>> Ni kauli ya Waziri Simbachawene, awataka wananchi kuendelea na maisha ya kawaida, serikali imejipanga kukabili tishio lolote
>> Jeshi la Polisi lasema utulivu umetokana na operesheni za ushirikiano kati yao na vyombo vingine vya ulinzi na usalama
Na ATHNATH MKIRAMWENI
SERIKALI imesema hali ni shwari nchini, imewataka wananchi kuendelea na shughuli za uzalishaji mali kama kawaida.
Akizungumza na gazeti hili, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, alitoa wito kwa wananchi kuendelea na maisha ya kawaida na serikali imejipanga vyema kukabili tishio lolote la uvunjifu wa amani.
Simbachawene, alitoa taarifa baada ya siku mbili, serikali ilipotoa tamko la kuwataka Watanzania, kuadhimisha miaka 64 ya Uhuru wakiwa nyumbani.
Waziri Simbachawene, aliwataka Watanzania kuwa watulivu, aliwahakikishia uimara wa vyombo vya ulinzi na usalama kuwa, vinafanya kazi muda wote.
Alisema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi, linaendelea kuimarisha ulinzi, miito ya maandamano inayosambaa mitandaoni, isipewe nafasi.
Alisema jukumu la Serikali na vyombo vyake ni kuendelea kusimamia usalama muda wote, ingawa kuna namna ya utekelezaji inayoweza kubadilika kulingana na mazingira katika kipindi husika.
TEKNOLOJIA ZA KISASA
Alieleza kuwa, nchi imewekeza katika teknolojia mbalimbali za kisasa zinazohusika kufuatilia na kufanya tathmini, hivyo mamlaka zitabaki makini kuangalia mienendo yote inayoashiria viashiria vya hatari kuzuia madhara kabla hayajatokea.
Simbachawene aliongeza kuwa, kama kutatokea dalili zozote za tishio, serikali itapambana kuhakikisha mwananchi anabaki salama.
Pia, Simbachawene aliwashukuru wananchi kutii maagizo ya serikali na kusimama na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kulinda amani ya taifa, akisema utulivu uliopo ni matokeo ya ushirikiano kati ya wananchi na viongozi wao.
KAULI YA POLISI
Kwa upande wake, Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini, David Misime, ameendelea kuwaonya wanaopanga maandamano ya amani yasiyokuwa na kikomo.
Taarifa yake iliyosambazwa kwa vyombo vya habari nchini, iliwakikishia wananchi hali ya usalama, imeendelea kuwa shwari, baada ya hatua mbalimbali kuchukuliwa usiku wa kuamkia Desemba 10, mwaka huu.
Uimara ya usalama huo, umetokana na operesheni za ushirikiano kati ya polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kufanyika kwa ufanisi.
Alisema Jeshi la Polisi, limeendelea kufuatilia kwa karibu makundi yanayohamasisha maandamano wanayoyaita; Ya amani na yasiyo na kikomo,” ambayo tayari yalipigwa marufuku tangu Desemba 5, 2025.
Jeshi hilo, limesema maandamano hayo, yalikosa kufuata matakwa ya Katiba ya mwaka 1977 na Sheria ya Polisi na Polisi Wasaidizi Sura ya 322.
Pia, Polisi walisema uchunguzi wao, umebaini uwepo wa mipango iliyokuwa ikipangwa kupitia klabu za mitandaoni na njia nyingine za mawasiliano, ambako wahusika walikuwa wakihamasishana kuvuruga shughuli za kiuchumi na kijamii nchini.
Hata hivyo, jeshi hilo, limekuwa likifuatilia mienendo hiyo muda mrefu na limefanikiwa kuzuia jaribio la maandamano hayo tangu Desemba 9, mwaka huu, ambayo yalikiuka sheria na utaratibu wa nchi.
Taarifa hiyo imeendelea kuonya yeyote atakayekiuka sheria kwa kushiriki kupanga au kutekeleza vitendo vinavyolenga kuhatarisha usalama wa nchi na kusimamisha shughuli za wananchi, atachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.
“Tunawahakikishia wananchi wote, tutaendelea kulinda usalama wa nchi yetu, sambamba na maisha na mali zenu muweze kuendelea na shughuli zenu kama kawaida,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, Jeshi la Polisi, lilitoa wito kwa wananchi kuendelea kufanya shughuli zao bila hofu, kufuata maelekezo ya vyombo vya ulinzi na usalama na kutii sheria za nchi.



