Na MWANDISHI WETU
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amelitaka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kuendelea kuimarisha ulinzi kwa kuwa, ulinzi imara ndiyo msingi wa amani na maendeleo ya nchi.
Amesema hakuna maendeleo bila amani, hivyo JWTZ inategemewa kuendeleza usalama na amani, wananchi waendelee kushiriki kikamilifu shughuli za kila siku.
Rais Samia aliyasema hayo mkoani Tanga, alipozungumza katika Mkutano wa Tisa wa Mkuu wa Majeshi (CDF) na Makamanda, uliyofanyika Shule ya Kijeshi ya Ulinzi wa Anga (SKUA).
“Hakuna maendeleo bila amani, sasa Jeshi la Wananchi wa Tanzania likiwa chombo muhimu cha ulinzi wa ndani na nje ya nchi, linategemewa kuendeleza usalama na amani, wananchi waendelee kushiriki kikamilifu shughuli za maendeleo.
Alisema mbali na kuwekeza katika mafunzo na mazoezi ya kijeshi, pia ushirikiano na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ni muhimu katika kudhibiti matishio ya usalama ukiwemo ugaidi.
Rais Samia, alifafanua kila chombo kina majukumu yake, lakini dhima kuu ni ulinzi wa uhuru, mamlaka na heshima ya nchi.
Vilevile, Rais Samia, alisema muda mrefu, JWTZ imeendelea kuwa mfano katika ukanda wa Afrika na Dunia kwa ujumla kutokana na weledi, nidhamu na utii.
Pia, aliwapongeza wanajeshi wanawake kwa kushiriki katika fani mbalimbali za urubani, uhandisi, udaktari na maeneo mbalimbali ya kiteknolojia.
Alisema wanawake wanaendelea kuthibitisha uwezo katika maeneo mbalimbali ya kijeshi, zikiwemo fani za urubani.
“Wanawake wanaendelea kuthibitisha uwezo katika maeneo mbalimbali ya kijeshi, katika fani za urubani, nilipokwenda kuangalia ndege zile za mafunzo tulizonunua, nimekuta marubani wanawake wako pale,”alisema.




