Na MWANDISHI WETU
SERIKALI imesema imeanza msako dhidi ya watumishi wa afya wanaofanya hujuma na kusababisha wagonjwa wakose huduma ndani ya hospitali za umma na kulazimika kwenda vituo vya binafsi.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, jijini Dar es Salaam, baada ya kubainika vitendo vya kuzima mashine za X-ray katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke, hatua iliyosababisha wagonjwa kukosa huduma muhimu na kuelekezwa katika vituo vya binafsi.
Waziri Mchengerwa alisema watumishi wote watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo watachukuliwa hatua za kisheria bila muhali.
Alisisitiza kuwa serikali haitavumilia hujuma zinazolenga kunufaisha sekta binafsi kwa kuwaumiza wananchi.
Mchengerwa alisema uchunguzi wa awali umebaini baadhi ya watumishi wasiokuwa waaminifu walizima mashine za X-ray kwa makusudi, licha ya kuwa vifaa hivyo vya kisasa vinafanya kazi kidijitali ‘Digital X-ray’.
Alisema taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kuhusu kuwepo mashine za X-ray zisizofanya kazi katika Hospitali ya Temeke siyo za kweli, bali ni matokeo ya hujuma zilizopangwa.
“Mashine zote za X-ray zilizopo Temeke zinafanya kazi na zimesimikwa kupitia uwekezaji mkubwa wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha huduma za afya nchi nzima,” alisema.
Alisema baada ya kupokea taarifa hizo, aliagiza kufanyika kwa uchunguzi wa kina kubaini ukweli.
Uchunguzi uliofanyika ulibaini kuwa hujuma hizo zilisababisha wagonjwa kukosa huduma ndani ya hospitali hiyo na kulazimika kwenda katika vituo binafsi vya afya.
Kwa mujibu wa Mchengerwa, vitendo hivyo ni usaliti mkubwa kwa serikali na wananchi na kwamba uchunguzi unaendelea kuwabaini wahusika wote, iwe ni mtu mmoja au zaidi.
“Natoa onyo kali kwa watumishi wote wa sekta ya afya, yeyote atakayehujumu huduma za afya kwa makusudi atachukuliwa hatua kali za kisheria na kinidhamu ikiwemo kufukuzwa kazi na kutopata ajira yoyote ndani ya hospitali, kama ni daktari tutamnyang’anya cheti chake na hatafanya kazi hata nje ya Tanzania,” alisisitiza.
Waziri Mchengerwa aliwahakikishia wananchi kuwa serikali itaendelea kusimamia kwa ukaribu utoaji wa huduma za afya na kuhakikisha vifaa vyote vinavyonunuliwa kwa fedha za umma vinatumika ipasavyo kwa manufaa ya wananchi.




