• ePaper
Friday, April 24, 2026
  • Login
No Result
View All Result
Uhuru Publication
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Login
No Result
View All Result
ePaper
Uhuru Publication
Home Habari

YASIJIRUDIE TENA

Abdurahman Jumanne by Abdurahman Jumanne
April 24, 2026
in Habari, Kitaifa
0
YASIJIRUDIE TENA
0
SHARES
4
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

Na ATHNATH MKIRAMWENI

RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amewahakikishia Watanzania yaliyotokea Oktoba 29, mwaka jana, hayatajirudia tena na kuahidi kubeba mzigo huo kwa  ujasiri na umakini kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama.

Rais Dk. Samia aliitoa kauli hiyo, Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati akipokea ripoti ya Tume ya Kuchunguza Matukio ya Kabla na Wakati wa 

Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, mwaka 2025, kutoka kwa Mwenyekiti wake, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman.

Alisisitiza dhamira ya serikali ni kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumishwa nchini, hivyo itachukua hatua zote muhimu kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa na Tume hiyo.

Rais Dk. Samia alisema hakutarajia tukio la vurugu za Oktoba 2025 kutokea  katika kipindi cha uongozi wake na tukio hilo limemtwisha mzigo mzito wa uongozi na uwajibikaji mbele ya wananchi.

“Nataka nikiri kwamba mimi binafsi sikutarajia kadhia hii ingetokea kwenye nchi yetu kipindi hiki nikiwa kiongozi mkuu wa nchi, jambo hili limenitwisha mzigo mzito mabegani kwangu,” alisema.

Rais Dk. Samia aliahidi kuubeba mzigo huo kwa ujasiri na umakini kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama.

“Kwa kadri Mwenyezi Mungu atakavyoniongoza na kunijalia, nitaubeba mzigo huu kwa ujasiri, kujiamini na tahadhari kubwa,” alisisitiza.

Alisema serikali imejipanga kuhakikisha matukio kama hayo hayajirudii nchini, kwa sababu tukio hilo lilitikisa taifa na kuacha maumivu kwa Watanzania.

Rais Dk. Samia  alisema serikali haitakaa kimya, bali itachukua hatua madhubuti kurekebisha pale ambapo udhaifu umeonekana.

Alieleza kwamba changamoto zilizobainishwa na tume si za kupuuzwa, bali kushughulikiwa kwa umakini. 

Alisema marekebisho yatahusisha kuimarisha taasisi, kuongeza uwajibikaji na kuhakikisha haki inatendeka bila upendeleo.

Alisema jukumu hilo haliwezi kubebwa na serikali pekee,  aliwataka wananchi wote kushiriki kikamilifu katika kujenga taifa, kwa sababu maendeleo na amani vinahitaji juhudi za pamoja.

Alikumbusha hakuna mtu au kundi linaloweza kubeba mzigo wa kulijenga taifa peke yake, alihimiza mshikamano na uwajibikaji wa pamoja kama msingi wa mafanikio.

Rais Dk. Samia aligusia umuhimu wa kujifunza kutokana na makosa ya nyuma, akisema taifa linapaswa kutumia uzoefu huo kama darasa la kujenga kesho iliyo bora zaidi.

Aliwataka Watanzania kuweka tofauti zao pembeni na kuunganisha nguvu kwa lengo la kulinda amani na kuimarisha maendeleo. 

VYOMBO VYA MAGHARIBI

Rais Dk. Samia alieleza kutoridhishwa na baadhi ya vyombo vya habari vya vilivyoripoti kadhia ya Oktoba 29, mwaka jana.

Alieleza kulikuwa na upotoshaji wa taarifa, kutoka kwa vyombo vya habari vya kimataifa, kwani havikuakisi uhalisia wa yaliyotokea.

Alisema baadhi ya taarifa zilikuwa zikiongeza chumvi au kupunguza ukweli, jambo lililochangia kuijengea picha hasi Tanzania katika jukwaa la kimataifa. 

Alisisitiza kuwa maumivu yaliyosababishwa na vurugu hizo ni ya Watanzania wenyewe, hivyo ni wao wanaopaswa kueleza simulizi sahihi ya kilichotokea.

Rais Dk. Samia alisema badala ya kupata faraja na mshikamano kutoka nje, baadhi ya vyombo hivyo vilionekana kutumia tukio hilo kama fursa ya kukosoa na kulaumu bila kuzingatia muktadha wa ndani wa nchi,  hali ambayo haikusaidia katika juhudi za kuponya taifa, bali kuongeza ‘presha’ na taharuki.

Rais Dk. Samia alionya kuwa ni muhimu kwa nchi kujenga uwezo wake wa kusimulia hadithi yake yenyewe, bila kutegemea tafsiri za nje ambazo zinaweza kuwa na maslahi tofauti. 

Alisisitiza umuhimu wa vyombo vya habari vya ndani kuwa makini, kitaalamu na vinavyozingatia maadili kuzuia pengo la taarifa kujazwa na simulizi zisizo sahihi.

Aliwahimiza Watanzania kutokuwa wepesi wa kuamini kila kinachoandikwa au kurushwa na vyombo vya nje, bali wawe na utamaduni wa kuchambua taarifa kwa kina. 

AIPONGEZA TUME

Rais Dk. Samia alisema tume hiyo ilifanya kazi katika mazingira magumu, lakini kwa uzalendo mkubwa na kwa kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa.

Alimpongeza Mwenyekiti wa Tume, Jaji Othman,  makamishna wa tume na sekretarieti kwa kazi waliyoifanya.

Rais Dk. Samia alisema matokeo ya uchunguzi yameweka bayana ukweli kuhusu kilichotokea, ikiwemo kubaini kuwa vurugu hizo zilipangwa, kuratibiwa na kufadhiliwa na watu wenye nia ya kuvuruga nchi.

Alisema malengo ya wahusika yalikuwa ni kuvuruga uchaguzi na kusababisha ombwe la uongozi,  kuingiza hali ya taharuki nchini, na miundombinu muhimu na huduma za kijamii zililengwa  kudhoofisha uchumi na mamlaka ya serikali.

Rais Samia alisisitiza kuwa juhudi za vyombo vya ulinzi na usalama zilisaidia kuzuia hali kuwa mbaya zaidi na kufafanua wale wote watakaobainika walikiuka sheria au taratibu watachukuliwa hatua bila upendeleo.

KUUNDA CHOMBO MAALUMU

Rais Dk. Samia alisema baada  ya ripoti hiyo, serikali itaunda chombo maalum cha uchunguzi wa jinai kuchunguza kwa kina waliohusika kupanga na kutekeleza vurugu hizo.

Alisema chombo hicho kitapitia madai ya watu waliopotea na vifo vilivyotokea, na wahusika wa uhalifu kama uporaji na uvamizi wa mali.

Rais Dk. Samia alisema serikali itagharamia matibabu ya majeruhi na kusaidia waliopata ulemavu wa kudumu kwa kuwapatia vifaa saidizi.

Aliahidi kuwa wafanyabiashara walioathirika wataangaliwa namna ya kufarijiwa kulingana na hasara walizopata.

Katika hatua nyingine, Rais Dk. Samia alitangaza kuwa serikali itaunda tume ya maridhiano itakayojumuisha wadau mbalimbali kurejesha mshikamano wa kitaifa.

Alisema mapendekezo ya tume hiyo ya maridhiano yatasaidia pia kuongoza mchakato wa marekebisho ya katiba.

AHIMIZA UTUNZAJI AMANI

Rais Dk. Samia aliwataka Watanzania kuendelea kudumisha amani na kuepuka kushawishiwa kuivuruga. Alisisitiza ni rahisi kupoteza amani, lakini ni vigumu kuirejesha. 

Alinukuu maneno ya hayati Mwalimu Julius Nyerere kuhusu umuhimu wa ujenga taifa lenye umoja badala ya mgawanyiko na alirejea fikra za Rais wa kwanza wa Ghana hayati Kwame Nkrumah, kuhusu umuhimu wa umoja katika kulinda rasilimali na uhuru wa nchi za Afrika.

Rais Dk. Samia alieleza kuwa changamoto hazipaswi kuwa sababu ya kufanya uharibifu bali zinapaswa kushughulikiwa kwa njia za kisheria na majadiliano.

Pia, aliwataka Watanzania kushirikiana na serikali kujenga taifa lenye amani, akisisitiza kuwa Tanzania haina mbadala na ni jukumu la kila mmoja kuilinda.

RIPOTI NI MALI YA RAIS

Akizungumzia ripoti hiyo, Rais Dk. Samia alieleza kuwa ripoti iliyowasilishwa ni mali ya Rais.   

Alisisitiza kuwa isitokee mtu mwingine akadai umiliki wa ripoti hiyo au kuichukulia kama yake, licha ya kuamua kuiweka wazi kwa wananchi.

Rais Dk. Samia alieleza kuwa uamuzi wa kuifanya ripoti hiyo iwe wazi ni tofauti na ilivyokuwa kwa tume za awali ambazo ripoti zake hazikuwekwa wazi. 

WADAU WA SIASA

Baadhi ya wadau wa masuala ya siasa waliipongeza tume hiyo na kusema imekidhi haja na matamanio ya Watanzania.

Mwanasiasa Mkongwe, Kate Kamba aliipongeza tume hiyo kwa kuwasilisha ripoti inayoonesha mwelekeo wa kuliponya taifa na kuimarisha amani.

Alisema kupitia ripoti hiyo amani ya nchi itaimarika na wanaojaribu kuichezea Tanzania hawatafanikiwa.

“Rais Dk. Samia ni kiongozi imara ameahidi atayafanyia kazi mapendekezo ya tume, hivyo Watanzania tunatakiwa tuwe wamoja, tuzungumze pamoja,  tuimarishe mshikamano na  umoja wetu kwa sababu hatujazoea vita,” alisema.

Mwanasiasa mkongwe, Hamad Rashid, alisema walioteuliwa katika tume hiyo wanao uwezo mkubwa na wametoa mapendekezo ya kisayansi na idadi ya vifo imethibitika.

Rais Dk. Samia aliunda tume hiyo Novemba 18, mwaka jana na ikaanza kazi  Novemba 20 mwaka jana, ikiongozwa na Jaji Chande  na wajumbe ni Jaji Mkuu Mstaafu, Profesa Ibrahim Juma, Balozi Ombeni Sefue, ambaye ni Mwanadiplomasia na Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu.

Wengine ni  Mwanadiplomasia na Balozi Radhia Msuya, Luteni Jenerali Paul Meela ambaye ni Mwanadiplomasia na Balozi mstaafu, Said Mwema, Mkuu wa Jeshi la Polisi Mstaafu, Balozi David Kapya, Mwanadiplomasia na Balozi mstaafu na Dk. Stergomena Tax, aliyewahi kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, na Katibu Mkuu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Previous Post

MSD YABAINISHA DHAMIRA KUIMARISHA USHIRIKIANO NA SEKTA YA AFYA BINAFSI

Next Post

UKWELI HADHARANI TUME YA JAJI CHANDE

Next Post
UKWELI HADHARANI TUME YA JAJI CHANDE

UKWELI HADHARANI TUME YA JAJI CHANDE

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Recommended

SIMBA SC YAWATOA HOFU MASHABIKI KUHUSU BAJABER

SIMBA SC YAWATOA HOFU MASHABIKI KUHUSU BAJABER

5 months ago
SIMANZI WATOTO WAKIFIA NDANI YA SWIMMING POOL

SIMANZI WATOTO WAKIFIA NDANI YA SWIMMING POOL

3 months ago

Popular News

  • WAZIRI MKUU AWASHUKIA WACHOCHEZI MIGOGORO

    WAZIRI MKUU AWASHUKIA WACHOCHEZI MIGOGORO

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • UKWELI HADHARANI TUME YA JAJI CHANDE

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • YASIJIRUDIE TENA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • MSD YABAINISHA DHAMIRA KUIMARISHA USHIRIKIANO NA SEKTA YA AFYA BINAFSI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • NDEJEMBI ATAJA VIPAUMBELE 10 SEKTA YA NISHATI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Stay Update, Subscribe Now!

Check your inbox or spam folder to confirm your subscription.

Ukurasa Rasmi wa Televisheni ya Gazeti la Uhuru.

Facebook-f Instagram X-twitter Youtube tiktok
Quick Links
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalum
  • Kolamu
  • Makala
Services
  • ePaper
Contact Information
  • Dar es Salaam,Tanzania
  • info@upl.co.tz
  • +255 783 925 742
Uhuru Publications , 2025 © All Rights Reserved
  • Terms & Conditions
  • Privacy Policy
  • FAQ
No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Contact
  • Hadithi

© 2026 JNews - Premium WordPress news & magazine theme by Jegtheme.

Are you sure want to unlock this post?
Unlock left : 0
Are you sure want to cancel subscription?