Na SULEIMAN JONGO,
Mbeya
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amesema Chama kinafanya kazi kubwa ya kuleta mabadiliko kuwaletea maendeleo wananchi.
Amesisitiza wananchi waendelee kuiamini na kuipa nafasi CCM izidi kudumisha amani kwa kuwa maendeleo hayatapatikana iwapo itatoweka.
Wasira alieleza hayo alipokuwa akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM kutoka Jimbo la Mbeya, akiwa katika ziara ya kumwombea kura mgombea urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan pamoja na wagombea wa ubunge na udiwani mkoani Mbeya.
Alitumia mkutano huo kumwombea kura Dk. Samia, wagombea ubunge na udiwani waliosimamishwa kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu Oktoba 29, mwaka huu.
“Kazi yetu ni kuleta mabadiliko katika maisha ya watu, ukitengeneza barabara unamwezesha huyu mtu kufikisha bidhaa zake sokoni kwa hiyo ataongeza kilimo na uchumi wake utaongezeka kwa sababu ana mahali pakuuza.
“Ukimnyima barabara analima chakula chake cha kula na kufa, anakula ashibe angojee kifo maana hakuna maendeleo hapo,” alisema Wasira.
Alisema kuwajengea wananchi miundombinu muhimu ikiwemo ya hospitali ni kuwapunguzia safari ya kwenda kutafuta dawa maeneo ya mbali kutoka katika makazi yao.
“Tumepiga hatua lakini maendeleo hayana kikomo na wala hayamalizi matatizo yote kwa mpigo kwa sababu hata ukifanya maendeleo makubwa zaidi unaweza ukazalisha matatizo mapya.
MIAKA MINNE YA MAFANIKIO
Alieleza katika miaka minne ya uongozi wa Rais Dk. Samia, CCM imesimamia maendeleo makubwa yaliyowagusa wananchi moja kwa moja.
“Tukisema Samia mitano tena ni kwa sababu kuna kazi amefanya na ameifanya kwa uzuri na ana uzoefu wa kuifanya, ametekeleza vema miradi mikubwa iliyoachwa na mtangulizi wake likiwemo bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere.
“Amejenga lile bwawa limefikia asilimia 100, hivi sasa tuna megawati 4,000 badala ya 1,600 alizoachiwa na mtangulizi wake na hakuna shida ya umeme labda matatizo ya miundombinu,” alisema.
Alieleza katika miaka minne na nusu, Serikali ya Awamu Sita imejenga shule mpya za msingi tisa, madarasa 280 mapya na sekondari nane katika wilaya hiyo bila wananchi kuchangishwa chochote.
KUHUSU AMANI
Wasira aliwasisitiza Watanzania kulinda amani kwa kuwa ndiyo nyenzo muhimu ya kuleta maendeleo ya sekta zote.
“Amani ikipotea hata madaraja tuliyojenga hayana maana, hata barabara zinachimbika kwa sababu amani imetoweka kwa hiyo kazi yetu Chama Cha Mapinduzi pamoja na kulinda umoja wa taifa, tunataka kuhakikisha amani amani inakuwepo kwa sababu ikitoweka hakuna maendeleo,” alieleza.
Naye, Ndele Mwaselela akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, alisema Chama mkoani humo kimejipanga vema kuhakikisha uchaguzi mkuu Oktoba 29, mwaka huu, wagombea wake wote wanapata kura za kishindo.
Mwaselela alisema wamejipanga kumtafutia kura nyingi Dk. Samia zitakazomwezesha kuibuka mshindi aendelee kuiongoza nchi kwa mafanikio.
Mgombea ubunge katika Jimbo la Mbeya Vijijini, Patali Shida, alisema iwapo ataibuka mshindi ataendelea kusimamia vema kasi ya maendeleo kuendeleza iliyofanyika katika miaka mitano iliyopita.