Na AMINA KASHEBA
WADAU wa ngumi za kulipwa nchini, wamempa mbinu bondia Hassan Mwakinyo za kushinda katika pambano lake dhidi ya Stanley Eribo wa Nigeria.
Wakizungumza jijini Dar es Salaam kwa nyakati tofauti, Wadau hao walisema Mwakinyo anatakiwa kuweka mbele nidhamu ya mchezo, kujiamini na kutomdharau mpinzani wake.
Pambano hilo lisilo la ubingwa raundi 10 uzito wa kati linatarajiwa kufanyika Desemba 26, mwaka huu Ukumbi wa Warehouse uliopo Masaki, jijini Dar es Salaama
Bondia mkongwe,Rashidi Matumla, alisema jambo la kwanza Mwakinyo anapaswa kufanya mazoezi kwa bidii kwa kuwa, yatampa nguvu ya kushinda pambano hilo.
“Anapaswa kujiamini, kuwa na nidhamu ya mchezo na kutomdharau mpinzani wake kwa sababu ana rekodi nzuri,” alisema Matumla.
Mkongwe huyo aliongeza kuwa Mwakinyo anatakiwa kufuata mafunzo aliyopewa na makocha wake.
Bondia wa zamani wa kick boxing, Japhet Kaseba, ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mabondia wa Ngumi za Kulipwa Tanzania, alimtaka Mwakinyo kucheza kwa kujiamini.
“Kila kitu kinawezekana kwa kuwa rekodi hiyo ya Mnigeria inaweza kufutwa kama hajawahi kupigwa ni muda wa Mwakinyo kupambana na kuweka rekodi ya kumpiga Eribo.
“Kitu kingine anatakiwa kujiamini, kuwa na nidhamu na kutomdharau mpinzani wake maana na yeye anaenda kujipanga kwa lengo la kupata ushindi ugenini,” alisema Kaseba.
Naye bondia, Feriche Mashauri, alisema ana imani Mwakinyo atafanya vizuri kwa kumpiga na kumaliza pambano mapema, japo awamu hii kuna ugumu kutokana na Mwakinyo kukaa nje ya ulingoni muda mrefu.
Katika rekodi ya mabondia hao,Mwakinyo amecheza jumla ya mapambano 27, ameshinda 24 na kupoteza mapambano matatu ajawahi kutoka sare.
Bondia Eribo amepanda ulingoni mara 19, ameshinda mapambano 18 na kutoka sare pambano moja hajawahi kupigwa.
Mwakinyo mara ya mwisho kupanda ulingoni ilikuwa Novemba 16, mwaka 2024, alipomchakaza kwa TKO raundi ya tisa katika pambano la kutetea mkanda wake wa Ubingwa wa WBO dhidi ya bondia, Daniel Lartey kutoka Ghana.




