Na MWANDISHI WETU
KAMISHNA Msaidizi Mwandamizi wa Polisi ( SACP), Faustine Mafwele na wenzake 42, wanatarajiwa kutoa ushahidi, katika kesi ya kughushi vibali vya kumiliki silaha, inayowakabili watu tisa wakiwemo maofisa wa polisi.
Pia, kutakuwa na nyaraka mbalimbali zikiwemo maelezo ya onyo ya washitakiwa, vibali vya kumiliki silaha, fomu za maombi ya kumiliki silaha na hati ya ukamataji mali.
Wakili wa serikali, Cathibert Mbiling’i, amedai hayo leo Machi 16, 2026, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Geofrey Mhini, shauri lilipopelekwa kuwasomea washitakiwa hoja za awali.
Katika kesi hiyo, washitakiwa ni Fedrick Malekela, Kalemwa Kaunga, John Kaposwe, Edger Mlogo, Robert Titus na Julieth Moshi, ambao ni maofisa wa polisi.
Wengine ambao siyo maofisa wa polisi ni mkulima Damson Mnyilenga, mfanyabiashara Simon Aloyce na Venrand Liberio ambao wote wanakabiliwa na kesi hiyo.
Baada ya washitakiwa kusomewa hoja za awali, walikiri taarifa zao binafsi, ambazo ni majina yao, umri, makazi na kazi yao, huku wakikana kutenda kosa.
Hakimu Mhini, baada ya kusikiliza hoja hizo, amesema kesi hiyo itasikilizwa siku tatu mfululizo kuanzia Aprili 8 hadi 10, mwaka huu na washitakiwa wapo nje kwa dhamana.
Katika kesi hiyo ,washitakiwa hao wanadaiwa kughushi vibali 16 vya kumiliki silaha vyenye majina ya watu mbalimbali.
Ilidaiwa kuwa, vibali hivyo vilikuwa na majina ya Ahmed Abdallah, Ahmed Sandrudin, Omary Abdallah, Robart Koka na Arafathi Ally.
Wengine ni Mohamed Salim, Suleman Mbewa, Mickdadi Chakindo, Irfan Nafiri, Gulamabas Najafi, Ismail Ismail, Salim Salim, Marwaan Habretsh, Maurice Kutiwe na Said Mohamed.




