• ePaper
Monday, May 25, 2026
  • Login
No Result
View All Result
Uhuru Publication
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Login
No Result
View All Result
ePaper
Uhuru Publication
Home Habari

USAFIRISHAJI MAJINI KUFUNGUA UCHUMI WA MWANZA NA TAIFA

Abdurahman Jumanne by Abdurahman Jumanne
April 1, 2026
in Habari, Kitaifa, Makala
0
USAFIRISHAJI MAJINI KUFUNGUA UCHUMI WA MWANZA NA TAIFA
0
SHARES
17
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

Na BALTAZAR MASHAKA, Mwanza

KWA miaka kadhaa, shughuli za usafirishaji mkubwa katika Ziwa Victoria zilisimama kwa namna isiyo ya kawaida. Meli zililala bandarini, zingine zikisubiri ukarabati, zikionekana kama kumbukumbu ya historia.

Kwa wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa na Mwanza hali hiyo ilimaanisha kupungua kwa biashara, ajira na mzunguko wa uchumi. Leo, taswira hiyo imebadilika.

Kupitia uwekezaji wa kimkakati wa serikali na mageuzi ya uongozi ndani ya TASHICO, meli zimerejea majini, safari zimeongezeka na Mwanza imeimarika tena kama kitovu cha usafiri wa majini na biashara ya kikanda.

Kwa nini mageuzi ya TASHICO ni muhimu sasa

Katika kipindi ambacho Tanzania inaelekeza nguvu katika uchumi wa buluu na miundombinu ya kimkakati, mafanikio ya TASHICO yanaonyesha kwa vitendo namna uwekezaji wa serikali unavyoweza kuigeuza taasisi ya umma kuwa chachu ya maendeleo.

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, katika kipindi ambacho imeendelea kuwekeza nguvu katika miundombinu ya kimkakati, TASHICO imeibuka kuwa mhimili wa uchumi wa Mkoa wa Mwanza na Taifa kwa ujumla.

Mafanikio ya kampuni hiyo yanaoneshwa kwa vitendo kupitia uwekezaji wa serikali, takribani sh. trilioni moja, ambapo TASHICO imefanikiwa kufufua na kupanua huduma za usafiri wa majini katika maziwa makuu na sasa inaelekea kutanua wigo hadi Bahari ya Hindi.

Akizungumza katika mahojiano maalumu, Mkurugenzi Mtendaji wa TASHICO, Eric Hamissi, anafafanua kuwa safari ya mageuzi ya taasisi hiyo na mchango wake katika kukuza uchumi wa Mwanza na taifa, ambapo hatua za awali zililenga kuleta uthabiti na ufanisi wa kampuni.

Mageuzi ya MSCL hadi TASHICO

Hamissi, alieleza kihistoria kampuni hiyo ilianzishwa mwaka 1948 ikiwa kitengo cha Shirika la Reli na Bandari za Afrika Mashariki, baadaye mwaka 1977, baada ya kuvunjka kwa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ikawa ni kitengo cha usafiri kwa njia ya maji chini ya Shirika la Reli Tanzania (TRC).

Mwaka 1997, ilibadilishwa na kuwa Kampuni ya Huduma za Meli (Marine Services Company-MSCL) na mwaka 2024 MSCL ilibadilishwa ikapewa jina la Kampuni ya Meli Tanzania (Tanzania Shipping Company Limited–TASHICO).

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji huyo, mabadiliko hayo si ya jina tu, ni mkakati mpana wa kuijenga kampuni kuifanya ya kisasa, yenye ushindani na mchango mkubwa kiuchumi.

Huduma na uwezo wa TASHICO

Tawi la Mwanza katika Ziwa Victoria ndilo lenye shughuli nyingi zaidi ndani ya TASHICO. Kwa sasa kampuni inamiliki jumla ya meli kumi na nane (18) katika matawi matatu ya Mwanza (Ziwa Vctoria), Kigoma (Ziwa Tanganyika) na Kyela (Ziwa Nyasa).

Kuongezeka kwa meli mpya na zilizokarabatiwa, upanuzi wa njia za usafiri, na kuimarika kwa mifumo ya mapato, siyo tu kumerejesha hadhi ya usafiri wa majini, pia, kumeimarisha mnyororo wa biashara, ajira na mapato katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, Magharibi na Kusini.

Ndiyo maana hadithi ya TASHICO ni kielelezo cha mwelekeo mpana wa uchumi wa Tanzania, kuelekea ushindani wa kikanda na kimataifa.

TAWI LA MWANZA (ZIWA VICTORIA)

Meli ya MV Mwanza inayotoa huduma ya usafiri kati ya Mwanza na Bukoba kupitia Kemondo, yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo, ujenzi wake ulianza Machi mwaka 2023 na kukamilika Septemba.

Pia, MV New Victoria Hapa Kazi Tu, iliyojengwa mwaka 1960, ina uwezo wa kubeba abiria 1,200 na mizigo tani 200, ilikarabatiwa mwaka 2020, inafanya safari zake mara tatu kwa wiki kati ya Mwanza na Bukoba kupitia Kemondo.

Aidha, MV New Butiama Hapa Kazi Tu, ni meli yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na mizigo tani 100, ikitoa huduma kati ya Jiji la Mwanza na Mji wa Nansio, katika Kisiwa cha Ukerewe, ilijengwa mwaka 1980 na kufanyiwa ukarabati mkubwa 2020.

MV Clarias inabeba abiria 216 na mizigo tani 10, ilijengwa 1961, imesimama kutokana na uchakavu, imetengewa fedha mwaka huu wa fedha 2025/2026 kwa ukarabati na mchakato wa manunuzi unaendelea wa kumpata mkandarasi.

Aidha, MV Serengeti ilijengwa mwaka 1988, inabeba abiria 593 na mizigo tani 350, ilisimama kutoa huduma mwaka 2016 kutokana na hitilafu katika injini zake, inatarajiwa kukarabatiwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Meli ya MV. Umoja yenye uwezo wa kubeba shehena ya mabehewa (Wagon Ferry) ya uzito wa tani 1,200 sawa na mabehewa 22 ya reli, ilijengwa 1964 na ilifanyiwa ukarabati mkubwa kuanzia Novemba 2021 hadi Septemba, 2023.

MT. Nyangumi meli ya kubeba shehena ya tani 350 za mafuta (sawa na lita 400,000), ilijengwa 1958 ambapo ilisimama tangu mwaka 2010 na iko katika mpango wa kufanyiwa matengenezo.

MT Ukerewe ni meli ya Uokozi iliyojengwa 1983, inafanyiwa ukarabati ambao umefikia asilimia 60, ilitarajiwa kukamilika mwishoni mwa Februari  2026.

Meli ya ML Wimbi Tishari (Motor Lighter)- 120 iliyojengwa 1938, inafanya safari zake kati ya Mwanza na visiwa vya Gana na Goziba, ikisafirisha dagaa na mazao ya uvuvi, ML Maindi na ya Tishari (Motor Lighter)- 120 iliyojengwa 1938, ilisimama tangu mwaka 2006 kutokana na uchakavu wa mitambo yake.

TAWI LA KIGOMA (ZIWA TANGANYIKA)

Serikali imeendelea kuboresha meli zake kwa usafiri na usafirishaji katika Ukanda wa Maziwa Makuu kuhakikisha unakuwa salama, hivyo inaendelea na ujenzi wa kiwanda cha kujengea meli katika Ziwa Tanganyika.

Pia, MV Liemba ya abiria na mizigo iliyojengwa mwaka 1923, yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na shehena ya mizigo tani 200, kwa sasa inafanyiwa ukarabati ambao umefikia asilimia 55, hadi Julai mwaka huu itakuwa imekamilika.

Meli ya MV Mwongozo, iliyojengwa mwaka 1982 ni meli ya kubeba abiria 800 na mizigo tani 80, iko katika mpango wa kufanyiwa matengenezo iendelee kutoa huduma katika Ziwa Tanganyika.

MT Sangara ya kubeba mafuta (Tanker), meli hiyo ina uwezo wa kubeba lita 350, ilifanyiwa maboresho makubwa kwa gharama ya sh. bilioni 3.6 ambapo Mei 20, mwaka jana, ilifanya safari ya majaribio kwenda Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Meli hiyo iliyojengwa mwaka 1981, baada ya ukarabati inasafirisha bidhaa za nishati ya mafuta kati ya Bandari ya Kigoma na Kalemie, nchini DRC.

Sea Warriors, ni boti ya utalii ilyojengwa mwaka 1994 ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 10, ilisimama tangu mwaka 2012 kwa sababu ya uchakavu, hivyo imetengewa fedha za mapato ya ndani katika bajeti ya mwaka ujao.

TAWI LA KYELA (ZIWA NYASA)

Katika tawi la Kyela, TASHICO inamiliki na kuendesha meli ya MV Songea, inayosafirisha abiria 200 na mizigo tani 43.5, ilijengwa 1974, ilisimama tangu Januari, 2017 sababu ya uchakavu, hivyo katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026, imetengewa fedha ya matengenezo.

MV Iringa ya abiria na mizigo, ina uwezo wa kubeba abiria 139 na tani tano za mizigo. Meli hiyo iliyojengwa mwaka 1974, ilisitisha huduma mwaka 2012 kutokana na uchakavu wa mitambo yake.

Meli nyingine ni MV Mbeya II, inayobeba abiria 200 na tani 200 za mizigo, ilijengwa mwaka 2020, inaendelea kufanya kazi ya kutoa huduma kwa wananchi.

Pia, MV Ruvuma za MV Njombe zilijengwa mwaka 2021, zinafanya kazi ya kusafirisha shehena ya mizigo, zikiwa na uwezo wa kubeba tani 1000 kila moja kwa wakati mmoja.

Taswira ya hali ya kifedha ya Kampuni Iliyokuwa Ukingoni

Hamissi alisema wakati anateuliwa kuongoza TASHICO Novemba, mwaka 2016 (wakati huo ikiwa MSCL), taasisi hiyo ilikuwa katika hali tete na ngumu kifedha na kiutendaji kutokana na changamoto mbalimbali.

Changamoto kubwa zilizokuwepo ni meli nyingi kusimama kwa sababu ya uchakavu na ukosefu wa vipuri, mapato yasiyokidhi gharama za uendeshaji, mishahara kuchelewa kwa miezi kadhaa, mifumo dhaifu ya usimamizi wa mapato, kuporomoka kwa imani ya abiria na wadau.

“Ni kweli nilikuta kampuni ikiwa na meli nyingi takribani meli 14 na boti moja ya mwendokasi. Hata hivyo, takribani meli zote zilikuwa zimesimama kutokana uchakavu, hivyo hapakuwa na chanzo mbadala cha uzalishaji wa mapato, kwa hiyo hali ya kifedha ilikuwa ni mbaya sana.”anasema 

Hivyo, kwa mtazamo wa kiuchumi TASHICO ilipitia awamu tatu: kuokoa (stabilization), kujenga upya (restructuring) na kupanua (expansion). Kwa kifupi, kampuni ilikuwa katika hatari ya kushindwa kujiendesha (operational insolvency), hata kama haijafikia hatua ya kufilisika kisheria.

Uwekezaji wa Serikali

Uwekezaji wa serikali uliofanyika kwa TASHICO, hadi sasa una thamani ya takribani sh. trilioni moja, umehusisha ukarabati wa meli chakavu, ujenzi wa meli mpya na chelezo.

Hadi sasa miradi iliyokamilika ni ya ukarabati wa meli za MV New Victoria, uliogharimu sh. bilioni 23, MV New Butiama sh. bilioni 5, MV Umoja sh. bilioni 6, na ujenzi wa meli mpya ya abiria na mizigo ya MV New Mwanza, zote katika Ziwa Victoria.

Hamissi alisema, meli hizo baada ya kukamilika zimeongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa kusafirisha abiria na mizigo kati ya Mwanza, Bukoba, Ukerewe na hata nchi jirani ya Uganda.

Alitolea mfano wa MV Umoja, imeimarisha biashara ya kikanda kwa kusafirisha mabehewa ya reli kati ya Mwanza na Port Bell na Jinja nchini Uganda, imesaidia kupunguza gharama za usafirishaji na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la Afrika Mashariki.

“Kwa Mkoa wa Mwanza, huduma hizi zimeongeza mzunguko wa biashara, kuchochea shughuli za usafirishaji kupitia kupakia na kupakua mizigo, kusafirisha mazao ya uvuvi, kilimo na biashara ndogo ndogo, huku zikitoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa mamia ya wananchi,” alieleza Hamissi.

Aliitaja miradi inayoendelea ni ujenzi wa Chelezo katika Ziwa Victoria na ukarabati wa meli ya MT Sangara katika Ziwa Tanganyika.

Mchango wa meli

Alisema kuongezeka kwa meli za MV New Victoria, MV New Butiama, MV New Mwanza, MV Umoja, MT Sangara na MV Mbeya II, kumesaidia TASHICO kuongeza uwezo wa kusafirisha abiria na mizigo ikilinganishwa na mwaka 2019/2020 wakati uwekezaji ulipokuwa unaanza.

“Ongezeko la abiria na mizigo inayosafirishwa na TASHICO, limesababisha kuongezeka mapato yanayozalishwa kupitia uendeshaji wa huduma zake, hivyo ni wazi ujio wa meli hizo baada ya kukamilika kwa miradi yake kumechangia sana uwezo wa TASHICO kuzalisha mapato yake,”alisema.

Hamissi alieleza kuwa hatua za awali zilijikita katika maeneo matatu zikilenga kuleta uthabiti wa kifedha, urejeshaji wa huduma na kurejesha imani kwa wananchi kabla ya kuanza upanuzi.

Ushirikiano na Serikali

Kupitia Wizara ya Uchukuzi na Hazina, Serikali ilitoa msaada wa kifedha wa mpito kwa ajili ya mishahara na kuanza miradi ya kimkakati ya ujenzi wa meli mpya.

Alisema uwekezaji huo unaokadiriwa kufikia takribani shilingi trilioni moja umewezesha kukamilika kwa miradi kadhaa ya ukarabati na ujenzi.

Mwanza Kitovu cha Uchumi wa Majini

Kwa sasa TASHICO inamiliki meli 18 katika matawi ya Mwanza, Kigoma na Kyela, katika Ziwa Victoria, meli kama MV New Mwanza yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo imeongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa kampuni katika huduma ya usafiri na usafirishaji.

Ajira na Mapato

Alisema kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali, idadi ya wafanyakazi imeongezeka mbali na ajira za moja kwa moja, sekta za huduma, usafirishaji, uvuvi na biashara zimepata msukumo mpya.

Kwa mtazamo mpana, alisema mkakati huo umepunguza gharama za usafirishaji wa mizigo, kuimarika kwa usafiri wa majini kumeongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la Afrika Mashariki, hususan katika biashara na Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Mafanikio ya Uongozi

“Mafanikio makubwa ninayojivunia katika kuiongoza TASHICO, ni kuweza kuubadili mwelekeo wa kampuni kutoka kampuni iliyokuwa inaelekea kufa na iliyokatiwa tamaa na hatimaye kuwa kampuni inayokua, inayojulikana, tegemeo na inayochangia ukuaji wa uchumi wa nchi ya maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla,” alisema Hamissi.

Alisema hayo yamefanyika kupitia mikakati madhubuti iliyowekwa ya kuifufua kampuni, kwa kushirikiana na serikali kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayohusisha ukarabati wa meli chakavu, ujenzi wa meli mpya na chelezo.

Pia, kuwekwa kwa mifumo ya kisasa ya udhibiti wa ukusanyaji wa mapato ya kampuni, kuboresha huduma zitolewazo na kampuni kwa wateja wake, kuitangaza na kuifanya ijulikane kwa wadau mbalimbali.

Kuboresha maslahi ya watumishi na kuajiri watumishi wapya na mahiri na kuogeza ikama ya wafanyakazi kutoka 135 mwaka 2020 hadi kufikia 250, kuongeza tija kwa kampuni.

Mwelekeo wa Baadaye: Bahari ya Hindi

Hamissi alieleza kuwa, TASHICO kwa sasa inaangalia uwezekano wa kupanua huduma hadi Bahari ya Hindi, hatua inayolenga kuifanya kampuni kuwa mhimili wa uchumi wa majini kitaifa.

“Mkakati huu ulilenga kupanua vyanzo vya mapato na kupunguza utegemezi wa chanzo kimoja. Dira yetu baadaye ni kuifanya TASHICO taasisi ya kisasa, yenye ushindani na inayounganisha masoko ya ndani na nje.” Alisema.

Kielelezo cha Mageuzi ya Taasisi za Umma

Alisema, Rais Dk.Samia na Serikali Awamu ya Sita anayoiongoza, ameendelea kuwekeza katika miundombinu ya kimkakati, maageuzi hayo ya TASHICO yanaonesha uwekezaji huo unavyoweza kugeuza taasisi ya umma kutoka mzigo wa kifedha kuwa chachu ya maendeleo.

“Tunamshukuru Rais Dk. Samia kwa uwekezaji wenye tija ambao umeifanya TASHICO leo hii, si tena kampuni iliyokatiwa tamaa, ni taasisi inayokua na  kuchangia katika mapato ya serikali, ajira za wananchi na ustawi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa na Taifa kwa ujumla,” alisema Hamisi.

Aliongeza: “Serikali  chini ya uongozi wa Dk. Samia, TASHICO imekuwa ni miongoni mwa vielelezo vya matokeo ya uwekezaji huo.” 

“Kwa Mwanza na Tanzania kwa ujumla, mchango wake si tu kampuni ya usafiri, ni zaidi ya usafiri wa majini, ni daraja la uchumi likiunganisha watu, masoko, ajira na matumaini mapya ya fursa za uchumi wa buluu,” anahitimisha Hamissi.

Previous Post

WIZARA YA VIWANDA YAZALISHA AJIRA LUKUKI

Next Post

MWENEZI KIHONGOSI NA MSISITIZO WA MAENDELEO, SIYO VURUGU

Next Post
MWENEZI KIHONGOSI NA MSISITIZO WA MAENDELEO, SIYO VURUGU

MWENEZI KIHONGOSI NA MSISITIZO WA MAENDELEO, SIYO VURUGU

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Recommended

FIDIA YANUKIA WANANCHI WALIOPISHA MRADI SGR

FIDIA YANUKIA WANANCHI WALIOPISHA MRADI SGR

9 months ago
KUDUMISHA SERA YA CHINA MOJA NA KUIMARISHA URAFIKI KATI YA CHINA NA TANZANIA

KUDUMISHA SERA YA CHINA MOJA NA KUIMARISHA URAFIKI KATI YA CHINA NA TANZANIA

4 days ago

Popular News

  • WAZIRI MKUU AHIMIZA MALEZI YA KIMAADILI NA USHIRIKIANO WA KIJAMII

    WAZIRI MKUU AHIMIZA MALEZI YA KIMAADILI NA USHIRIKIANO WA KIJAMII

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • WAZIRI MKUU AVITAKA VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA KUWA MACHO DHIDI YA WAVUNJA AMANI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • KILIO CHA BANDO CHATUA BUNGENI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • ZIARA YA KIHONGOSI YAACHA NEEMA KWA WANAWAKE MARA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • TANZANIA YAJIPANGA KUDHIBITI MIJI HOLELA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Stay Update, Subscribe Now!

Check your inbox or spam folder to confirm your subscription.

Ukurasa Rasmi wa Televisheni ya Gazeti la Uhuru.

Facebook-f Instagram X-twitter Youtube tiktok
Quick Links
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalum
  • Kolamu
  • Makala
Services
  • ePaper
Contact Information
  • Dar es Salaam,Tanzania
  • info@upl.co.tz
  • +255 783 925 742
Uhuru Publications , 2025 © All Rights Reserved
  • Terms & Conditions
  • Privacy Policy
  • FAQ
No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Contact
  • Hadithi

© 2026 JNews - Premium WordPress news & magazine theme by Jegtheme.

Are you sure want to unlock this post?
Unlock left : 0
Are you sure want to cancel subscription?