Na MWANDISHI WETU
MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafirishaji Ardhini (LATRA), imesema inatoa vibali kwa waendeshaji daladala katika Jiji la Dar es Salaam, wenye mabasi yenye uwezo wa kubeba abiria 26 na zaidi, kutoa huduma kwa Njia ya BRT( I), ambako vituo vya mwendokasi vimeharibika.
Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Habibu Suluo, alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari, huku akiwataka wasafirishaji hao kujitokeza kuomba vibali kwa njia ya mfumo wao na wale watakaowahi watapewa kipaumbele.
“Hii inatokana na changamoto ya njia ya mwendokasi ambayo imejitokeza katika Mradi wa BRT I, kutoka Mbezi Luis, Kimara kuingia Posta, Muhimbili, Makumbusho, ambapo jumla ya nafasi 150 zipo kwa wasafirishaji wenye utayari,” amesema.
Amesema, vibali hivyo vinatolewa kwa miezi mitatu wakati DART ikiendelea kufanya marekebisho ya miundombinu ya barabara hiyo.
Kwa upande wa BRT II ya kutoka Gerezani kwenda Mbagala, amesema barabara hiyo haina utaratibu mpya kwani ni kituo kimoja tu cha Mbagala Zakiem kilichopata changamoto, hivyo baada ya marekebisho yake mwekezaji Mofat, ataendelea kutoa huduma kama kawaida.




