DODOMA
NA MWANDISHI WETU
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amepokea hati za utambulisho kutoka kwa mabalozi watano walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao ambapo amesisitiza dhamira ya Tanzania kuimarisha ushirikiano unaojengwa kwa misingi ya kuheshimiana, maendeleo ya pamoja na mahusiano mema.
Katika halfa hiyo iliyofanyika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma, Dk. Samia aliweka msisitizo kwamba Tanzania na serikali wanazotoka mabalozi hao, zinachangia dhamira ya pamoja katika kukuza biashara, uwekezaji na maendeleo.
Pia, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kidiplomasia katika kukuza sekta muhimu za biashara na uwekezaji, kilimo, afya, elimu, nishati, uchumi wa buluu, utalii na teknolojia.
Mabalozi na waliowasilisha hati zao ni Domingos de Almeida da Silva Coelho, Balozi wa Angola, Marjo Johanna Jacoba Crompvoets, Balozi wa Ufalme wa Uholanzi na Mohammad Javad Hemmatpanah, Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Wengine ni Ivan Lančarič, Balozi wa Jamhuri ya Slovakia na Gabriel Pandureni Sinimbo, Balozi wa Jamhuri ya Namibia.
Rais Dk. Samia pia alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika sekta za afya, elimu, uchumi wa buluu, utali, teknolojia.
Katika sekta ya elimu, alieleza dhamira ya serikali kuimarisha mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana kupitia ushirikiano na nchi zenye utaalamu wa kiteknolojia ili kuwapatia vijana ujuzi utakaowezesha kuajiriwa au kujiajiri.
Vilevile, alizipongeza nchi hizo kwa mchango wao katika safari ya maendeleo ya Tanzania na kuhimiza ushirikiano wa kina zaidi unaoendana na Dira 2050 na Sera ya Mambo ya Nje inayotilia mkazo diplomasia ya uchumi, ushirikiano wa kimkakati na ushiriki hai katika majukwaa ya kikanda na kimataifa.
Katika hatua nyingine, Rais Dk. Samia aliwahakikishia mabalozi hao hali ya amani, utulivu na usalama nchini, akisisitiza kuwa Tanzania inabaki kuwa mahali salama kwa wananchi wake, wawekezaji na wafanyabiashara.
USHIRIKIANO NA ANGOLA
Ushirikiano huo unahusisha sekta za biashara, nishati, madini, uchumi wa buluu, mifugo na utalii,
USHIRIKIANO NA UHOLANZI
Ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Uholanzi unahusisha sekta za kilimo, afya, elimu, uvuvi, maji na uwekezaji.
USHIRIKIANO NA IRANI
Ushirikiano uliopo baina ya Tanzania Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umejikita katika sekta za biashara, nishati, teknolojia, kilimo, afya na elimu.
USHIRIKIANO NA SLOVAKIA
Ushirikiano na taifa hilo unaakisi maeneo ya nishati jadidifu, ubunifu wa kidijitali, uzalishaji viwandani, usalama wa mtandao, elimu na utalii.
Slovakia imefungua hivi karibuni ubalozi wake nchini Tanzania, hatua inayochochea ushirikiano wa muda mrefu wa kiuchumi na maendeleo.
USHIRIKIANO NA NAMIBIA
Ushirikiano unahusisha biashara, uchumi wa buluu, nishati, madini, mifugo na utalii. Pia, ugunduzi wa mafuta na gesi nchini Namibia ni fursa ya kujenga uwezo wa pamoja na ushirikiano katika mnyororo wa thamani wa nishati katika siku zijazo.
Wakati huo huo, Rais Dk. Samia amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali ambapo kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk. Moses Kusiluka, ilisema Fortunatus Makore Magambo ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mifuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).
Kabla ya Uteuzi huu, Magambo alikuwa Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaj na Miradi katika mfuko huo huku Plasduce Mkeli Mbosca ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).




