Na ATHNATH MKIRAMWENI
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ametoa ujumbe mzito wa mshikamano na matumaini kwa wananchi wa Zanzibar na Watanzania wote katika maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Amesisitiza Mapinduzi hayo, yameendelea kuwa nguzo ya kujenga jamii ya watu huru, yenye utu na maendeleo.
Amesema kuwa, maadhimisho hayo ni kumbukumbu ya historia muhimu na dira ya mustakabali wa Taifa.
Akitoa salamu za maadhimisho hayo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, Rais Dk. Samia, alisema kwa kipindi cha miaka 62, dhamira ya msingi ya Mapinduzi, imeendelea kulenga katika kujenga jamii inayozingatia misingi ya umoja, haki, amani na mshikamano.
Alieleza kuwa, tunu hizo zimeiwezesha Zanzibar kudumisha utulivu wa kijamii na kuendelea kupiga hatua za maendeleo katika nyanja mbalimbali.
Rais Dk. Samia, alisisitiza kuwa, mafanikio yaliyopatikana ni matokeo ya kulindwa misingi ya Mapinduzi iliyoasisiwa na waasisi wake.
Alisema tunu za Mapinduzi, zimeendelea kuwa dira ya uongozi na mshikamano wa wananchi, ndiyo msingi wa kuimarisha utu na usawa katika jamii.
Vilevile, Rais Samia, aliwataka wananchi kuendelea kubeba dhamana ya kulinda na kuendeleza tunu hizo kwa vitendo.
Alisisitiza kila kizazi kina wajibu wa kuzirithisha tunu za Mapinduzi kwa vizazi vijavyo, kulinda amani, umoja na maendeleo ya Zanzibar na Taifa kwa ujumla.
“Ninawatakia nyote kheri katika maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Kwa miaka 62, tumeendeleza dhamira ya msingi ya Mapinduzi ya kujenga jamii ya watu huru, yenye utu, yenye maendeleo, umoja, haki, amani na mshikamano.
“Sote tunao wajibu wa kuendelea kuzilinda tunu hizi na kuzirithisha kwa vizazi vijavyo, kama tulivyorithi kutoka kwa waasisi wetu,” alisema Rais Dk. Samia.
MAKAMU WA RAIS
Kwa upande wake, Makamu wa Rais Balozi, Dk. Emmanuel Nchimbi, naye alituma salamu za Mapinduzi kwa kuwatakia Watanzania wote kheri ya kumbukizi ya Siku ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Alisema siku hiyo ni ya kihistoria, inapaswa kutumika kama fursa ya kutafakari misingi na thamani ya Mapinduzi hayo kwa Taifa.
Balozi Dk. Nchimbi, alisisitiza kuwa, Mapinduzi yanapaswa kuenziwa siyo kwa kufanya kazi kwa bidii pekee, bali kwa kuoanisha kazi hizo na utu.
Alieleza kuwa, kufanya hivyo, Taifa litaendelea kusonga mbele kwa mshikamano, huku likijenga jamii yenye tabasamu la utu na maelewano.
Aidha, Makamu wa Rais, aliwataka wananchi kusherehekea kumbukizi hizo kwa amani na utulivu.
Pia, aliwahimiza Watanzania kuendelea kuulinda na kuudumisha Muungano wa Tanzania, huku akisisitiza mshikamano wa kitaifa ni nguzo muhimu ya maendeleo na ustawi wa nchi.
“Ninaungana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan, kuwatakia Watanzania wote kheri ya kumbukizi ya Siku ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
“Tuyakumbuke na kuyaenzi Mapinduzi haya, siyo kwa kufanya kazi kwa bidii pekee, bali kuoanisha kazi zetu na Utu. Hapo ndipo tutasonga mbele kwa mshikamano, tukijenga tabasamu la utu. “Tusherehekee kwa amani na utulivu, huku tukiendelea kuulinda na kuudumisha Muungano wetu,” alisema.
WAZIRI MKUU
Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, aliungana na Rais Dk. Samia, kuwatakia Watanzania wote kheri ya kumbukizi ya Siku ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Alisema kumbukizi hiyo ni fursa muhimu kwa Taifa, kukumbuka historia na misingi iliyojenga amani na maendeleo ya nchi.
Dk. Miwgulu, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha uzalendo, umoja, mshikamano na utulivu miongoni mwa wananchi.
Alieleza kuwa, tunu hizo, zimekuwa msingi imara wa amani na maendeleo ya taifa, ndiyo nguzo ya kudumisha mshikamano wa kitaifa.
Aliwahimiza Watanzania kuyaenzi Mapinduzi hayo siyo kwa kufanya kazi kwa bidii pekee, isipokuwa kuoanisha kazi zao na utu, kwani kufanya hivyo taifa litaendelea kusonga mbele kwa mshikamano, huku likijenga jamii yenye tabasamu la utu.
“Ninaungana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan, kuwataki Watanzania wote kheri ya kumbukizi ya Siku ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
“Tuendelee kuimarisha Uzalendo, Umoja, Mshikamano na Utulivu ambavyo vimekuwa msingi imara wa Amani na Maendeleo ya Taifa Letu.
“Tuyakumbuke na kuyaenzi Mapinduzi haya, siyo kwa kufanya kazi kwa bidii pekee, bali kuoanisha kazi zetu na utu.
“Hapo ndipo tutasonga mbele kwa mshikamano, tukijenga tabasamu la utu,” alisema.




