Na MUSSA YUSUPH,
Musoma
KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Kihongosi, ametoa wito kwa vijana kutokubali kutumika kisiasa kuvuruga amani ya nchi.
Kihongosi aliyasema hayo katika mkutano wa kampeni uliohutubiwa na Mgombea Urais kupitia CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, uliofanyika wilayani Busega mkoani Simiyu.
Kihongosi ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, alieleza siasa hazipaswi kutumika kuchochea vurugu na kusisitiza umuhimu wa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kulinda amani.
Kuhusu maendeleo, alisema katika Kata ya Lamadi kulikuwa na changamoto ya maji ambapo kazi kubwa imefanyika ya kusimamia mradi wenye thamani zaidi ya sh. bilioni 400.
Alisema maji hayo yatasambazwa Meatu, Busega, Itilima hadi Bariadi, hivyo kupunguza changamoto ya uhaba wa maji.
Pia, alisema wananchi wa eneo la Nyanshimo wameondokana na kero ya mafuriko baada ya Dk. Samia kutoa fedha za kujenga daraja.