Na HANIFA RAMADHANI,
Pemba
MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema yeye alikuwa mtu wa kwanza kukubaliana na marehemu Maalim Seif Sharrif Hamad, kuunda serikali ya umoja wa kitaifa kwa lengo la kuimarisha amani, umoja na mshikamano kwa wazanzibari.
Amesema katiba iliwataka kufanya hivyo, ndiyo jambo lililosababisha kuimarika kwa umoja, amani na mshikamano kwa Wazanzibari.
Dk. Mwinyi, ameyasema hayo wakati akizungumza na viongozi wa dini wa madhehebu mbalimbali katika Ukumbi wa Skuli ya Utaani, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Amesema kabla ya maridhiano hayo, Wazanzibari walikuwa siyo wamoja na wengine walishindwa kuzikana, kufanya ibada sehemu moja na wengine, waliacha wake zao kutokana na siasa za chuki na wengi walikuwa wakizungumza Unguja na Upemba na asili za watu.
“Mimi ni mtu wa kwanza kuzungumza, kukubaliana na marehemu Seif Sharif Hamad kuunda serikali ya umoja wa kitaifa, kwani katiba ilitutaka kufanya hivyo, ndiyo jambo lililopelekea kuimarika kwa umoja, amani na mshikamano uliopo mpaka leo hii,”amesema.
Amesema walikubaliana na marehemu Maalim Seif, kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na hayo ndiyo maridhiano ya kisiasa, ndiyo maana mpaka sasa kuna serikali ya umoja wa kitaifa na njia pekee ya mshikamano wao.
“Wapo waliokuwa wanatusema tena wamo humu ndani ya seriakali, lakini wakitoka nje wanatusema utadhani wao hawamo, narudia tena kusema sikilizeni sera zao, hamtosikia jambo la kisera, bali ni maneno ya ugomvi, matusi na kiubaguzi.
“Wanasahau kwamba, umoja tuliokuwa nao Wazanzibari bila ya kujali asili zetu ni jambo la msingi, kwani kila mtu ana asili yake, haiondoi uzanzibari wetu,” amesema.
Amesema Serikali ya CCM, inazungumzia amani ndiyo maana nchi inaendelea kupiga hatua za maendeleo.
Amesema viongozi wakisimama kuwachagua, wanajivunia kuwa wamoja, kwani awali watu walikuwa wakizungumzia ukabila.
Amesema mambo yote, yanaanza na amani, kwani sehemu yoyote bila ya amani, hakuna jambo linalofanyika na watahangaika kurudisha amani.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Dk.Mohammed Said Mohammed Dimwa, alisema ndani ya miaka mitano aliyopewa ridhaa, Dk.Mwinyi ameibadilisha Zanzibar kwa kiasi kikubwa.
Amesema hayo yote ni kwa sababu, Dk.Mwinyi ni kiongozi mwenye hofu ya Mungu, mwandilifu, asiyependa makuu, mpenda amani na mwenye dhamira njema ya kuwatumikia wananchi.
Amesema miaka mitano ya uongozi wake, Dk.Mwinyi, miongoni mwa jambo kubwa alilofanya ni suala zima la kutunza amani ndani ya nchi, kwani katika vitabu vya dini na maandiko, husema baada ya dhiki, faraja hivyo, Dk.Mwinyi ni faraja yao.
Dimwa, amesema dini zote, zinahamasisha amani, hivyo lazima kuiendeleza na kuidumisha, kwani ndiyo msingi wa maendeleo.
Ameeleza kuwa, kila kipindi kama hiki, wakati wa kujiandaa na uchaguzi, kila mtu roho yake ipo juu, lakini Dk.Mwinyi, ameleta amani ndani ya nchi, ndiyo maana nchi imetulia ikisubiri uchaguzi.
“Bila ya kuwa na amani, hatuwezi kufanya maendeleo, kwani kiongozi wetu ana hofu kubwa ya Mungu, hapendelei kuona amani inavunjika nchini,” amesema
Amewaasa kutokubali kuvunja amani, badala yake, kuendelea kuhubiri tunu hiyo, ili nchi yao iendelee kupiga hatua za maendeleo na kuwaombea kura wagombea wa CCM, kwani unapowachagua viongozi hao, wakiwemo marais ndiyo umechagua maendeleo.
Naye Katibu Mtendaji Ofisi ya Mufti Zanzibar, Shekh Khalid Ali Mfaume, amesema amani, utulivu, umoja, mshikamano, uadilifu na haki ni mafundisho yaliyokuwepo katika vitabu vya dini.
Amesema viongozi wa dini, wasichukue maneno ya kisiasa na kuyaingiza katika dini, kwani amani, utulivu, uadilifu, haki, mshikamano na umoja ni ajenda ya kidini.
Amebainisha kuwa, Dk.Mwinyi, amesimamia amani kwa dhamira njema, ndiyo maana Zanzibar inaendelea kupiga hatua na watu wanafanya shughuli zao za kiuchumi na kijamii, bila changamoto hasa kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.
Amesema amani haivunjiki bure, bali inatokana na maneno, hivyo aliwaasa kila mmoja ana jukumu la kubeba jambo hilo.
Kwa upande wao viongozi wa dini, walimpongeza Dk.Mwinyi kwa kudumisha amani na kufanya maendeleo makubwa nchini.
Mohammed Abdallah Foum kutoka dini ya kiislamu, alisema Dk.Mwinyi, amejizatiti katika kuwaunganisha Wazanzibari na kusema kuwa, jambo hilo ni jema kwani Mtume (SAW) alilifanya hilo na yeye Dk.Mwinyi alipoingia madarakani alifanya hivyo.
Alibainisha kuwa, Zanzibar walikuwa hawana siasa za uadilifu bali walikuwa na changamoto lakini yeye yote hayo aliyafanyia kazi ikiwemo suala la mitaala.
Said Abdalla Nassor, alisema Dk.Mwimyi amejenga nchi kwa misingi ya amani, umoja na uzalendo.
Pia, alisema Dk. Mwinyi, ameendesha nchi kwa subira, haiwezekani kuondosha uhalisia wa maendeleo kwa sababu ya maneno, kwani nchi zote zilizoendelea zinatokana na maendeleo kupitia barabara afya na elimu.




