Na MWANDISHI WETU
HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili-Mloganzila, hapotoshi kutokana na wanawake wengi kuchangamkia kwa kasi kubwa upasuaji wa kuongeza makalio.
Unaambiwa hivi; upasuaji wa makalio hivi sasa umepiku upasuaji wa matiti.
Pia, imesema matokeo ya upasuaji wa matiti huonekana mara moja huku makalio huchukua baada ya siku 21 kupona.
Akizungumza na Uhuru leo, Daktari Bingwa wa Upasuaji na Mkuu wa Idara ya Upasuaji Mloganzila, Dk. Erick Muhumba, amesema huduma ya kuongeza makalio ndiyo inaonekana kuhitajika zaidi tofauti na matiti.
Amesema wagonjwa wengi waliopata huduma hizo wanaonyesha kuridhishwa na matokeo kutokana na huduma nzuri wanazotoa.
“Kwa takwimu zetu tunavyotoa huduma ya upasuaji wa kuongeza makalio inaongoza zaidi kushinda ya matiti, naona ni kutokana na baadhi ya watu wanapenda kubadilisha maumbo yao hata watu maarufu hunufaika na huduma zetu.
“Katika kazi zetu hizi za upasuaji wa kuongeza makalio tuliwahi kupata changamoto moja ambapo mgonjwa alipata maambukizi katika kidonda, lakini baada ya kupatiwa matibabu alirejea katika hali yake ya kawaida na kupona vizuri, tunamshukuru Mwenyezi Mungu tunaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi,” amesema.
Akizungumzia maumivu yanayoweza kutokea baada ya upasuaji, amesema hayana tofauti na yale yanayotokea katika upasuaji mwingine wowote, huku akisisitiza wagonjwa wote hufuata taratibu za kawaida za maandalizi kabla ya kufanyiwa upasuaji.
Aidha, amesema kwa wale wanaotumia dawa za kujichubua ngozi, virutubisho mbalimbali au wanaovuta sigara hushauriwa kusitisha matumizi hayo kwa muda kupunguza hatari ya kupata madhara wakati na baada ya upasuaji.
“Kwa kuwa huu sio upasuaji wa dharura, tunampa mgonjwa muda wa kujiandaa, tunashauri aache matumizi ya dawa za kujichubua, kuacha kuvuta sigara kwa kipindi kinachoshauriwa kabla ya kufanyiwa upasuaji,” amesema.
Akifafanua kuhusu matokeo ya upasuaji, amesema kwa upande wa matiti, mabadiliko huanza kuonekana mara moja baada ya upasuaji, huku kwa upande makalio umbo kamili huanza kuonekana baada ya wiki tatu siku 21.
Amesema kidonda cha upasuaji wa makalio huanza kupona ndani ya wiki moja, huku mgonjwa akiendelea kutumia dawa za antibiotiki kwa siku tano hadi saba kulingana na ushauri wa daktari.
Dk. Muhumba, amesema katika upasuaji wa kuongeza makalio, madaktari huchukua mafuta chini ya ngozi ya tumbo, kisha kuyachakata na kuyahamishia katika makalio kupata umbo linalohitajika.
Amesema baada ya upasuaji mgonjwa hatakiwi kukalia moja kwa moja makalio kwa muda wa siku 21, bali anapaswa kutumia mto maalumu au taulo kukalia mapajani kulinda matokeo ya upasuaji.
Aidha, amesisitiza kuwa kidonda cha upasuaji hakipaswi kuloweshwa na maji hadi pale kitakapopona kwa mujibu wa maelekezo ya daktari.
Kuhusu uwezo wa kupata watoto, Dk. Muhumba alisema upasuaji wa kuongeza makalio au matiti haumzuii mwanamke kupata ujauzito wala kunyonyesha, kwani huduma hizo hazina athari kwa uwezo wa uzazi.
Amewashauri wanawake ambao hawaridhiki na maumbo yao na wanahitaji kuyabadilisha kufika Hospitali ya Mloganzila kwa ushauri na huduma kutoka kwa madaktari bingwa kuhakikisha usalama na matokeo bora.




