Na SELINA METHEW
KATIKA mijadala ya kisasa ya kisiasa na kijamii, neno “maandamano” limeendelea kupata tafsiri tofauti kulingana na muktadha na malengo ya wanaolitumia.
Baadhi ya wananchi, wanatumia neno maandamano kama haki ya kikatiba ya kueleza hisia au kupinga jambo.
Hata hivyo, kwa mtazamo mpana wa maendeleo ya taifa, dhana hii inahitaji kupanuliwa zaidi kwamba maandamano ya kweli kwa wananchi yanatakiwa kutafsiriwa kama njia ya kujiletea maendeleo, siyo yale yanayoishia vurugu na uharibifu wa mali.
Huu ndiyo ujumbe mkuu uliojitokeza kufuatia kauli za Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, alipokuwa akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Kagera.
Alisema kwa msisitizo mkubwa kuwa, nguvu ya wananchi, hasa vijana, inapaswa kuelekezwa katika shughuli za uzalishaji mali badala ya kushiriki katika vitendo visivyo na tija.
Alieleza kauli yake ya “kuandamana kataa, tafuta fedha,” haikumaanisha kupinga haki za msingi za wananchi, ililenga kuhamasisha mabadiliko ya fikra kutoka katika utegemezi wa siasa za vurugu kwenda siasa za maendeleo.
Alisema huu ni ujumbe unaohitaji tafakuri ya kina, hasa kipindi ambacho changamoto za kiuchumi zinahitaji nguvu kazi, ubunifu na mshikamano wa kitaifa.
Kwa mtazamo huu, alisema maandamano ya maana ni yale ya kupambana na umasikini kwa kufanya kazi kwa bidii; kupinga ujinga kwa kuwekeza katika elimu; na ni yale ya kupambana na maradhi kwa kuboresha huduma za afya na kuzingatia mtindo bora wa maisha.
Kiongozi huyo, alisema haya ndiyo maandamano yanayojenga taifa imara na lenye kujitegemea.
AMANI NA UTULIVU
Hata hivyo, alisema ili tafsiri hii iweze kuleta matokeo chanya, ni lazima kuwe na mazingira ya amani na utulivu.
Alisema amani ndiyo msingi wa kila aina ya maendeleo kwa kuwa bila amani hakuna uwekezaji, hakuna biashara wala uzalishaji unaoweza kufanyika kwa ufanisi.
Ndiyo maana, alisema onyo lake kuhusu kulinda amani lina uzito mkubwa kwa kuwa pindi amani inapovurugika, kila shughuli ya kiuchumi husimama na wananchi hulazimika kukimbia kuokoa maisha yao.
Kihongosi alieleza katika hali hiyo anayepoteza siyo mtu mmoja bali ni taifa zima. Ni ukweli usiopingika kuwa vurugu huathiri zaidi makundi yaliyo hatarini yakiwemo watoto, wazee, wanawake na watu wenye mahitaji maalum ambao mara nyingi hawana uwezo wa kujilinda au kukimbia kwa haraka.
Katika muktadha huo, alisema wito wa kulinda amani unatakiwa kuzingatiwa kama jukumu la kila mwananchi, akisisitiza kuwa amani si mali ya serikali peke yake bali ni urithi wa wote unaotakiwa kulindwa kwa gharama yoyote ile.
MATUMIZI MABAYA YA MADHABAHU
Sambamba na hilo, alisema matumizi mabaya ya dini ni miongoni mwa changamoto zinazoweza kuhatarisha mshikamano wa taifa.
Alifafanua baadhi ya watu wameanza kutumia madhabahu kama majukwaa ya kisiasa yenye lengo la kueneza chuki na mgawanyiko.
Alisema hali hiyo inapaswa kupingwa kwa nguvu zote kwa kuwa dini, kwa asili yake, inalenga kuwaunganisha watu na kuwajenga kiroho, lakini inapogeuzwa kuwa chombo cha uchochezi hupoteza mwelekeo na kuwa hatari kwa ustawi wa jamii.
AKEMEA SIASA ZA UKABILA
Aidha, alisema kauli ya “tuunganishwe na utanzania siyo dini zetu” inabeba ujumbe mzito wa uzalendo kwa kuwa inaweka mbele maslahi ya taifa kuliko tofauti za kiimani.
Kihongosi alisema siasa za chuki zinazogawanya watu kwa misingi ya ukabila, ukanda au dini ni tishio kwa umoja wa kitaifa, akibainisha kuwa historia ya mataifa mengi inaonyesha mgawanyiko wa aina hiyo husababisha migogoro mikubwa na kurudisha nyuma maendeleo.
Katika kukabiliana na changamoto hizo, alisema elimu kwa umma inahitajika zaidi ili wananchi wafahamu kuwa mara nyingi wanaochochea vurugu hawawi wahanga wa matokeo yake, bali wanaoumia ni wananchi wa kawaida wanaopoteza mali, maisha na fursa za kiuchumi.
VIJANA MSITUMIKE VIBAYA
Akizungumzia vijana, alisema kundi hilo linapaswa kuwa makini zaidi kwa kuwa limekuwa likitumika vibaya katika kutekeleza vurugu zinazochochewa na watu wenye maslahi binafsi.
Alisema ni muhimu kwa vijana kubadili mtazamo na kutumia nguvu zao katika kujenga badala ya kubomoa.
Alisema ujasiriamali, ubunifu na elimu ni silaha muhimu zitakazowasaidia vijana kufikia ndoto zao na kuchangia maendeleo ya taifa.
ULINZI MIUNDOMBINU YA UMMA
Kwa upande mwingine, alisema suala la kulinda miundombinu ya umma linapaswa kupewa uzito unaostahili kwa kuwa imejengwa kwa gharama kubwa kwa fedha za walipa kodi, hivyo uharibifu wake ni sawa na kujiumiza wenyewe.
Ni muhimu, alisema, kujenga utamaduni wa kuthamini na kulinda rasilimali za taifa ili kuhakikisha maendeleo yaliyopatikana yanaendelea kudumu na kunufaisha vizazi vijavyo.
VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA VIHESHIMIWE
Pia, alisema umuhimu wa kuheshimu vyombo vya ulinzi na usalama hauwezi kupuuzwa kwa kuwa vina jukumu la kulinda amani na usalama wa raia.
Alieleza kuwa kuvichukia au kuvidharau kunadhoofisha mfumo mzima wa ulinzi wa taifa.
Kihongosi alisema wananchi wanapaswa kushirikiana na vyombo hivyo ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama na tulivu, akisisitiza kuwa ushirikiano huo ni nguzo muhimu ya maendeleo endelevu.
Kwa ujumla, Kihongosi alisema hoja kuu ni kwamba maendeleo ya taifa hayapatikani kwa njia ya vurugu bali kwa juhudi za pamoja za wananchi wanaofanya kazi kwa bidii.
Alisema “maandamano” ya kweli ni yale ya kupambana na changamoto za maisha kwa njia halali na endelevu.
Alisema ni wakati sasa kwa wananchi kubadili mtazamo kwa kuacha kushawishika na ajenda zisizo na tija na badala yake kuelekeza nguvu zao katika kujenga taifa.
Aliongeza kuwa hatua hii itakawezesha kujenga mustakabali bora kwa vizazi vya sasa na vijavyo.




