Na NJUMAI NGOTA,
Tabora
MGOMBEA Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema katika kipindi cha miaka minne na nusu, ambayo Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amekuwa madarakani, amesimamia kikamilifu, usalama wa nchi na kuviimarisha vyombo vya ulinzi na usalama.
Dk. Nchimbi, amesema hayo Kijiji cha Kigwa, Jimbo la Igalula, mkoani Tabora, alipohutubia mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara wa kampeni za Chama, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu.
Ameeleza zaidi kuhusu mafanikio makubwa ya Rais Dk. Samia katika uimarishaji wa vyombo vya ulinzi na usalama.
“Katika kipindi cha miaka minne na nusu, Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan, amesimamia kikamilifu usalama wa nchi.
“Ameimarisha vyombo vya ulinzi na usalama kwa idadi ya waajiriwa wake, mafunzo wanayopata, vitendea kazi na kuimarisha mbinu za kivita na medani,” alisema.
Pia, Dk. Nchimbi, amesema katika miaka mitano ijayo, wamedhamiria kuhakikisha usalama na amani ya Watanzania, inaendelezwa.
Amesema hatua hizo ni mwendelezo wa misingi iliyowekwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, ambaye alilijenga taifa kwa misingi ya haki, amani, mshikamano na inazidi kuimarishwa na Rais Samia kwa vitendo.
Dk. Nchimbi, amesema mafanikio hayo, hayawezi kuzungumzwa bila kumtambua Rais Samia kama kiongozi aliyebeba dhamana kwa moyo wa kizalendo na kiu ya maendeleo ya watu wake.
Mgombea mwenza huyo, ameeleza kuwa, hayo yote yamefanyika chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia.
Katika mkutano huo, Dk. Nchimbi amesimikwa kuwa Mtongi msaidizi wa Chifu Hangaya, akipewa heshima ya jina la Nyungu la Mawe.
Dk. Nchimbi, amesema amepokea kwa unyenyekevu nafasi hiyo ya kumsaidia Chifu Hangaya katika safari ya maendeleo.
“Nawashukuruni kwa heshima hii ya kuwa Mtongi wa Chifu Hangaya. Sisi kule Songea, tunamwita kiongozi mkuu Zulu na msaidizi wake Nduna.
“Kwa lugha ya kwetu, Mama Samia ni Zulu, mimi ni Nduna. Nitalitumikia jukumu hili kwa heshima kubwa,” alisema.
MIRADI MIKUBWA YA MAENDELEO
Akieleza mipango ya CCM kwa miaka mitano ijayo, Dk. Nchimbi, alisema Chama kimejipanga kutekeleza miradi mikubwa katika sekta mbalimbali za kilimo, elimu, afya, viwanda, maji, na uchukuzi.
Katika sekta ya kilimo, alisema serikali itaimarisha utoaji wa ruzuku ya mbegu na mbolea, kuwajengea uwezo maofisa ugani na kujenga skimu za umwagiliaji katika maeneo ya Lula, Majengo Bora, Sheria, Mwamabondo, Miswaki, Sitaki na Goweko.
Kwa upande wa wafugaji, Dk. Nchimbi, alisema serikali itakarabati na kujenga malambo, machinjio, majosho na kuendelea kutoa ruzuku ya dawa na chanjo kwa mifugo.
ELIMU
Kuhusu sekta ya elimu, Dk. Nchimbi, alieleza serikali itajenga shule mpya za msingi tatu, sekondari mbili na kuongeza madarasa katika shule zilizopo.
Pia, aliahidi kujenga hospitali, vituo vya afya vinne na zahanati tisa.
Kwa upande wa biashara, alieleza mpango wa kujenga soko la kisasa na stendi ya kisasa Igalula, kukuza biashara na kuboresha maisha ya wakazi wa jimbo hilo.
Aidha, Dk. Nchimbi aliahidi kukamilika kwa reli ya kisasa ya SGR itakayopita katika maeneo ya Makutopora-Tabora (kilometa 368), Tabora-Isaka (kilometa 165), Mwanza-Isaka (kilometa 341), Tabora-Kigoma (kilometa 508) na Uvinza-Msongati (kilometa 282).
MAJI
Dk. Nchimbi, alisema lengo la serikali ni kufikisha huduma ya maji safi na salama kwa asilimia 90 kwa wakazi wa Igalula.
Alisema mradi mkubwa unaotarajiwa ni upanuzi ule wa kutoka Ziwa Victoria, kufikia vijiji 15, ujenzi wa bwawa na chujio la maji Shitage na Kizengi.
Pia, Dk. Nchimbi, alisema barabara za jimbo hilo zitajengwa kwa lami na nyingine kwa changarawe.
Katika mkutano huo, Dk. Nchimbi, alimwombea kura Mgombea Urais wa CCM, Dk. Samia, wagombea ubunge na udiwani.