Na HANIFA RAMADHANI,
Pemba
MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema CCM inajivunia kwa kufanya kampeni za kistaarabu, kisayansi na kuyafikia makundi yote ya wananchi Unguja na Pemba.
Amesema CCM, inatarajia ushindi wa kishindo kutokana na namna ilivyofanya kampeni zake na kunadi sera nzuri na hamasa kubwa waliyoipata kwa wananchi katika kila mkutano.
Dk. Mwinyi, aliyasema hayo, akifunga kampeni zake za Urais katika Kisiwa cha Pemba huko Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Alisema wamefanya kampeni za kistaarabu na wameweza kunadi sera kwa kuyafikia makundi yote Unguja na Pemba.
Alisema wakati CCM inanadi sera zake, vyama vingine visivyokuwa na sera, vilikuwa vikihubiri matusi na kejeli kila vikipanda majukwaani.
“Wazanzibari hawataki kusikia hayo, hawataki kusikia matusi wala kejeli, wanachotaka wao ni kusikia nini tutafanya katika kipindi cha miaka mitano ijayo,” alisema.
Alisema Chama Cha Mapinduzi, kimefanya mikutano mingi ya hadhara ya makundi yote Unguja na Pemba.
Pia, alisema Chama kilijinadi kwa kuyasema yake ambayo kimeyafanya katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na kueleza nini kitafanya kipindi kijacho.
Alisisitiza kuwa, Oktoba 29 ni siku ambayo wananchi wataamua hatma ya nchi na kuwataka wasibweteke, kwani ndiyo siku ya maamuzi.
Vilevile, aliwataka wananchi kuichagua CCM kwa lengo la kulinda tunu za kitaifa kama vile Mapinduzi na Muungano.
DK. DIMWA
Naye, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk. Mohammed Said Mohammed ‘Dimwa’, alisema CCM ilifanya kampeni zake kwa ustaarabu mkubwa na kwamba, kampeni zilikuwa za kitaalamu bila ya kumbughudhi mtu.




