U20, hivyo hajaridhishwa na kiwango cha Simba katika michuano hiyo.
“Bado tuna safari kubwa ndani ya kikosi chetu, tuliingia katika mchezo huo wachezaji wakionekana hawapo tayari kwa ajili ya ushindi, sijaridhishwa na timu, tunahitaji mabadiliko makubwa na ya haraka,” alisema Dokta Moo.
Naye baba mzazi wa Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, ambaye ni shabiki wa Simba, Shabani Kamwe alisema kuwa hali ni mbaya ndani ya kikosi chao bado wanahitaji kujipanga zaidi ili kushinda katika mechi kubwa.
Alisema kuwa timu yao haina muunganiko unaoweza kusababisha wachezaji kupambana na kupata matokeo mazuri hasa katika mechi kubwa.
“Kikosi chetu bado hakipo vizuri, tunahitaji uboreshaji mkubwa kwa hali kikosi kilivyo hatuwezi kufika mahali popote.
“Hatuna muunganiko wa wachezaji wanaoweza kupambana kuamua matokeo chanya, tunahitaji suluhisho la mapema ili kuinusuru timu yetu msimu huu,” alisema.
Azam msimu huu imetinga fainali ya michuano hiyo kwa mara saba baada ya 2012, 2013, 2017, 2018, 2019, 2022 na sasa 2026.
Katika misimu saba imebeba mataji matano mwaka 2012, 2013, 2017, 2018 na 2019.




