Na ELIZABETH JOHN
WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, amemwelekeza Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, kuwafukuza kazi Ofisa Mtendaji Mkuu na Menejimenti yote ya Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TAMESA), kufuatia tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka, ubadhirifu wa fedha na kusababisha usumbufu kwa wananchi wanaotumia vivuko, eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na wananchi wa eneo hilo, Waziri Mkuu, amesema serikali imepokea taarifa kuhusu kinachoendelea katika utoaji huduma za vivuko na changamoto zinazojitokeza na kuwakera wananchi mara kwa mara.
Amesema uchunguzi uliofanywa na timu ya wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za serikali, umeonesha wazi kuwepo matumizi mabaya ya madaraka na fedha.
Amezitaja taasisi hizo kuwa ni Ofisi ya Rais, Wizara ya Fedha, Wizara ya Ujenzi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Taasisi nyingine ni Vyombo vya Usalama vya Serikali, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma, Kitengo cha Kudhibiti Utakatishaji Fedha na Mamlaka ya Serikali Mtandao.
“Hawa ndiyo waliokagua, wakakuta wamekwapua zaidi ya sh. bilioni 2.5, kwa hatua hii tuchunguze nini kingine, hii ya uchunguzi juu ya uchunguzi ndiyo huwa inawapa kiburi na kuwafanya waendelee kuiba, hawa wafukuzwe kazi, wakamatwe na wapelekwe mahakamani,” alisema.
Mwigulu alimtaka Waziri Ulega, amwelekeze Katibu Mkuu, kuwafukuza kazi wote waliohusika na vyombo vinavyohusika, viwapeleke katika mkono wa sheria, uchunguzi uliofanyika una wajumbe wote wanaotakiwa kuchunguza.
“Kumekuwepo na matumizi mabaya ya madaraka na fedha, pengine ndiyo maana tunapata shida hii ya vivuko kuharibika mara kwa mara, kivuko kimekwama kwa kudaiwa sh. milioni 800, lakini katika taarifa ya upotevu wa fedha, watumishi wamekwapua sh. bilioni 2.5 maana yake, fedha hii ingekuwa imetumika vizuri, kivuko kingekuwa kinafanya kazi,” alisema.
Pia, alimtaka Waziri Ulega, achukue hatua zaidi, hata vivuko vinavyoharibika atafute mtu wa kuchunguza, zipo taarifa kuwa, vivuko vinatengenezewa mazingira ya kuharibika watu wapige dili katika matengenezo.
“Kwa kuwa hakuna anayekagua kama vimetengenezwa, watu wenye tabia ya wizi, wanaweza wakachomoa vyuma na kutanguliza kwa fundi ili wapate fedha ya matengenezo, tusipoangalia tutatengeneza vivuko kwa bei kubwa kuliko bei ya kivuko kipya, haya ni mambo yasiyokubalika’
Alieleza kuwa, uharibifu wa mara kwa mara wa vivuko, umeendelea kusababisha usumbufu mkubwa kwa abiria na magari, hali iliyofanya msongamano na kuchelewesha shughuli za kijamii na kiuchumi, huku gharama za matengenezo, zikiendelea kuongezeka bila kuleta matokeo yanayolingana na fedha zinazotumika.
“Hawa wamegawana vivuko viwili, yaani wameiba nauli na vivuko, haya ndiyo mambo yanayomuudhi Rais wetu (Dk. Samia Suluhu Hassan), lazima tuyakomeshe.
“Njia ya kuyakomesha, watumishi wote wanaobainika wala wasihamishwe wala kusimamishwa kazi, wafukuzwe na kufikishwa mahakamani, Tanzania hatuna uhaba wa vijana wa kuweza kufanya kazi,” alisema.
Waziri Mkuu, alimwagiza tena Waziri Ulega, kuwasiliana na Wizara ya Fedha, kuhakikisha fedha zinazohitajika kwa matengenezo ya vivuko, zinatolewa mara moja, kuwezesha vivuko vikamilike na virudi kutoa huduma kwa wananchi haraka iwezekanavyo.
Alieleza kuwa zaidi ya Dola za Marekani milioni tatu, zinahitajika kukamilisha kazi ambayo tayari imefikia asilimia 81, lengo vivuko virejee kazini na kutoa huduma bora kwa wananchi waliokuwa wakikabiliwa na usumbufu.
Aidha, Waziri Mkuu alielekeza fedha hizo ziunganishwe na sh. milioni 800 zilizotengwa kwa kivuko kingine kilicho katika hatua ya maendeleo ya asilimia 30, nacho matengenezo yote yakamilike kwa wakati.
Dk. Nchemba, aliagiza kwamba, malipo yafanyike mapema na ikiwezekana, matengenezo yakamilike ndani ya mwezi mmoja.
Alisisitiza kuwa Wizara ya Fedha, inafahamu umuhimu wa jambo hilo na haitaiacha kuchelewesha mchakato huo muhimu kwa wananchi wa Kigamboni.
Mwigulu, aliwapongeza wawekezaji wa sekta binafsi kwa mchango wao katika kupunguza ukubwa wa tatizo la usafiri wa vivuko, akisema ujio wao, umesaidia kupunguza msongamano na mateso kwa wananchi.
Waziri Mkuu, aliagiza vibali vitolewe mara moja kwa wawekezaji waliokidhi vigezo, hususan kutoka sekta binafsi, kupunguza mateso ya wananchi na kuboresha huduma bila kuathiri mpango wa serikali wa ushirikiano na wawekezaji.
“Mheshimiwa Waziri, waruhusuni wawekezaji waendelee kutoa huduma, maji yapo, abiria wapo, magari yapo, kwanini ichukue muda mrefu watu kupewa ruhusa.
“Haya ndiyo mazingira ambayo watu wanatengenezaga ubosi ili wapate rushwa, kwamba wanaendelea kuangalia, wakati kila kitu kipo wazi, waambie wataalamu wako kuwa, waziri mkuu ametoa ruhusa wao waandike barua, walete hicho kivuko cha mizigo na magari,”.
Alihoji kuwa, watu wa sekta binafsi, hata wakitaka kujenga daraja linalofunguka meli kubwa zikipita kwa nini uwazuie wakati wanatumia pesa yao?
Mwigulu alitumia fursa hiyo, kuwasilisha salamu za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kuwa amemtuma kuwahakikishia wananchi ahadi zote zilizotolewa wakati wa kampeni, zinaendelea kutekelezwa, huku nyingine zikiwa tayari zimeanza kutekelezwa.
Alieleza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita, inaendelea kutekeleza mipango mbalimbali katika sekta za afya, elimu na vijana, ikiwemo kuajiri watumishi wa afya, kujenga hospitali mpya, kuboresha huduma za dharura bila kuzingatia malipo ya awali na kuimarisha mazingira ya elimu.

Mwigulu, alisema serikali imetenga rasilimali kuwawezesha vijana, wanawake na makundi maalumu kiuchumi na kulinda biashara ndogo ndogo za wananchi kama sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kupambana na umaskini.
Alisisitiza kuwa, serikali haitavumilia watumishi wanaotumia vibaya madaraka waliyopewa, kukosa huruma kwa wananchi na kuchezea fedha za umma, akisema hatua kali zitaendelea kuchukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kufanya hivyo.
Mwigulu, alisema Tanzania ina watu wengi wenye uwezo, uadilifu na uzalendo wa kulitumikia taifa, hivyo hakuna sababu ya kuvumilia viongozi wanaosababisha mateso kwa wananchi na hasara kwa serikali.
Alimalizia kwa kusisitiza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita haijalala, inatambua changamoto za wananchi, inaendelea kuzitatua kwa vitendo, huku akitoa wito kwa viongozi wote kuwajibika, kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na kulinda maslahi ya wananchi.
WAZIRI ULEGA
Waziri Ulega, alisema Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, iliwaelekeza kwamba, wawe wanafanya shughuli za usafirishaji kwa ubia na kampuni binafs kupata huduma bora zaidi.
“Tunashukuru kampuni ya Said Salim Bakharesa, ilituunga mkono ikaja kuungana na kuifanya kazi hii kwa pamoja baada ya kuingia, imesaidia sana wananchi kuwa na uamuzi, mwenye uwezo wa sh. 500 kwenda katika kivuko cha muwekezaji na mwenye sh. 200 atasubiri kivuko cha serikali.
Alisema Wakala wa Ufundi na Umeme (TAMESA) kwa muda mrefu, imekuwa na kasoro kadhaa za kiutendaji na kinidhamu, waliunda tume ya kiserikali ya kukagua juu ya mwenendo katika shirika hilo kujua fedha zinazopatikana zinakwenda wapi, utendaji wa vivuko upoje na mengine.
“Nitumie fursa hii kuishukuru sana ofisi yako Waziri Mkuu, mlitusaidia sana kupata timu ya watu waadilifu waliofanya ukaguzi na kubaini ubadhilifu mkubwa uliokuwa unaendelea katika shirika hili.
“Mwanzoni mwa mwezi huu, nilifanya ukaguzi na viongozi wenzetu wa Mkoa wa Dar es Salaam, viongozi wawakilishi wa wannachi na baadae tukachukua hatua ya kumsimamisha kazi mtendaji mkuu wa TAMESA na timu yote ya Menejimenti yote, sasa hivi taratibu za kiutumishi zinaendelea ili watendaji hawa waweze kuchukuliwa hatua za kisheria itakapobainika kuwa ni wabadhilifu na wametumia vibaya madaraka ambayo wamepewa na serikali,” alisema.
Desemba 10, mwaka huu, Waziri Ulega, alimsimamisha kazi Ofisa Mtendaji Mkuu wa TEMESA pamoja na kurugenzi yake kufuatia uchunguzi uliofichua ubadhirifu wa zaidi ya sh. bilioni 2.5 ndani ya taasisi hiyo.
Hatua hiyo, ilifuatia ripoti ya tume maalumu iliyoundwa ndani ya miezi miwili kuchunguza tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma.
Ulega alitangaza uamuzi huo wakati wa ziara ya mradi wa maendeleo ya kivuko cha Nyunya Nyamisati na kutoa maagizo kwa wakandarasi kuongeza kasi ya ujenzi.




