Na MUSSA YUSUPH,
Geita
MGOMBEA Ubunge wa Viti Maalumu, Jesca Magufuli, amesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ni kiongozi mwenye ujasiri mkubwa na shupavu ambaye katika kipindi cha miaka minne ametekeleza miradi mikubwa ya kimkakati.
Jesca ameyasema hayo katika mkutano wa kampeni uliohutubiwa na Mgombea Urais kupitia CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, uliofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Bukombe.
Amesema licha ya kutekeleza miradi hiyo aliyorithi kutoka kwa mtangulizi wake, Hayati Dk. John Magufuli, lakini ameanzisha miradi mingine ya kimkakati.
“Wengi tunafahamu adha tuliyokuwa tukikumbana nayo pale Daraja la Kigongo – Busisi. Ametufanyia makubwa sisi wakazi wa Kanda ya Ziwa.
“Tuna kila sababu ya kumwamini kiongozi wetu, tukajitokeze kwa wingi kumpigia kura Dk. Samia ifikapo Oktoba 29 mwaka huu,” amesisitiza.
Jesca, amesema katika ilani ya uchaguzi (2025 – 2030), CCM imeahidi kutengeneza ajira zaidi ya milioni nane, kutoa mafunzo kwa vijana na kukuza teknolojia kuongeza wigo wa ajira kwa vijana.
“Samia ni mtu wa kazi, mpeni kazi, akafanye kazi,” amesisitiza.