Na IRENE MWASOMOLA
TUME ya Kuchunguza Matukio ya Kabla na Wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, mwaka 2025, imetaja vyanzo vitano vilivyosababisha ghasia ikiwa ni pamoja na changamoto za kijamii za muda mrefu, masuala ya kisiasa ikiwemo madai ya katiba mpya.
Vyanzo vingine ni madai ya uboreshaji wa Tume Huru ya Uchaguzi, ugumu wa maisha, ukosefu wa ajira na mazingira ya biashara yasiyo rafiki, madai ya utekaji na kupotea kwa watu, masuala ya kijamii yanayojumuisha mmomonyoko wa maadili, kero za rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.
Kauli hiyo ilitolewa Ikulu, jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman, alipokabidhi ripoti ya tume hiyo kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
“Ghasia za wakati na baada ya uchaguzi zinatokana na changamoto mbalimbali zilizokuwepo bila kutatuliwa. Mosi masuala ya kisiasa yanayohusisha madai ya katiba mpya, demokrasia katika mfumo wa vyama vingi.
“Pili, ni masuala ya kijamii yanayojumuisha ugumu wa maisha, ukosefu wa ajira, mazingira ya biashara yasiyo rafiki na utitiri wa tozo na kodi na mfumo usio rafiki wa utozaji na ukusanyaji,” alisema.
Alisema chanzo kingine ni utendaji usioridhisha wa watendaji wa ngazi za chini, ikiwemo kutotatua kero za wananchi kwa wakati.
Kwa mujibu wa Jaji mstaafu Chande, tume ilipokea maeneo 31 ambayo yalitajwa na mashahidi kuwa ni chanzo cha ghasia hizo, ambapo baada ya kuchakata iliviainisha vyanzo vitano na vichocheo vinane.
UTEKAJI
Jaji mstaafu Chande alisema kwa mujibu wa Jeshi la Polisi kwa kipindi cha miaka mitatu, watu 758 walipotea na kutekwa kati ya hao 445 hawajapatikana.
Alisema jeshi hilo lilieleza masuala ya utekaji yalihusisha mambo mbalimbali ikiwemo masuala ya mapenzi, imani za kishirikina, watu kujiteka wenyewe, usafirishaji haramu wa binadamu na kulipizana visasi.
KATIBA MPYA 2028
Jaji mstaafu Chande alisema tume ilipendekeza serikali iweke utaratibu wa majeruhi wa vurugu wapate matibabu bure, wakiwemo wanaohitaji vifaa saidizi.
Pia, tume hiyo ilipendekeza serikali kutenga siku ya maombolezo kuwakumbuka Watanzania zaidi ya 500 waliopoteza maisha katika vurugu hizo za wakati na baada ya Oktoba 29, mwaka jana.
Mwenyekiti huyo alisema wamependekeza katiba mpya ipatikane mwaka 2028.
Vilevile, ilipendekeza kuundwa kwa tume ya uchunguzi wa kijinai, kufuatia matukio hayo kwa lengo la kufuatilia tuhuma na kubaini wahusika wakuu waliopanga na kuratibu ghasia hizo.
Hata hivyo, tume hiyo ilipendekeza serikali kuiimarisha mfumo wa ajira uwe wa ushindani na haki.
Mapendekezo mengine ni kuimarisha ulinzi shirikishi kupitia mamlaka ya serikali za mitaa, hatua ambayo itasaidia kubaini matukio ya uhalifu kabla hayajafanyika.
Aidha, tume hiyo ilipendekeza ushiriki wa vijana katika mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) yawe ya lazima kwa wanaomaliza kidato cha sita.
Jaji mstaafu Chande alieleza kuwa, tume hiyo ilipendekeza maridhiano, kwa sababu matukio ya ghasia hizo yamesababisha majeraha kwa taifa.
Alisema tume hiyo ilipendekeza Jeshi la Polisi kurudisha uhusiano wake na jamii, kuundwa baraza la wazee na washauri litakalohusisha viongozi wastaafu na wazee wengine katika jamii.
VICHOCHEO VYA GHASIA
Mwenyekiti huyo alisema baadhi ya wanasiasa na wanaharakati walishiriki kuhamasisha watu na kutumia changamoto zao kama fursa za kuwashawishi kufanya vurugu hizo.
Kwa mujibu wa Jaji mstaafu Chande, baadhi ya mashahidi walikiri kupewa simu kupiga picha na kurekodi video kwa lengo la kurusha katika mitandao ya kijamii kuongeza hasira kwa wananchi.
Jaji mstaafu Chande alieleza kuwa, kundi la tatu la vichocheo vya vurugu ni baadhi ya watu waliokatwa majina katika nafasi za kugombea uongozi.
MADHARA YA GHASIA
Alisema uchunguzi wa tume ulibaini ghasia hizo zilisababisha vifo vya watu 518 ambapo Mkoa wa Dar es Salaam, vilikuwa vingi zaidi.
Mwenyekiti huyo alisema vifo 197 ambavyo ni sawa na asilimia 90 vilitokana na kupigwa risasi na 22 sawa na asilimia 10 havikuhusiana na matumizi ya silaha za moto.
Jaji mstaafu Chande alisema kati ya maiti 518, miili 480 ilitambuliwa na kuchukuliwa na familia zao.
Aliongeza kuwa, hadi hivi sasa, kuna maiti tatu ambazo zipo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili hazijachukuliwa na ndugu zao.
Mwenyekiti huyo alisema maiti 199 zilikuwa na majeraha ya sehemu za mkono na miguu, maiti moja ilikuwa haina baadhi ya viungo.
Alisema tume hiyo imependekeza kufanyika kwa upelelezi wa kina wa matukio hayo
Jaji mstaafu Chande alisema tume ilipokea ushahidi wa watu kupotea au kutopatikana, kupigwa risasi katika makazi yao ikiwemo ndani ya nyumba.
Alisema majeruhi 2,390 kati ya hao 2,270 ni raia na asilimia tano ni maofisa wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Jaji mstaafu Chande aliongeza kuwa, majeruhi 219 waliopata majeraha makubwa.
UKWELI MAKABURI YA HALAIKI
Alisema tume ilishirikiana na wataalamu kuchunguza madai ya uwepo wa makaburi ya halaiki eneo la Kondo, wilayani Kinondoni, hata hivyo hayakuthibitika.
DHANA YA MAANDAMANO
Alisema kilichotokea Oktoba 29, mwaka jana, siyo maandamano, bali ni ghasia, kwani hayakuzingatia sheria kwa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi.
Mwenyekiti huyo alisema baadhi ya watu walibeba silaha yakiwemo mawe, panga, bunduki na manati, jambo ambalo ni kinyume na sheria.
Jaji mstaafu Chande alisema sheria za kikanda na kimataifa haziruhusu maandamano ya namna hiyo.
Alisema kilichotokea wakati na baada ya uchaguzi hayakuwa maandamano ya amani.
Vilevile, alisema ghasia hizo zilipangwa kufanyika siku ya uchaguzi mkuu ambazo zililenga kusababisha watu wengine wasipige kura.
MAANDAMANO YALIFADHILIWA
Alisema walipokea ushahidi kuwa, maandamano hayo yalifadhiliwa, yalipangwa, yaliratibiwa, na vijana wengine walipatiwa mafunzo.
Alisema baadhi ya watu walipita mitaani, sokoni na kugawa kati ya sh. 10,000 hadi 50,000 na wengine waliahidiwa ajira.
Jaji mstaafu Chande alitaja makundi hayo ni vijana wa bodaboda na wajasiriamali wadogo.
Mwenyekiti huyo alisema kijana mmoja wa eneo la Usa River mkoani Arusha alipewa sh. 50,000 na aliahidiwa sh. 5,000,000.
Alieleza kuwa, mbinu 16 zilizotumika kufanikisha vurugu hizo ikiwemo kuweka vizuizi barabarani, kuchoma moto vituo vya kupiga kura, kuharibu mali, kuiba na kupora mali za wananchi.
VIASHIRIA
Alisema viashiria vya uvunjifu wa amani vilijitokeza miezi sita kabla ya uchaguzi, ambapo Oktoba 17, mwaka jana, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), iliwasilisha taarifa ya bango liliohamaisha ghasia.
Mwenyekiti huyo alisema licha ya viashiria vya mitandaoni, tume ilibaini uwepo wa vijana wasiopungua 500 katika majengo na misitu ambayo walihifadhiwa.
Alisema katika Jiji la Dar es Salaam eneo moja kulikuwa na vijana waliohifadhiwa katika nyumba iliyokuwa mita 10 kutoka kituo cha polisi.
Aidha, Jaji mstaafu Chande alisema kazi ya uchunguzi ilifanyika katika maeneo 202 yaliyoathirika zaidi katika wilaya 21 na mikoa 11 ambayo ni Mbeya, Dar es Salaam, Ruvuma, Mwanza, Iringa, Dodoma, Geita, Songwe, Arusha, Shinyanga na Mara.
Mwenyekiti Jaji Chande alisema tukio la kwanza la uvunjifu wa amani kwa Dar es Salaam lilitokea Kimara Baruti.
Alisema kwa upande wa Dar es Salaam tume ilifanya mijadala na vikundi 31 vyenye washiriki zaidi ya 4,000.
Mwenyekiti huyo alisema tume ilipokea mawasilisho ya maandishi kwa njia ya posta 149 na madodoso 4,891 na ujumbe fupi wa simu 33,250.
Jaji mstaafu Chande alisema tume ilikutana na makundi maalumu, mamalishe, bodaboda, wajasiriamali, mahabusu, viongozi wa dini, maofisa ustawi wa jamii, waganga wakuu wa mikoa, wakuu wa mashtaka wa mikoa na wadau wengine.
Mwenyekiti huyo alisema watu wanaodhaniwa kuwa ni askari waliingia katika kibanda cha kuangalia televisheni jijini Mwanza na kuwafyatulia risasi watu 15.
Alisema tume ilitumia vyanzo vya moja kwa moja, mbinu za maelezo, takwimu kwa kuhusisha mashahidi wa tukio, mahojiano ya ana kwa ana.
Mwenyekiti huyo alisema miongoni mwa mbinu iliyotumika kuzungumza na waathirika ni mahojiano ya ana kwa ana ambapo waathirika 1,325 walisikilizwa.
Alisema picha zilizozunguka mitandaoni baadhi yake zilikuwa halisi na nyingine zilichezewa kwa kutumia Akili Unde.
Jaji mstaafu Chande alisema picha mnato 450 na mjongeo 850 zilikusanywa na kuwasilishwa na mashuhuda wa matukio.
Alisema mojawapo ya picha ambayo siyo ya kweli ni ile iliyoonesha maiti zipo katika mifuko ya bluu zikizikwa katika makuburi ya halaiki.
Aliongeza kuwa, tume ilitembelea Zanzibar na Kilimanjaro mikoa ambayo haikuwa na ghasia, kujifunza.
Alisema vipo vyama vya siasa vichache na mashirika vilialikwa kwa maandishi, havikufika .




