Na MWANDISHI WETU
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Siha imefungua mashauri matatu ya uhujumu uchumi namba 2831, 2834 na 2837 ya mwaka 2026 dhidi ya Dkt. Donatus Boniphace Tsete, Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma katika Hospitali ya Taifa ya Kibong’oto.
Mashauri hayo yalifunguliwa Februari 10, 2026 mbele ya Jasmin A. A., Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Siha, ambapo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo mlalamikaji.
Kwa mujibu wa TAKUKURU, mshtakiwa anakabiliwa na jumla ya makosa saba katika kila shauri.
Katika kosa la kwanza, anashtakiwa kwa matumizi mabaya ya madaraka kinyume na Kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/2007, kikisomwa pamoja na Aya ya 21 ya Jedwali la Kwanza, Kifungu cha 57(1) na 60(2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa, Sura ya 200 (Marejeo ya mwaka 2019).
Inadaiwa kuwa alitumia cheo chake vibaya na kufuja fedha zilizotengwa kwa ajili ya mpango wa usimamizi wa usugu wa dawa za kifua kikuu (Drug-Resistant Tuberculosis Mentorship) kwa Halmashauri ya Wilaya ya Same (Tsh. 5,082,000), Simanjiro (Tsh. 5,061,000) na Arusha (Tsh. 5,490,000).
Kosa la pili ni kughushi kinyume na vifungu vya 333, 335(1) na 337 vya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 (Marejeo ya mwaka 2022), kwa madai ya kughushi saini kwenye fomu za mahudhurio (attendance) kuonesha washiriki walilipwa fedha hizo.
Kosa la tatu linamhusisha na kuandaa nyaraka zenye maelezo ya uongo kinyume na vifungu vya 342 na 337 vya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 (Marejeo ya mwaka 2022). Nyaraka hizo zinatajwa kuwa ni hati za malipo pamoja na viambatisho vyake, ikiwemo dokezo la safari (travel memo) na orodha ya malipo (pay list).
Katika kosa la nne, anadaiwa kutumia nyaraka hizo kumdanganya mwajiri wake kinyume na Kifungu cha 22 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329 (Marejeo ya mwaka 2019).
Kosa la tano ni ubadhirifu wa fedha kiasi cha Tsh. 15,633,000 kinyume na Kifungu cha 28(1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
Kosa la sita ni kuisababishia mamlaka hasara ya kiasi hicho hicho cha Tsh. 15,633,000 kinyume na Aya ya 21 ya Jedwali la Kwanza, pamoja na vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi, Sura ya 200 (Toleo la mwaka 2019).
Kosa la saba ni kuwasilisha nyaraka zenye maelezo ya uongo kinyume na vifungu vya 342 na 337 vya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 (Toleo la mwaka 2019).
Mshtakiwa amekana mashtaka yote na amekidhi masharti ya dhamana yaliyowekwa na mahakama, hivyo yupo nje kwa dhamana.
Kesi imeahirishwa hadi Februari 23, 2026.
Katika hatua nyingine, mshtakiwa ameiomba mahakama ruhusa ya kuingia katika makubaliano ya kukiri kosa (plea bargaining) kwenye mashauri yote matatu. Mahakama imemtaka aandike barua kwa Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Kilimanjaro kuwasilisha ombi hilo na tayari ameandika barua akisubiri majibu.
Mashauri hayo yanaendeshwa na mawakili wa Serikali, Suzan Kimaro na Bernard Ndamallya kutoka TAKUKURU.




