Na NJUMAI NGOTA,
Pwani
MGOMBEA Mwenza wa Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema katika miaka minne na nusu, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, amefanya mambo mengi makubwa, likiwemo kukamilika kwa ujenzi wa Bandari Kavu ya Kwala.
Dk. Nchimbi alisema hayo, Uwanja wa Mama Salmini, Mlandizi, mkoani Pwani, katika mkutano wa hadhara wa kampeni za Chama kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu.
Alisema kukamilika kwa bandari hiyo, kumeleta mabadiliko makubwa ya kimtazamo kwa wananchi wa mkoani huo na Watanzania.
Kwa mujibu wa Dk. Nchimbi, mafanikio hayo ni ushahidi wa wazi kuwa, serikali imeitekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa vitendo.
Balozi Dk. Nchimbi aliongeza kwamba, kukamilika kwa Bandari Kavu ya Kwala ni hatua muhimu ambayo imefungua fursa mpya za kiuchumi mkoani Pwani na Taifa kwa ujumla.
Mradi huo mkubwa ni miongoni mwa miradi ya kimkakati iliyoasisiwa na kusimamiwa kwa umakini mkubwa na serikali chini ya uongozi wa Dk. Samia.
“Katika miaka hii minne na nusu, Rais Samia ameinua uchumi wa Taifa kutoka asilimia nne hadi kufikia asilimia 5.6 kwa kushirikisha sekta zote, zikiwemo kilimo, viwanda, biashara na huduma nyingine muhimu,” alisema.
Kwa upande wa diplomasia ya uchumi, Dk. Nchimbi alisema Tanzania hivi sasa imeimarika kimataifa kwa kiwango kikubwa, jambo lililosaidia kuvutia wawekezaji na kushirikiana na nchi nyingine kwa manufaa ya Watanzania.
Balozi Dk. Nchimbi alibainisha serikali imefanya mageuzi makubwa katika biashara kwa kuwawezesha wananchi wengi kusajili biashara zao, ambapo hadi hivi sasa zaidi ya Watanzania 224,536 wamesajili biashara, ikilinganishwa na 137,000 waliokuwepo kabla.
“Haya ni mageuzi makubwa katika mfumo wa kufikiri na kufanya biashara. Wananchi wetu hivi sasa wanaelewa umuhimu wa kuwa na biashara zilizosajiliwa na zinazotambulika rasmi,” alisisitiza.
Akizungumzia mipango ya miaka mitano ijayo iwapo Chama kitapewa ridhaa ya kuongoza nchi, Dk. Nchimbi alieleza dhamira ya CCM na Dk. Samia ni kuendelea kuboresha huduma za kijamii na kiuchumi kwa wakazi wa Mlandizi.
“Tutaimarisha Hospitali ya Wilaya ya Mlandizi, tutajenga vituo vya afya viwili na zahanati tisa,” aliahidi.
Kuhusu sekta ya elimu, Dk. Nchimbi alisema wanakusudia kujenga shule za msingi tano na sekondari nne, madarasa 60 kwa shule za msingi na 46 kwa sekondari.
Akizungumzia sekta ya kilimo, Dk. Nchimbi alisema serikali ya CCM ijayo, inakusudia kuendeleza na kujenga skimu mpya za umwagiliaji, kuimarisha huduma za ugani na kuhakikisha kila mkulima anapata elimu ya kisasa ya kilimo kupitia mashamba darasa.
Alisema katika sekta ya ufugaji, wanakusudia kukarabati mabwawa sita ya kunyweshea mifugo na kuyafanya ya kisasa, kujengwa kwa majosho matatu na mnada mpya wa kisasa.
Akielezea sekta ya biashara, Dk. Nchimbi alibainisha Ilani ya CCM ya mwaka 2025-2030, imeainisha ujenzi wa soko la kisasa la Mlandizi, stendi ya mabasi na kuboresha mazingira ya biashara.
Katika sekta ya nishati, alisema vijiji vyote tayari vimepata huduma ya umeme na kilichosalia ni kukamilisha kazi katika vitongoji 48.
Alisema vijiji hivyo, vipo katika mpango wa kupata huduma hiyo kupitia utekelezaji wa Ilani na kwamba, wanakusudia kujenga vituo viwili vya kupoza umeme maeneo yote, yawe na uhakika na nishati hiyo.
Dk. Nchimbi aligusia sekta ya maji na kusema serikali imejipanga kukamilisha miradi mbalimbali ya maji, ukiwemo wa Kwala unaohusisha Bandari Kavu ya Kwala na wananchi wa maeneo hayo.
“Mradi huu pia utanufaisha maeneo ya viwanda, mtandao wake wa maji safi utaendelezwa kufikia zaidi ya maeneo 10, yakiwemo Misugusugu na Visiga,” alisema.
Kuhusu barabara, alisema Ilani ya CCM imedhamiria kujenga barabara na kilometa zake katika mabano ambazo ni Mlandizi – Ruvuma (23), Mlandizi – Maneromango (65), Mlandizi hadi Msikitini na ya Halmashauri yenye urefu wa mita 400 na 300 na kilometa moja kwenda Kwala ambazo zitajengwa kwa kiwango cha lami.
Dk. Nchimbi alimwombea kura mgombea urais wa Chama, Dk. Samia, wagombea ubunge na udiwani wanaotokana na Chama.
Naye, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini, Hamoud Jumaa, alisema wananchi wa jimbo hilo, hawana chembe ya shaka kuhusu ushindi wa Chama katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu.
Jumaa alisema ushindi huo, utatokana na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025, chini ya uongozi wa Dk. Samia.