NA MUSSA YUSUPH,
Tabora
BURUDANI ya muziki kutoka kwa wasanii ililirindima katika viwanja vya Nanenae Ipuli mkoani Tabora katika kampeni za Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Safari hii walikuwa Samia Kings ambao walishusha burudani kabambe iliyomfanya Dk. Samia kusimama jukwaani kujumuika na wananchi kuimba wimbo wa Tunaimani na Samia na kuacha gumzo mkoani hapa.
Kundi hilo la Samia Kings linawajumuisha wakongwe wa Bongo Fleva, Chege Chigunda ‘Chege’, Madee Ally ‘Madee’ na Ambwene Isaya ‘AY’.

Mbali na wimbo huo, wakongwe hao waliimba wimbo wa Ukimuona Mama Samia ambao nao ni maalum kumnadi Dk. Samia.
Wimbo huo uliwainua wagombea ubunge na udiwani ambao walikusanyika usawa wa jukwaa kuu kuimba na kucheza wimbo huo.
Kadhalika, maelfu ya wananchi waliohudhuria mkutano huo uliofanyika jana, walikonga mioyo yao kupitia burudani zilizoporomoshwa na wasanii wa miondoko ya bongo fleva, singeli, dansi, kwaya na ngoma za asili.
Wasanii wa singeli waliwavutia mashabiki, msanii Whozu alikuwa wa kwanza kufungua jukwaa kwa wimbo wake ‘Piga kelele kidogo’ unaotikisa katika mikutano hiyo.
Whozu ambaye alitinga jukwaani akiwa amevalia fulana nyeusi yenye nembo ya CCM, alitawala kila kona ya jukwaa.
Baada ya Whozu, magwiji wa muziki wa dansi, Patcho Mwamba na Charles Baba wakiongoza kundi la wasanii la Mama Ongea na mwanao, iliwadia muda wa kutoa burudani.

Kundi hilo liliangusha burudani tamu kwa mtindo wa mdura kupitia kibao chao maarufu ‘Yu wapi.’
Wimbo huo ni maalumu kumnadi Dk. Samia ukielezea miradi mbalimbali aliyoitekeleza na fursa za kiuchumi alizozifungua.
Wasanii wengine waliojumuika katika kundi hilo ni Chuchu Hans, msanini wa vichekesho Mr. Zumo, Dokii, Lamata na Mzee Pembe.
Wengine ni Muhogo mchungu, Jasiri, Asha boko na wengine wengi ambao walihitimisha burudani yao kwa sebene la nguvu.
Khadija Shaaban maarufu kama ‘Keysha’ alivurumisha burudani kwa wimbo wake wa ‘Kazi na Utu’.
Msanii huyo ambaye aliwahi kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Dodoma, wakati akiimbia wimbo huo vijana wa hamasa kutoka vyuo vikuu walijumika naye uwanjani kwa kucheza wimbo huo uliopigwa kwa mahadhi ya rhumba.
Baada ya wasanii hao kupanda jukwaani, ilifika muda wa Tanzania One Theatre (TOT) kushusha vitu vitamu.
Bendi hiyo maarufu nchini ilipiga ngoma zake pendwa kama Big up CCM ikiambata na miondoko ya Reggae.
“Bila Chama Cha Mapinduzi, nchi ingekuwa wapi. Bila Chama Cha Mapinduzi, mshikamano ungekuwa wapi…bila Chama Cha Mapinduzi, wapinzani wangetoka wapi,” waliimba sehemu ya mashairi ya wimbo huo.

Ilipotimu saa 11:04 msafara wa Dk. Samia uliingia uwanjani hapo huku shangwe, nderemo zikitawala kutoka kwa wananchi kumpokea mgombea huyo wa Urais.
Wakati msafara ukiingia uwanjani, TOT walimsindikiza Dk. Samia kwa wimbo wa ‘Sasa Kumekucha’.
Msafara huo wa Dk. Samia ulinogeshwa zaidi ya maandamano ya baiskeli, wabeba miamvuli na kikundi cha matarumbeta kutoka Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM).
Wakati hayo yakijiri kiongozi wa bendi hiyo, Malkia wa mipasho, Khadija Kopa, alihitimisha burudani kwa kibwagizo maalumu kwa wapinzani.
Hiyenahiyena zilitawala uwanjani hapo kutoka kwa maelfu ya wananchi waliofurika kumsikiliza mgombea huyo wa Urais kupitia CCM.