Na NASRA KITANA
KOCHA Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves, amesema anajivunia wachezaji wa kikosi chake, kwa kuendelea kujitoa kwa moyo wote kuipambania timu katika michuano inayowakabili.
Pia, amesema baada ya kuondolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) hivi sasa wanarejea katika mashindano ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho (FA) kusaka ushindi.
Hivi karibuni Yanga iliondolewa katika michuano hiyo, baada ya kuifunga mabao 3-0 JS Kablye katika mchezo wa hatua ya makundi uliochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu, leo watashuka dimbani kukabiliana na Cosmopolitian FC, katika mechi ya mzunguuko wa pili Kombe la FA (Shirikisho) itakayopigwa Uwanja wa KMC, Dar es Salaam saa 1:00 usiku.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Pedro alisema kila mchezaji ndani ya kikosi chake alijitoa vizuri katika michuano ya kimataifa na ligi, hivyo ana matumaini ya kufanya vizuri zaidi.
“Tumetolewa katika michuano ya ligi ya mabingwa Afrika, nguvu zetu zote tunazielekeza katika michuano ya ligi kuu na FA,” alisema.
Pedro aliahidi kuwa, timu hiyo haitakuwa tayari kupoteza mchezo kwa kuwa wamejipanga kupambana mwanzo mwisho kushinda, kufikia malengo waliojiwekea.
Kocha huyo aliwaomba mashabiki na wapenzi wa timu yao kuendelea kuiunga mkono timu yao ifanye vizuri.
Naye, mchezaji wa timu hiyo, Dikson Job alisema kwa upande wao wamejipanga kupata matokeo mazuri na kufikia malengo.
“Tumetolewa ligi ya mabingwa Afrika, lakini hatujakata tamaa, tutapambana kuhakikisha tunashinda kila mchezo wetu tuwe mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya FA, msimu ujao tutashiriki tena michuano ya kimataifa,” alisema Job.




