NA SELINA MATHEW, Dodoma
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kitaisimamia serikali na hakitasita kuwachukulia hatua viongozi wavivu, wazembe na watakaojihusisha na vitendo vya rushwa.
Kimesisitiza kuwa, viongozi wa aina hiyo, watakuwa na wakati mgumu kipindi hiki, ambacho Chama hakitakuwa na mzaha katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya 2025 – 2030.
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, aliyasema hayo jijini hapa, wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisisitiza kuwa, kile ambacho Watanzania waliahidiwa, lazima kitekelezwe, hivyo viongozi wanapaswa kuwajibika ipasavyo.
Alisema wataweka vipimo vya uwajibikaji na utendaji kazi wa viongozi wa serikali, kwa kuchekecha utendaji wao.
“Yule ambaye ufanisi wake utakuwa ni chini, Chama kitachukua hatua mara moja.
“Wale watakao fanya vizuri, Chama kitendelea kuwalinda kuhakikisha kazi yenye matunda mema kwa Watanzania inafanikiwa,” alisema Kihongosi.
Alisema Chama kimetoka mbali na Watanzania, kina historia kubwa, hivyo hakitaruhusu mambo yaharibike kwa namna yoyote.
Alisisitiza hatua zitachukuliwa kwa viongozi ambao watashindwa kutimiza wajibu wao.
“Tunawaomba Watanzania, waendelee kuwa watulivu, imani kwa CCM na serikali inayotokana, kesho yetu Watanzania ni njema kuliko jana.
“Maono ya Rais Dk. Samia ni kuona taifa linapiga hatua kubwa ya maendeleo, hivyo tutaendelea kusimamia misingi ya upendo, amani, umoja, mshikamano, kuheshimiana na kustahimiliana katika utendaji wetu wa kazi,” alisema.
Aliwapongeza viongozi walioapishwa juzi huku akiwaeleza kuwa, wanapaswa kutambua kwamba, Rais Dk. Samia ana kasi ya kuijenga Tanzania iliyo bora, uteuzi wao una maana kuwa anawaamini na watampa majawabu.
“Hivyo, Chama kinawataka mawaziri na naibu mawaziri, waende kufanya kazi kwa weledi, wasimwangushe Rais Samia.
“Viongozi hawa, wengi ni wapya, kuja kwao katika serikali, maana yake kuna wengi hawakupata fursa ya kuteuliwa.
“Kipindi wanafurahia uteuzi huo na wamekula kiapo kuingia kwao ofisini, wakumbuke kuwa Rais Samia, hana mchezo, anataka kazi na utendaji uliotukuka, uliojaa utu ndani yake kwa Watanzania.”
Alisisitiza kuwa Chama Cha Mapinduzi, hakitasita kuchukua hatua kwa kiongozi yeyote mzembe na mla rushwa ndani ya serikali iliyoundwa na CCM.
UTEKELEZAJI WA ILANI
Kuhusu utekeleza wa ilani ya Uchaguzi 2025 – 2030, kupitia ahadi za mgombea, Kihongosi aliwataka kutambua kuwa, wajibu wa Chama ni kuisimamia serikali, siyo serikali kukisimamia Chama.
“Chama ambacho kimetafuta kura, kimeunda serikali, sasa tunakwenda kuisimamia serikali kikamilifu na ndiyo maana nimewataka wateuliwa waende kuwajibika kwa sababu, hatua zitachukuliwa kwa kiongozi wa serikali, awe mteuliwa au mchaguliwa.
“Nchi inaongozwa kwa misingi ya sheria, hivyo Chama kinaamini utendaji kazi. Hatuamini kwa watendaji wazembe, wala rushwa hao wakibainika watafikishwa mahakamani moja kwa moja,” alisisitiza Kihongosi.
RAI YAKE
Alitoa rai kwa watendaji wa serikali, kufanya kazi kuhakikisha wanakidhi matarajio na maono ya Rais Samia.
“Mtu asiende ofisini akafanya kazi zake binafsi, akajiangalia yeye na kuacha dhamana ambayo amepewa, Chama kitachukua hatua kali kwa watendaji wazembe,” alisisitiza Kihongosi.
Alisema kazi imeanza, Chama kitaifuatilia serikali kuhakikisha yaliyoahidiwa katika kampeni, yanatekelezwa.
Pia, alisema wataweka mkazo zaidi kusimamia ahadi zitakazotekelezwa ndani ya siku 100.
Alisema Chama, kinazitaka wizara wizara zinazohusika na sekta zinazohusiana na ahadi katika siku 100, waendelee kuwajibika kikamilifu.
Alisema wakati Rais Samia akizindua Bunge la 13 Novemba 14, 2025, alitoa hotuba ya ujenzi wa mshikamano wa kitaifa katika kuwaletea Watanzania maendeleo.
“Ilikuwa hotuba ya msamaha na huruma kwa kuwa, aliviomba vyombo vya sheria, kuwasamehe vijana waliofanya vurugu siku ya uchaguzi kwa kufuata mkumbo
.”Ilikuwa hotuba ya mlezi na mtoto kwa taifa lake, unaweza kuita hivyo, sababu aliwausia vijana, kuwa yeye na wazazi walipokuwa vijana, wangefanya hayo tusingekuta Tanzania yenye umoja, amani, maadili na upendo iliyopo sasa,” alisema Kihongosi.
SHUKRANI KWA WATANZANIA
Kihongosi alitumia fursa hiyo, kuwashukuru Watanzania, wanaCCM na vyama vingine vya siasa waliojitokeza kupiga kura siku Uchaguzi Mkuu, Oktoba 29, mwaka huu.
Hata hivyo, Kihongosi aliwasihi Watanzania kuilinda amani ya taifa kwa kuwapuuza na kuwakataa wanaochochea uvunjifu wa amani.




