Na ATHNATH MKIRAMWENI
KASI ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imeendelea kudhihirisha kwa vitendo dhamira ya kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli, hususan katika sekta ya afya.
CCM, Mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa ile inayofanya vizuri katika ukelezaji ilani ya uchaguzi, kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo hususan afya kwa lengo la kuokoa maisha ya wananchi.
Kasi ya utekelezaji miradi mikubwa ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali, ikiwemo Hospitali ya Wilaya ya Uvinza, imeleta sura mpya ya utoaji huduma na kuongeza imani ya wananchi kwa serikali yao.
Kupitia uongozi thabiti wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Serikali ya awamu ya sita imeendelea kuwekeza fedha nyingi katika kuboresha sekta ya afya.
Uvinza ni miongoni mwa wilaya zilizonufaika kwa kiasi kikubwa na uwekezaji huo, ambapo sh. bilioni 5.8, zimepokelewa kujenga na kuboresha huduma za afya.
Kati ya fedha hizo, sh. bilioni 4.3, zimetumika kujenga majengo mapya 15 ya kutolea huduma hospitalini hapo. Majengo hayo yanajumuisha jengo la wagonjwa wa nje (OPD).
Ujenzi wa maabara, mionzi, jengo la upasuaji, wodi za wazazi, watoto, magonjwa ya ndani kwa wanawake na wanaume, wodi za upasuaji, chumba cha kuhifadhia maiti, bohari ya dawa, jengo la kufulia na jengo la utawala.
Mbali na fedha za serikali kuu, wadau wa maendeleo wamechangia sh. milioni 89, huku halmashauri ikitoa zaidi ya sh. milioni 508 kutoka mapato ya ndani.
Wananchi wa Uvinza nao wameonesha uzalendo kwa kuchangia zaidi ya sh. milioni 3.5, na nguvu kazi zao katika kufanikisha ujenzi wa miundombinu hiyo.
Akizungumzia mradi huo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Dk. Maira Biseko, alisema maboresho yaliyofanyika katika hospitali ya Wilaya ya Uvinza, yameongeza uwezo wa hospitali kuhudumia wagonjwa wengi zaidi kwa wakati mmoja.
Alisema katika kipindi cha hivi karibuni, wagonjwa zaidi ya 2,000 walihudumiwa katika jengo la dharura, ambapo 914 sawa na asilimia 17 walipatiwa huduma ya haraka.
“Wagonjwa 42 pekee walipata rufaa kwenda Maweni Regional Referral Hospital kwa matibabu ya kibingwa zaidi. Kupungua kwa rufaa hizo ni ishara ya kuimarika kwa huduma ndani ya wilaya.
“Huduma za watoto wachanga, hususan watoto njiti na wenye uzito pungufu, zimeboreshwa hivyo kupunguza safari za rufaa na hatari kwa maisha ya watoto hao,”alisema.
Alieleza, kumekuwa na ongezeko kubwa la kina mama wanaojifungulia hospitalini badala ya majumbani, hatua inayochangia kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Alisema wananchi sasa wanapata huduma karibu yao, jambo linalookoa muda na gharama za usafiri kwenda hospitali ya rufaa mkoani.
Katika ziara ya kukagua miradi hiyo, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi alipongeza utekelezaji mzuri wa mradi na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kusimamia fedha za umma kwa uadilifu.
Aliridhishwa na uwiano wa thamani ya fedha na ubora wa majengo yaliyokamilika. Pamoja na mafanikio hayo, hospitali bado inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa watumishi na nyumba za kuishi watumishi hao.
Uongozi wa wilaya umeahidi kuendelea kushirikiana na serikali kuu kuhakikisha changamoto zilizopo zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Kihongosi alisema utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Wilaya ya Uvinza umeleta mageuzi makubwa katika sekta ya afya, umeimarisha ustawi wa jamii na kuthibitisha dhamira ya chama hicho kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli na endelevu.
Alisema ziara yake Uvinza, inalenga kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na serikali chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia.
Akiwa katika hospitali ya wilaya, alisema wamekagua miradi mbalimbali ikiwemo jengo la ICU na wameridhishwa na ubora wa majengo na vifaa tiba vya kisasa vilivyowekwa.
Alieleza kuwa, hospitali hiyo imepokea sh. bilioni 5.8 kutoka serikalini, wananchi na wadau wa maendeleo. Kati ya fedha hizo, sh. bilioni 4.3 zimetumika kujenga majengo 15 ya hospitali.
Aliwashukuru wadau wa maendeleo kwa kuchangia zaidi ya sh.milioni 89 na mapato ya ndani ya halmashauri yakichangia zaidi ya sh. milioni 508 na wananchi walichangia nguvu kazi na fedha zaidi ya sh. milioni 3.5.
Kuhusu changamoto, alitaja uhaba wa watumishi wa afya, lakini akakumbusha kuwa Rais Dk. Samia hivi karibuni alitoa ajira mpya 5,000 za watumishi wa afya kupunguza pengo hilo na kueleza imani yake kuwa tatizo hilo litapungua kadri muda unavyokwenda.
Alipokea ombi la ujenzi wa nyumba za watumishi na kumtaka mbunge wa eneo hilo,kuanzisha mchakato serikali iweze kuendeleza pale itakapowezekana.
Kihongosi aliwapongeza Mganga Mkuu na watumishi wote wa hospitali kwa kazi kubwa na ya kizalendo wanayoifanya, akisisitiza kuwa kazi ya afya inahitaji moyo wa kujitolea.
Alisema si muumini wa kuwalaumu watumishi wa afya kwa kuwa anatambua uzito wa majukumu yao, huku akiwapongeza kwa kazi kubwa wanayoifanya na kuwataka kuongeza juhudi.
Aliipongeza kamati ya siasa ya mkoa na wilaya, Mbunge na Diwani kwa usimamizi mzuri wa miradi, akisema thamani ya fedha inaonekana wazi katika majengo yaliyokamilika.
Alisisitiza umuhimu wa kudumisha umoja, kuepuka migogoro, fitina na majungu kazini kuongeza ufanisi.
Kihongosi alieleza, kazi ya uongozi ni wito na inapaswa kufanywa kwa bidii kwa maslahi ya Watanzania.
“Kwa niaba ya Rais Dk. Samia, nawashukuru viongozi na watumishi kwa mchango wao katika utekelezaji wa Ilani ya CCM, imani hii ni kubwa kwani ifikapo mwaka 2025–2030, ilani hiyo itakuwa miongoni mwa ilani bora kutokana na kasi ya utekelezaji inayoonekana,”alisisitiza.
Aliwataka viongozi na wananchi kuendelea kuiheshimu serikali na chama, na kuomba Mungu awasaidie katika kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na ufanisi.
Kwa upande wake Mariam Justin aliyefika kupata huduma katika hospitali hiyo, alimshukuru Rais Dk. Samia kwa huduma bora za afya zinazotolewa kwani vimewasaiidia wanawake wengi kujifungua salama.
” Sasa tuna uhakika na upatikanaji wa huduma za afya kwa sababu tukifika hospitali tumekuwa tukipokelewa vizuri na kuhudumia vizuri, kweli Rais Dk. Samia amefanya makubwa kwetu, hatuna cha kumlipa zaidi ya asante mama ” alisema.
Katika ziara hiyo, Mwenezi Kihongosi ameendelea kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ya afya mbali na mradi huo wa uvinza iko mingine iliyokaguliwa na kiongozi huyo wa Chama, kwa lengo la kutimiza azma ya Rais Dk. Samia ya kuwapatia afya njema wananchi kwa gharama nafuu.
Siyo miradi ya afya tu, bali iko mingine ya kiuchumi kama masoko na miundombinu ya barabara bila kuisahau ile ya elimu inayoendelea kutekelezwa na kukaguliwa na kiongozi huyo wa Chama.




