Na AMINA KASHEBA
SERIKALI imewataka Watanzania kujipanga na kuchangamkia fursa katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).
Michuano hiyo inatarajiwa kufanyika kwa mara ya kwanza katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.
Akizungumza Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo wa Taifa (BMT), Neema Msitha amesema Watanzania wanatakiwa kuchangamkia fursa mbalimbali kuhakikisha wananufaika na fainali hizo.
“Mashindano ya Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), tuliona Watanzania mbalimbali walivyonufaika nayo kwa kujiongezea kipato kupitia biashara zao.
“Tunaomba Watanzania wajipange kuhakikisha wanachangamkia fura zitakazojitokeza katika michuano ya AFCON 2027, kwani kuna fursa mbambali ambazo wakizitumia vizuri zitawasaidia kujiongezea kipato,” amesema.
Katibu huyo alisema Watanzania wanatakiwa kuhakikisha wanatumia vizuri fursa za mashindano ya AFCON kwani kutakuwa na wageni wengi ambao watakuja nchini.
“Usishangae uwanjani wakajaa wageni kuliko wenyeji kutokana na ukubwa wa mashindano hayo na watu ambao watakuwa wanakuja kusindikiza timu zao, kujifunza na kufuatilia michuano.
“Watanzania wasione mashindano ya AFCON 2027 yapo mbali, hivyo waanze maandalizi ya mapema kuhakikisha wanafikia malengo waliyojiwekea,” amesema.
Katibu huyo alitoa shukrani kwa Watanzania ambao waliojitokeza kwa wingi katika michuano ya CHAN 2024 na kuipa sapoti yakutosha Taifa Stars ambayo ilitolewa hatua ya robo fainali.