Na NJUMAI NGOTA,
Mbogwe
MGOMBEA Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, ameahidi serikali ijayo ya Chama, imejipanga kuhakikisha wachimbaji wadogo wa madini, wanapewa kipaumbele kwa kutengewa maeneo maalumu ya kuchimba, kuwainua kiuchumi na kuchochea maendeleo ya taifa.
Dk. Nchimbi, amesema hayo, katika Shule ya Msingi Masumbwe, wilayani Mbogwe, mkoani Geita, alipozungumza na mamia ya wakazi wa wilaya hiyo, katika mkutano wa kampeni za CCM, kueleza utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020-2025, kunadi Ilani mpya ya mwaka 2025-2030 na kumwombea kura Mgombea Urais wa Chama, Dk. Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani.
“Kama mmegundua maeneo ya wachimbaji wadogo, yameongezeka na leseni zimeendelea kutolewa.
“Tunasema, tunakwenda kutenga maeneo maalumu kwa wachimbaji wadogo kwa sababu, hawa ndiyo wanaokuja kuwa matajiri wakubwa baadaye, wanachangia maendeleo na wanalipa kodi kwa upendo.
“CCM tumedhamiria kuwapa mazingira bora ya kufanikisha shughuli zao kwa kutenga maeneo maalumu ya uchimbaji,” amesema.
Amebainisha kuwa, tofauti na ulipaji kodi kwa lazima, wachimbaji wadogo wa Tanzania, hulipa kodi kwa hiyari na kwa moyo wa uzalendo, wakijua wanajenga taifa.
“Mtu akiwa Mtanzania, anachangia kwa upendo akijua anajenga taifa lake,” amesema.
UTAFITI WA MADINI KUIMARUSHWA
Kuhakikisha sekta ya madini inazidi kukua kwa tija, Dk. Nchimbi, alisema serikali chini ya CCM, itaimarisha utafi ti wa madini kwa kuongeza bajeti ya shughuli hizo kutoka asilimia 16 ya sasa hadi asilimia 50.
“Tunataka watu wetu wawe na taarifa sahihi. Wakijua mahali kuna madini, waombe leseni na waanze kazi bila kubahatisha. Hii itapunguza migogoro ya ardhi na kuongeza tija katika sekta hii,” amesema.
SERA NA SHERIA MPYA ZA MADINI
Balozi Nchimbi, amesisitiza wataweka mkazo kwa kutunga sera na sheria mpya, zitakazolinda maslahi ya wachimbaji wa Tanzania hususan maeneo ya madini ya kimkakati.
“Vilevile tunakwenda kubadili sera, kutengeneza sheria ambazo zitawalinda wachimbaji wa Tanzania hasa katika madini ya kimkakati.
“Mtanzania anachangia kwa upendo akijua anajenga taifa lake,” amesema.
Akielezea mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne wilayani humo, Dk. Nchimbi amesema leseni za utafi ti wa madini zipo 41.
“Kwa nini tunafanya utafi ti Mbogwe, kwa sababu imedhihirika watu wa Mbogwe wengi wanapenda kujishughulisha na uchimbaji, lakini hakuna maeneo.
“Hivyo, lazima tutafute maeneo zaidi watu wachimbe, kwa sababu Mwenyezi Mungu ametupa baraka ya madini maeneo mbalimbali nchini, tunatakiwa kufanya utafi ti, tufanye kazi ya kuyatafuta yatuletee maendeleo,” amesema.
Pia, leseni za wachimbaji madini katika wilayani humo zimetolewa 548 na za maeneo tengefu 147.
Kwa upande wake, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Bukombe ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amewaomba wananchi wilayani humo na Watanzania kwa ujumla, wajitokeze kwa wingi siku ya kupiga kura na kumchagua Dk. Samia, Balozi Dk. Nchimbi, wabunge na madiwani.