AMINA KASHEBA Na SIMON NYALOBI
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za rambirambi kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, kufuatia kifo cha mwanamuziki mkongwe, Steven Hiza, kilichotokea nyumbani kwake, jijini Tanga.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na kutiwa saini na Error! Filename not specified.Shaaban Kissu kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Rais Dk. Samia alimtaja marehemu Hiza kuwa msanii mahiri na mzalendo aliyetumia kipaji chake kuelimisha, kuburudisha na kuhamasisha jamii.
Pia, Hiza alitumia sanaa kama chombo cha kuimarisha maadili, umoja na utambulisho wa Taifa.
“Hiza, aliyewahi kuhudumu katika bendi ya muziki ya Atomic JazzBand, atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika kukuza na kuendeleza muziki wa Tanzania, hususan kupitia wimbo wake maarufu wa ‘Tanzania Yetu ndiyo Nchi ya Furaha,’ wenye hisia za uzalendo na mshikamano wa kitaifa,” alisema Rais Dk. Samia kupitia taarifa hiyo.
Rais Dk. Samia alitoa rai kwa wanamuziki na wadau wa tasnia ya muziki nchini kudumisha na kuenzi mchango wa Hiza kwa kuendeleza misingi ya uzalendo, ubunifu na uzalishaji wa kazi za sanaa zenye tija kwa taifa.
Rais Samia alitoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa, wanamuziki, wadau wa sanaa na Watanzania wote kwa ujumla.
Aidha, aliwaombea wafiwa uvumilivu, faraja na moyo wasubira katika kipindi hiki kigumu cha msiba, huku akimwomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu Hiza mahali pema peponi.
HIZA KUZIKWA LEO
Katibu Mkuu wa Chama cha Muziki wa Rhumba Tanzania, Hassan Msumari alisema jana, Hiza anatarajiwa kuzikwa leo katika makaburi ya Gossage, yaliyopo jirani na ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), mkoani Tanga.
Msumari alisema hayo alipozungumza na gazeti hili kutoka mkoani Tanga na kueleza kuwa Hiza alifariki dunia juzi, nyumbani kwake Mwanzange.
Hiza alitamba na wimbo wa ‘Tanzania Yetu’ akiwa na bendi ya Atomic Jazz, uliomwezesha kupata tuzo ya heshima na kupewa sh. milioni 50 na Rais Dk. Samia.
Kwa mujibu wa Msumari, Hiza alikutwa na umauti nyumbani kwake, ikiwa ni siku moja baada ya kufanya shoo.
“Mzee Hiza amefariki dunia na nguvu zake, alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa pumu kwa takriban miaka 20. Jumapili alikwenda kutumbuiza na aliporudi nyumbani usiku alivyolala ndiyo moja kwa moja hakuamka.
“Mkongwe huyu ameacha alama kubwa nchini kwani amefanya mambo mengi kupitia wimbo wa ‘Tanzania Yetu’ ambao utaendelea kuishi miaka yote,” alisema Msumari.
Katibu huyo alisema utaratibu wa kupumzisha mwili wa mwanamuziki huyo katika nyumba yake ya milele unaendelea nyumbani kwake.
“Tunaishukuru serikali yetu chini ya Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan kwani aliweza kuona mchango wake na kumpa shilingi milioni 50. Pia, taarifa za kifo cha Hiza tulimweleza Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma ‘Mwana FA’ na amekuja msibani,” alisema.
ALLY CHOKI
Mwanamuziki Ally Choki alisema Hiza alikuwa kioo kwa waimbaji wengi nchini kwa kuwa alitunga nyimbo zenye maadili na kuishi katika jamii.
“Tutamuenzi kwa kufanya kazi kwa bidii na kutunga nyimbo zenye maadili, Hiza ameacha alama kubwa katika taifa letu, hivyo vijana wanapaswa kusikiliza nyimbo zake kuongeza uelewa,” alisema Choki.
BASATA
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), limesema Hiza ameacha alama kwa wimbo wake wa ‘Tanzania Yetu’ ambao umebeba taswira kubwa ya taifa.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kaimu Katibu Mtendaji wa BASATA, Edward Buganga alisema Tanzania imepata pigo kubwa kwa kuondokewa na mwimbaji huyo ambaye alikuwa tunu ya nchi.
“Mzee Hiza alikuwa tunu ya taifa kwa sababu sauti yake aliitumia vizuri hadi hivi sasa wimbo wake unaendelea kuishi vizazi na vizazi, pia ameacha pengo katika tasnia ya muziki kutokana na aina ya uimbaji wake.
“BASATA kwa ujumla tumehuzunika na msiba huu kwa sababu alikuwa mwimbaji mwenye uwezo mkubwa hadi Rais Dk. Samia alimpa fedha kutokana na mchango wake katika nchi kupitia kipaji chake,” alisema Buganga.
Kaimu Katibu huyo alisema mkongwe huyo alitumia sanaa kama sehemu ya kufikisha ujumbe na kuitangaza nchi kupitia nyimbo.
“Wito wangu kwa vijana ambao ndiyo wanaanza kazi ya sanaa kuiga mfano wa Hiza kwa sababu amekuwa na mchango mkubwa katika taifa hili na mwalimu wa mashairi kwa wanamuziki wengi nchini,” alisema Buganga.
JEFF WA SIKINDE
Mwanamuziki mkongwe wa bendi ya Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde Ngoma ya Ukae’ Habib Jeff, alisema kifo cha Hiza, kimepunguza washauri wa muziki huo kwa vijana.
Jeff alisema Hiza alikuwa mwalimu mahiri wa kufundisha misingi ya muziki wa dansi nchini, hivyo kifo chake kimeacha pigo.
“Nimepata taarifa za msiba wa Mzee Steven Hiza, kusema kweli tumempoteza mtu ambaye alikuwa anawasaidia vijana kukua katika muziki kutokana na uzoefu wake,” alisema.
Jeff alieleza mchango wa mwanamuziki huyo hautasahaulika hususan katika wimbo wake maarufu wa Tanzania Yetu na nyingine.
Mkongwe huyo aliwaomba wanamuziki kuendelea kujifunza kutoka kwa Hiza kwa kuwa historia yake ya muziki imetapakaa nchi nzima.
LUIZA MBUTU
Mkurugenzi wa bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’ Luiza Mbutu, alisema Hiza, ameacha funzo kwa wanamuziki wa hivi sasa la kujikita kutunga nyimbo zitakazodumu.
“Mzee wetu ametuachia funzo kwetu kwamba, tutunge nyimbo zitakazodumu muda mrefu, kama alivyotunga wimbo wa Tanzania Yetu, ambao licha ya miaka mingi kupita bado unaendelea kutamba,” alisema.
Luiza alisema wimbo wa Tanzania Yetu anaufahamu tangu akiwa mdogo, lakini hadi hivi sasa unaendelea kupendwa kutokana na maudhui yake.
Mwenyekiti huyo wa zamani wa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA), alisema alibahatika kuonana na mwanamuziki huyo ana kwa ana, mwaka jana.
PAPA UPANGA
Mwanamuzi wa zamani wa bendi ya Msondo Ngoma, Issihaka Katima ‘Dj Papa Upanga’, alisema Hiza, ameacha nembo muhimu kupitia wimbo wake wa Tanzania Yetu.
Dj Papa Upanga alibainisha kuwa, mwanamuziki ameacha nembo kupitia wimbo wa Tanzania Yetu ambao hautasahaulika.
“Hiza ataendelea kukumbukwa nchini kupitia wimbo wake, ambao ni gumzo kila mahali, hata sisi tunaopiga katika bendi zetu za mitaani mashabiki hawawezi kukuelewa bila ya kusikia wimbo huo kutokana na maudhui yake,” alisema.
Mwanamuziki huyo alisema alipokea taarifa za kifo cha Hiza kwa masikitiko makubwa, huku akisikitika kutokwenda katika maziko ya mwanamuziki huyo kutokana na kukabiliwa na changamoto za maisha.




