Na JOE NAKAJUMO
VIWANDA ni moja ya msingi ya maendeleo ya nchi yoyote. Tanzania haipo nyuma katika kuhakikisha viwanda vinachukua nafasi kubwa katika kuchangia Pato la Taifa.
Kwa kutambua hilo, Tanzania kwa miaka mingi imekuwa ikitekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa. Julai Mosi, mwaka huu wa 2026, itaanza kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Dira 2050, inatilia mkazo katika maendeleo ya viwanda kama msingi wa kuongeza thamani ya raslimali, kupanua wigo wa ajira, kupunguza uagizaji bidhaa kutoka nje na kuongeza mauzo ya bidhaa za Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, alizindua Bunge la 13, Novemba mwaka jana, 2025. Aliwaambia wabunge kuwa malengo ya nchi hayawezi kufikiwa bila kukuza sekta ya viwanda nchini.
Hivyo limewekwa lengo la kuongeza kasi ya ukuaji wa sekta ya uzalishaji viwandani kutoka asilimia 4.8 hadi kufikia asilimia 9 kwa mwaka ifikapo mwaka 2030.
KONGANI ZA VIWANDA
Dk. Samia alilieleza Bunge jipya kuwa katika kipindi kilichopita, serikali iliweza kuanzisha kongani kubwa ya viwanda na kuvutia wawekezaji wengi zaidi. Miongoni mwa kongani iliyoanzishwa ni Kwala, mkoani Pwani. Itakapokamilika, itazalisha ajira moja kwa moja 100,000 na sizizo za moja kwa moja 500,000.
Rais alitaja kongani ya Buswagi, mkoani Shinyanga, inayotarajiwa kuzalisha ajira 300,000 itakapokamilika.
Alisema itaongezwa kongani nyingine mpya na ya kisasa Bagamoyo, inayotarajiwa kuzalisha ajira nyingi kwa vijana na Tanzania.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, alisema sekta ya viwanda na biashara ni mhimili mkuu wa kujenga Tanzania ya uchumi wakati, wa juu, shirikishi na yenye ajira nyingi.
AJIRA MILIONI SITA VIJANA
Katika kutekeleza ahadi moja ya ahadi za Rais Dk. Samia, kutengeneza ajira ndani ya siku 100, tangu aingie madarakani kwa kipindi cha pili, Waziri Judith ametangaza mpango wa serikali kujenga kongani za viwanda 9,040 zitakazozalisha ajira milioni 6.5 kwa vijana katika maeneo mbalimbali nchini.
Waziri anayataja maeneo ya kongani yatakayojengwa viwanda ni Kigamboni, mkoani Dar es Salaam, Nyakato (Mwanza), Azimio (Arusha), Uvinza (Kigoma) Nyasa (Ruvuma), Songwe na Mbeya.
SIKU 100 ZA MAFANIKIO YA VIWANDA
Katika taarifa ya mafanikio ndani ya siku 100, Waziri Judith alisema ujenzi wa viwanda hivyo unamaanisha vinakuja vijijini na pembezoni mwa maeneo mbalimbali ya nchi.
Hii itasaidia kuongeza kipato cha wakulima kupitia uongezaji wa thamani na maelfu ya vijana wanafunguliwa milango ya kumiliki, kuendesha viwanda na biashara katika kongani.
Aliyataja mafanikio mengine ndani ya siku 100, kuwa ni pamoja na kutolewa mikopo yenye thamani ya zaidi ya sh.milioni 280, kuzalisha ajira 546 kwa vijana, usajili wa kampuni, majina ya biashara na leseni za viwanda uanzishwaji mitaa ya viwanda na kongani ambazo zitazalisha maelfu ya ajira na kuandaa programu za biashara 100,000 kwa vijana.
Waziri Judith alisema Tanzania kuna kongani za viwanda 34, zikiwemo Kwala Industrial Park na Modern Industrial Park-Mlandizi.
TAARIFA ZA MASOKO
Kadhalika katika kipindi cha siku 100, zaidi ya vijana 1,000 wamepata mafunzo ya ujasiriamali na kuingizwa katika programu za uatamizi wa biashara na wafanyabiashara zaidi ya 26,000 wamepata taarifa za masoko kupitia mifumo ya kidijitali.
Mafanikio mengine ni uanzishaji viwanda vipya vya nishati mbadala, uchakataji mazao, dawa na mbolea kuwekwa katika msitari wa uzalishaji na wakulima wa korosho kuingiziwa zaidi ya sh. trilioni
moja kupitia mfuko wa stakabadhi ghalani.
Kuhusu mchango wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa, Waziri wa Viwanda na Biashara, alisema sekta hiyo imeongeza mchango wake kutoka asilimia 7 mwaka 2023 hadi asilimia 7.3 mwaka 2024.
Sekta ya biashara imechangia asilimia 8.6 katika Pato la Taifa. Thamani ya uzalishaji wa bidhaa za viwandani, ilifikia sh. trilioni 26.4 mwaka 2023.
MCHUCHUMA NA LIGANGA
Judith ameitaja miradi mikubwa itakayozalisha maelfu ya ajira kuwa ni mradi wa chuma wa Mchuchuma na Liganga, Magadi Soda Engaruka, mradi wa chuma wa Maganga Matitu na mradi wa makaa ya mawe Kale waka.
TANGA YA VIWANDA YAREJEA
Wakati wa ziara yake mkoani Tanga, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith mapema Januari, alisema serikali imeanza utekelezaji mpango mkakati wa kufufua viwanda 18 visivyofanyakazi kwa muda mrefu.
Hatua hii ni kutekeleza maelekezo ya Rais Dk. Samia, kutaka kurejesha hadhi ya mkoa wa Tanga ambao viwanda vilishamiri.
Akizungumza baada ya kukagua baadhi ya viwanda,Waziri Judith alisema serikali imejipanga kuhakikisha vilivyobainishwa, vinaanza uzalishaji kuchochea soko la ndani na nje.
FOMA, NONDO, MBAO SOKONI
Miongoni mwa viwanda vilivyokaguliwa na kupewa kipaumbele kufufuliwa ni Kiwanda cha Chuma ‘Steel Rolling Mills’,kiwanda cha mbao cha ‘Sikh Saw Mills’ na kiwanda cha sabuni cha ‘Foma Detergent’.
Mwekezaji wa Kiwanda cha Chuma, ameanza majaribio ya mitambo mipya kwa kuzalisha nondo na kuahidi ndani ya miezi mitatu ataanza uzalishaji wa tani 30 hadi 40.
Katika kiwanda cha mbao,’Sikh Saw Mills’,mwekezaji, anakikarabati na kununua mashine nne mpya. Ukarabati umefikia asilimia 60.
Waziri Judith alisema lengo ni kuona bidhaa zinaingia sokoni na vijana wa Tanga wapate ajira kama ilivyokuwa zamani.
FURSA UWEKEZAJI PWANI
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, anautaja mkoa huo kuwa ni kitovu cha viwanda na ukanda wa miradi ya kimkakati. Aliwaeleza wawekezaji wa ndani na nje fursa zilizopo mkoani humo.
Kunenge alisema ndani ya miaka minne, viwanda 244, vimejengwa mkoani Pwani, sawa na wastani wa viwanda 61 kwa mwaka.
AJIRA 9,000 MKULAZI
Kiwanda kingine ambacho kimezalisha ajira ni Kiwanda cha Sukari Mkulazi, mkoani Morogoro. Kimezalisha ajira zaidi ya 9,900 kwa Watanzania. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, alisema kiwanda kimepunguza changamoto ya ajira na kipato cha wananchi maeneo kuzunguka kiwanda.
“Kiwanda kimechochea ukuaji wa uchumi kupitia ajira za moja kwa moja 1,920 na zisizo za moja kwa moja 8,000. Uzalishaji kwa sasa ni tani 30,000 za sukari. Lengo ni kuzalisha tani 50,000 ifikapo mwaka 2026/2027. Kinaendeshwa kwa ubia na wawekezaji Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Jeshi la Magereza Tanzania,” alisema.




