Na LILIAN JOEL, Arusha
VILIO na majonzi vimetawala katika Kijiji cha Kimnyaki, kilichopo Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, baada ya watoto wawili wa familia moja kupoteza maisha wakati wakiogelea katika bwawa (swimming pool) la Kilimanjaro Court, lilipo katika moja ya hoteli maarufu wilayani humo.
Akizungumza kwa masikitiko makubwa, msemaji wa familia ya watoto hao ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Kimnyaki, Samwel Meliyo, alisema tukio hilo lilitokea Januari 7, mwaka huu, majira ya saa 9:00 alasiri.
Meliyo aliwataja waliofariki kuwa, ni Abednego Joachim (13), ambaye mwaka huu alitarajiwa kuanza kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Serikali ya Mwanderi na Ebenezer Joachim (9), ambaye alikuwa anasoma darasa la tatu katika shule ya Blue Berry.
“Tumepokea msiba huu kwa mshtuko na masikitiko makubwa, kwa sababu watoto hawa waliondoka na mama yao mzazi wakiwa wazima lakini, baada ya muda mfupi tukapata taarifa kwamba wamepoteza maisha wakiogelea,” aliongeza.
“Nilipojulishwa kwamba kuna msiba umetokea hapa bomani nilidhani babu wa watoto hawa mzaa baba yao, kwa sababu ni mgonjwa alitibiwa Selian kisha kupewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya KCM, lakini baada ya kufika nikajulishwa siyo yeye ni watoto, nilipata mshtuko mkubwa,” alisimulia kwa maumivu.
Kwa mujibu wa Meliyo, hawezi kueleza kwa kina kilichowasibu watoto wao wakati wakiogelea kwani mama yao mzazi ambaye alikuwa nao amelezwa hospitalini kutokana na hali yake kutokuwa nzuri, huku baba yao akiwa katika hali ngumu ya mawazo.
Aidha, Meliyo alitumia fursa hiyo kuiomba serikali kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wamiliki wa eneo hilo kutokana na uzembe uliosababisha watoto hao kupoteza maisha, akidai inawezekana hapakuwa na wa kuangalia watoto wakiogelea.
“Tumejulishwa kwamba meneja wa eneo hilo na watu wengine wanne wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha. Niiombe serikali ichukue hatua kali za kisheria pale itakapobaini kulikuwa na uzembe,”aliomba.
Kuhusu mazishi ya watoto hao, Meliyo alisema yatafanyika Januari 10 mwaka huu, nyumbani kwao Kimnyaki na kwamba hali za wazazi wa watoto hao siyo nzuri.
Mmoja wa wanafamilia aliyejitambulisha kwa jina la Kenyata Joel maarufu (Dad), alisema alipigiwa simu na baba wa marehemu, akimuomba awahi Hospitali ya St. Joseph, iliyopo jirani na eneo hilo kwa madai kwamba watoto wamepata ajali.
“Nilikuwa Ngaramtoni, nikatoka mara moja nikidhani wamepata ajali ya gari lakini nilipofika hospitalini hapo nilikuta ni ajali ya maji kisha tukaenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mount Meru, lakini watoto walikwishafariki,” alifafanua kwa huzuni.
MBUNGE
Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Johannes Lukumay, alitoa rai kwa wamiliki wa maeneo ya kuogelea katika jimbo hilo kuajiri watumishi wenye taaluma ya kuogelea ili tatizo likitokea uokozi ufanyike kwa haraka bila kuleta majanga.
Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto Mkoa wa Arusha, Oswad Mwanjenjele, alikiri kulijua tukio hilo lakini, hawakupata taarifa mapema hivyo marehemu hao waliokolewa na watu wengine.




