Na HANIFA RAMADHANI,
Zanzibar
MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewaomba wananchi kuhakikisha kuwa, wanajitokeza kwa wingi Oktoba 29, mwaka huu kuipigia kura CCM.
Dk. Mwinyi, aliyasema hayo katika mkutano wa kufunga kampeni za Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa upande wa Zanzibar, Viwanja vya Mnazi Mmoja Mjini Unguja.
Alisema kampeni ni jambo moja na kupiga kura ni hatua muhimu ambayo itakihakikishia Chama ushindi wa kishindo.
Pia, alisema kampeni zimefanywa kwa ustaarabu mkubwa na kwamba, wameyafikia makundi yote, kila walipopita wananchi waliahidi kukipatia Chama ushindi.
Aidha, Dk. Mwinyi, alitumia nafasi hiyo, kujiombea kura na kumwombea kura Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia na wagombea wa ubunge, uwakilishi na udiwani wa CCM.
DK. SHEIN
Rais wa Zanzibar mstaafu na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Dk. Ali Mohammed Shein, alisema uchaguzi ni tukio la hesabu na zinazohesabiwa ni kura zinazopigwa na mwenye kura nyingi ndiyo mshindi.
Alisema kwa vuguvugu aliloliona katika kampeni za CCM bara na Zanzibar, wingi wa wanaCCM na wananchi waliohudhiria katika mikutano hiyo, inadhihirisha kuwa, ushindi wa kishindo hauna shaka.
Pia, alisema ni lazima wananchi wakapige kura kwa kuzingatia amani, utulivu umoja na mshikamano na kuwataka wakishapiga kura kila mmoja atulie nyumbani kwake akisubiri matokeo.
Aliongeza kuwa, wananchi wakapige kura kwa lengo kuimarisha Muungano kwani ndiyo hazina ya nchi na jukumu kubwa la maendeleo.
Naye, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mjini, Talib Ali Talib, alisema watahakikisha Oktoka 29, Dk. Samia ndiye atakayekuwa Rais wa Tanzania na kuwa, sababu ya kufanya hivyo wanayo.
Alisema katika kipindi kifupi cha uongozi wake, amefanya mambo makubwa na ametekeleza ilani ya CCM kwa vitendo pamoja na kuimarisha amani nchini.
Pia, alisema watahakikisha Dk. Mwinyi anapata ushindi wa kishindo kwa upande wa Zanzibar kutokana na mambo makubwa na utekelezaji wa ilani uliotukuka ndani ya kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake.




