Na ZIANA BAKARI
BAADHI ya wadau wakiwemo wachambuzi wa masuala ya siasa, wasomi, wachumi na viongozi wa dini, wametoa maoni tofauti, kuhusu hatua zinazochukuliwa na serikali kuwawezesha vijana kiuchumi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na UHURU wadau hao walipongeza serikali kuwezesha vijana kiuchumi na kuwatengenezea mazingira bora ya kujiajiri na kuajiriwa.
Katibu mstaafu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali Ngemela Lubinga, aliipongeza serikali kwa hatua hiyo kwa sababu inaleta tafsiri nzuri kwamba imejipanga kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana.
Alisema jambo la muhimu vijana wahakikishe wanakuwa na ujuzi utakaowasaidia kupata maarifa mbalimbali ya kuwapa mbinu za kujiajiri.
“Namuunga mkono Waziri Nanauka alichosema kwa sababu serikali ipo kwa lengo la kuwasaidia vijana kufikia malengo yao, niwasihi kukubali kujifunza na serikali isichoke kuwasaidia ,”alisema.
Mwanasiasa ambaye ni mdau wa maendeleo nchini, Abdul Kambaya, alimshauri Nanauka, kufuatilia fedha za mikopo ya vijana inayotolewa na halmashauri.
Alisema utaratibu huo utasaidia sehemu kubwa ya kujua takwimu za vijana waliopata fedha hizo na utendaji kazi wa kila hamshauri utaonekana.
Mtaalamu wa Uchumi, Profesa Samuel Wangwe, aliishauri serikali kuendelea kutoa elimu ya ujasiriamali kwa vijana, ambayo itakuwa chachu kupata ujuzi mbalimbali utakaowasaidia kupata kipato cha kujikimu kimaisha.
Katika hatua nyingine, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), Dk. Philip Daninga, alisema hatua ya serikali kuwawezesha vijana kiuchumi, italeta tafsiri ya kwamba imetoa kipaumbele zaidi kwa vijana.
Aidha, alibainisha moja ya changamoto kubwa iliyopo ndani ya jamii ni ajira hivyo, serikali imekuja na mwarobaini wa kuunda Wizara ya Vijana ambayo itahakikisha inawawezesha vijana kiuchumi na kijamii.
“Niwashauri vijana kuwa karibu na wizara hiyo kufuatilia fursa mbalimbali zitakazotangazwa wazichangamkie na kuhakikisha wanakuwa na ujuzi utakaowasaidia kujiajiri,”alisema.
Naye, Shekhe wa Wilaya ya Temeke, Zairay Hassan, aliwashauri vijana kuendelea kuiamini serekali kwa sababu jitihada wanazofanya ni kusaidia kuondoa changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana.
Desemba 23, mwaka huu, Nanauka, alisema serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuwawezesha vijana kiuchumi na kijamii, ikiwa ni utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2050 na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2025-2030.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam juzi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, alisema serikali inalenga kuhakikisha vijana wanapata ajira zenye staha, ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko na fursa za kujiajiri kupitia sekta mbalimbali za uzalishaji.
Alisema Ilani ya CCM, imeweka lengo la kuzalisha ajira zisizopungua milioni nane katika kipindi cha miaka mitano ijayo kupitia kuongeza uzalishaji, kuvutia uwekezaji na kukuza sekta zenye fursa kubwa kwa vijana.
Waziri Nanauka, alitaja changamoto zinazowakabili vijana kuwa ni ukosefu wa ajira, ajira zisizo rasmi na tija, upungufu wa ujuzi na changamoto ya mitaji kwa vijana wajasiriamali na kampuni changa.




