Na MUSSA YUSUPH
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), amehitimisha kampeni zake katika mikoa ya kaskazini.
Mikutano aliyofanya, imevutia hisia kubwa kutoka kwa wananchi baada ya Dk. Samia kutoa ahadi 10, ambazo zimelenga kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi yatakayogusa maendeleo ya watu, kupitia sekta za miundombinu, utalii, kilimo na viwanda.
Katika mikutano hiyo iliyofanyika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha kisha kuhitimisha mkoani Manyara, Dk. Samia, alisisitiza kuwa, lengo kuu la serikali yake, pindi atakapopewa ridhaa ya kuliongoza taifa, ni kujenga uchumi jumuishi wenye kugusa maisha ya kila Mtanzania.
Ili kutimiza lengo hilo, Dk. Samia, ametoa ahadi 10 katika mikutano yake ya kampeni, ambazo ni mkakati wa ujenzi wa viwanda na miundombinu, kuongeza idadi ya watalii, ujenzi mji wa AFCON, utekelezaji mradi wa Liganga na Mchuchuma.
Zingine ni mkakati wa kujitosheleza kwa ngano, viwanda na mashamba yaliyobinafsishwa, uvuvi, upimaji maeneo ya madini, uboreshaji maslahi ya walimu na nchi kutokopa mikopo yenye masharti magumu.
TANGA YA VIWANDA NA UJENZI WA RELI
Katika mkutano huo uliofanyika Uwanja vya Usagara jijini Tanga, Dk. Samia, amesema endapo akipewa ridhaa ya kuliongoza Taifa, amedhamiria kurejesha hadhi ya mkoa huo kuwa wa viwanda.
Katika kuthibitisha hilo, Dk. Samia, ametangaza mikakati ya kujenga reli ya kisasa yenye urefu wa kilometa 1,108 kutoka Tanga – Arusha hadi Musoma, ambayo itaunganishwa na Bandari ya Tanga.
“Tutaanza utekelezaji mradi wa reli, kuunganisha Bandari ya Tanga kuelekea Arusha hadi Musoma, takriban kilometa 1,108.
“Reli hii, itafungua maeneo ya viwanda na madini, hivyo kuongeza fursa za ajira ndani ya Mkoa wa Tanga.
Alisema reli hiyo ni sehemu ya mpango wa maboresho ya Bandari ya Tanga, kuwa eneo maalumu la bohari ya mafuta na gesi.
“Bandari ya Tanga inakwenda na maamuzi tuliyoyafanya kuwa Tanga ni bohari ya mafuta na gesi, hilo litachangia kuzalisha ajira nyingine 2,100. Hili linakwenda kunyanyua uchumi wa wanatanga.
“Mbali na mradi huu, tuna miradi mingine ya kimkakati inayofungamana na bandari hii. Mojawapo ni bomba la mafuta kutoka Hoima hadi Chongoleani.
Alisisitiza: “Mradi ambao umekamilika kwa asilimia 84 na umeleta manufaa mengi sana kwa mfano, tayari eneo la Chongoleani pekee, watu 1,300 wameajiriwa katika mradi huu na ndani ya Wilaya ya Tanga, watu 2,000 wameajiriwa.”
Mbali na ujenzi huo, alisema serikali kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), zitashirikiana kujenga barabara ya Handeni – Singida.
“Barabara ya Handeni – Singida, hii nayo tumeiunganisha kwa sababu watakaojenga bandari ni wenyewe TPA kwa sababu ya urahisi kusafirisha mizigo yao. TANROADS watashirikiana na bandari kujenga barabara hiyo,” alisisitiza.
MJI WA AFCON
Kwa upande wa michezo, Dk. Samia, alitangaza serikali inatarajia kujenga mji wa kisasa wa Mashindano ya Soka kwa nchi za Afrika (AFCON 2027), mkoani Arusha ambao utachochea sekta ya michezo na utalii katika jiji hilo.
Mji huo, utajengwa katika eneo linalojengwa uwanja wa kisasa wa soka mkoani hapa utakaotumika katika michuano ya soka barani Afrika, inayotarajiwa kutimua vumbi mwaka 2027.
“Tunajenga uwanja wa AFCON kwa mashindano ya AFCON, uwanja unakwenda kuwa kivutio cha utalii, kwa sababu eneo lilipo uwanja huo, tutajenga AFCON City ambao ni mji maalumu wa AFCON.
Alieleza: “Mji wa AFCON utakuwa pale, uwanja ule tumeshaukamilisha kwa asilimia 63, utakapokamilika utabeba watu 32,000.
“Hivyo, tunatarajia Julai mwakani, uwanja utakuwa tayari. Lakini tutaendelea na awamu ya pili kujenga Mji wa AFCON.”
KUONGEZA IDADI YA WATALII
Kuhusu watalii, Dk. Samia, alisema mkakati wa serikali yake katika kipindi cha miaka mitano ijayo, ni kuongeza idadi ya watalii kufikia milioni nane.
Dk. Samia, aliyasema hayo katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Mashujaa mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
“Wote sisi ni mashahidi. Kwa utalii, tumefungua fursa kubwa kwa vijana, tumeongeza hoteli, mapato, idadi ya waongoza watalii, lakini tumefungua ajira nyingi kwa vijana kupitia utalii,” alieleza.
Dk. Samia, alisema serikali imeongeza idadi ya watalii kama ilivyolengwa katika ilani ya uchaguzi ifikie milioni tano kwa watalii wa ndani na nje.
Alibainisha kuwa baada ya mafanikio hayo lengo la sasa ni kufikisha idadi ya watalii milioni nane kwa mwaka.
MRADI WA LIGANGA NA MCHUCHUMA
Mgombea Urais kupitia CCM, Dk. Samia, alitangaza kuwa serikali ipo katika hatua za mwisho, kuanza utekelezaji mradi wa kihistoria wa Liganga na Mchuchuma.
Alisema utekelezaji mradi huo utakaohusisha uchimbaji madini ya chuma na makaa ya mawe, utachochea zaidi ukuaji sekta ya viwanda kwa upatikanaji malighafi za kutosha.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika uwanja wa Mashujaa wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro, Dk. Samia alisema mradi huo utaongeza kasi ya maendeleo ya viwanda.
“Hili tunalisema kwa uhakika kwa sababu tayari tupo katika mazungumzo ya mwisho kabisa kuanza kazi mgodi wetu wa Mchuchuma na Liganga. Mgodi wenye chuma nyingi sana na makaa ya mawe mengi.
“Tupo katika hatua za mwisho mgodi ule ndiyo utakaolisha viwanda vingine kama cha Kilimanjaro Tools,” alisisitiza Dk. Samia huku akishangiliwa na maelfu ya wananchi waliofurika katika mkutano huo.
MIKOPO YA MANYANYASO
Kuhusu mikopo, Dk. Samia, alisema serikali yake, itaongeza wigo wa ukusanyaji mapato ya kodi, lengo likiwa kuindolea nchi manyanyaso yatokanayo na mikopo.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro, alisisitiza kuwa, serikali itakopa mikopo ambayo itaheshimu uhuru wa nchi.
“Kila tulichokiweka mle (ilani ya uchaguzi), tunajua fedha ya utekelezaji inatoka wapi lakini nataka niwaambie lingine tumeongeza makusanyo ya mapato.
Alisisitiza: “Tunaendelea kuongeza makusanyo ya mapato ndani ya nchi yetu kuepuka manyanyaso ya mikopo na misaada.
“Tunajua hakika fedha zinatoka wapi. Tutakopa ndiyo, lakini mikopo ambayo itaheshimu uhuru wa nchi yetu ndiyo tutakayokopa.”
MASHAMBA NA VIWANDA VILIVYOBINAFSISHWA
Dk. Samia, alitangaza kufanya mabadiliko makubwa pindi atakapopewa ridhaa ya kuliongoza taifa, yatakayogusa mashamba na viwanda vilivyobinafsishwa.
Mashamba na viwanda ambavyo vitaguswa ni yale ya chai na mkonge ambayo yamebinafsishwa, lakini wawekezaji wameshindwa kuyaendeleza.
Katika kuthibitisha hilo, Dk. Samia alitoa maagizo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wizara ya Katiba na Sheria, kupitia upya mikataba ya ubinafsishaji maeneo hayo na ile itakayobainika kukiukwa itavunjwa.
Alsema lengo la hatua hiyo ni kuiwezesha serikali na vyama vya ushirika kuyaendeleza mashamba na viwanda hivyo ili viongeze tija ya uzalishaji mazao kwa wakulima.
Dk. Samia alitoa maagizo hayo katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika mjini Korogwe mkoani Tanga, jana.
NEEMA KWA WAVUVI
Akiwa wilayani Babati, Dk. Samia Suluhu Hassan, alitangaza neema kwa wavuvi nchini yenye lengo la kuwaondolea vikwazo katika shughuli zao.
Alisema ili kuongeza kasi ya uvuvi nchini, serikali imetenga fedha kununua mitambo ya kuondoa magugu katika mito na maziwa yote nchini.
Mpango huo ni sehemu ya utekelezaji Ilani ya Uchaguzi ya CCM, inayosisitiza serikali kuja na mpango wa matumizi bora ya bahari na maji baridi, kuleta manufaa kwa wananchi.
Alisema katika Ilani ya uchaguzi ya CCM kifungu cha 26 (1) inasema; serikali itatekeleza mpango wa matumizi maeneo ya bahari na maji baridi kwa kushirikiana na wananchi lengo kuleta manufaa.
“Moja ya kazi hiyo ni kuondoa magugu katika maziwa mbalimbali nchini. Serikali imejipanga vyema na ilani imetuelekeza kuyafanyiakazi maeneo hayo,” alisisitiza.
MKAKATI KUONGEZA UZALISHAJI NGANO
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika wilayani Hanang mkoani Manyara, Dk. Samia aliahidi kuja na mkakati wa kuliwezesha taifa kujitosheleza kwa ngano ikiwemo serikali kuyatwaa mashamba yaliyochukuliwa na wawekezaji bila kuyaendeleza.
Pia, aliwatoa hofu wakulima wa mbaazi nchini kuhusu soko la zao hilo ambapo ametaja hatua muhimu zinazochukuliwa na serikali kuhakikisha bei ya mbaazi haishuki chini ya asilimia 70.
“Najua wakazi wa Hanang ni wakulima wazuri wa ngano na mazao mengine kama mbaazi na dengu. Lengo letu kitaifa kufikisha tani milioni moja ifikapo mwaka 2030 kutoka Hanang ili tuweze kujitegemea kwa mahitaji ya ngano,” alisisitiza.
Dk. Samia alieleza hatua zitakazochukuliwa katika kufikia lengo hilo ni kushughulikia mashamba makubwa ambayo yalitolewa kwa wawekezaji ambao hawajayaendeleza.
Hivyo, aliitaka Mamlaka ya Maeneo Huru ya Uwekezaji kuangalia upya mikataba ya uwekezaji na namna yatakavyoweza kurudishwa mashamba hayo serikalini.
UPIMAJI MAENEO YA MADINI
Kwa upande wa sekta ya madini, Dk. Samia aliahidi katika kipindi cha miaka mitano ujayo, serikali itapima asilimia 20 ya eneo la nchi kubaini aina za madini yaliyopo.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha, alisema serikali imedhamiria kuongeza mchango wa sekta hiyo katika pato la Taifa.
“Nchi yetu tumepima madini yote yanayochimbwa nchi nzima ni eneo la asilimia 16 ndilo limepimwa, tuna lengo miaka mitano ijayo kupima tena asilimia 18 hadi 20 ya nchi kubaini madini tuliyonayo na tuwaalike wataalamu waje tuone namna ya kuchimba madini hayo ili kukuza ajira kwa vijana,” alibainisha
MASLAHI YA WALIMU
Katika mikutano yake kanda ya kaskazini, Dk. Samia alitangaza neema kwa walimu ambapo alisema katika miaka mitano ijayo serikali yake itaendelea kuimarisha maslahi ya walimu huku akisisitiza atandelea kujenga mabweni, kuongeza vifaa vya kufundishia na kujifunza kwa wenye ulemavu.
Alisisitiza kuwa hakuna yeyote atakayeachwa katika mageuzi yanayofanyika kwenye sekta ya elimu nchini kwani mkakati wa serikali imedhamiria kukuza kiwango cha elimu nchini.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni za Uchaguzi Mkuu kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Dk. Samia alisema serikali itaendelea kutekeleza mpango wa kutoa elimu bila ada.
“Serikali itaendelea kujenga miundombinu ya elimu kwa kuhakikisha maslahi ya walimu, nyumba za walimu, vifaa vya kufundisha na kufundishia vinapatikana ili kukuza elimu nchini. Kama mnavyojua tumebadilisha mitaala ya elimu, nasi tunajipanga kuendana na mabadiliko ya mitaala.