Na MWANDISHI WETU
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ametangaza kuwa, Oktoba 29, mwaka huu kuwa siku ya mapumziko, kuwawezesha Watanzania wote kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, uamuzi huo, unafuatia tangazo la Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), lililobainisha kuwa, siku hiyo, itatumika kupiga kura za kumchagua Rais, Wabunge na Madiwani.
Taarifa hiyo, ilieleza kuwa, Rais Dk. Samia, ametumia mamlaka aliyopewa chini ya Sheria ya Sikukuu za Kitaifa, Sura ya 35, kuidhinisha siku hiyo kuwa ya mapumziko kwa nchi nzima, wakiwemo watumishi wa umma na wafanyakazi wa sekta binafsi.
Hatua hiyo, inalenga kuhakikisha wananchi wenye sifa za kupiga kura, wanashiriki kikamilifu mchakato wa kidemokrasia bila vikwazo vya kikazi au shughuli nyingine za kila siku.
Serikali ilitoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kwa wingi katika vituo vyao vya kupigia kura na kusisitiza umuhimu wa kudumisha amani, utulivu na heshima kwa misingi ya demokrasia katika mchakato huo.




