Na NASRA KITANA
WACHEZAJI wa timu za Simba na Yanga, wamewaomba mashabiki wake kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam kuwapa sapoti katika mechi za marudiano katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL).
Katika ratiba ya hatua ya pili ya mtoano ya CAFCL, Yanga itachuana na Silver Striker ya Malawi kesho wakati Simba ikishuka dimbani dhidi ya Nsingizini Hotspurs ya Eswatini keshokutwa.
Yanga itaingia katika mtanange huo ikiwa na kumbukumbu ya kichapo cha bao 1-0 ilichokipata Malawi wakati Simba ikipata ushindi wa mabao 3-0 nchini Eswatini.
Nyota wa Simba, Jonathan Sowah, alisema bado hawajamaliza kazi hivyo mashabiki na wapenzi wa Simba wanatakiwa kujaa kwa wingi uwanjani kuwapa sapoti ya kutosha.
Sowah alisema anajua utakuwa mchezo mgumu lakini wachezaji watapambana kuhakikisha wanatimiza malengo ya timu.
“Tunakwenda kukamilisha mchezo wetu wa marudiano na lengo kubwa ni kuhakikisha tunapata ushindi hivyo tunawaomba mashabiki na wapenzi wa Simba kujaa kwa wingi uwanjani watupe sapoti ya kutosha na kutuongezea morali ya ushindi,” alisema Sowah.
Beki wa Wekundu hao wa Msimbazi, Shomari Kapombe, alisema ushindi walioupata ugenini umewaongezea morali ya kutosha katika mchezo wa marudiano lakini bila ya mashabiki wao itakuwa ni ngumu kufanya vizuri.
“Tunawaomba mashabiki wetu wajae kwa wingi uwanjani watupe sapoti ya kutosha kwani bila wao sisi si kitu, umoja na mshikamano wao kwetu utatuongezea nguvu ya kufanya vizuri zaidi,” alisema Kapombe.
Mlinzi wa Yanga, Ibrahim Bacca alisema mashabiki na wapenzi wa timu yao wanatakiwa kuingia kwa wingi uwanjani kuwapa sapoti ya kutosha watinge makundi.
“Jamani mchezo wetu ni bure hivyo niwaombe mashabiki wa Yanga kuhakikisha wanakuja kwa wingi uwanjani kuipa sapoti ya kutosha timu na kutuongezea morali tutinge hatua ya makundi,” alisema Bacca.
Naye nahodha wa timu hiyo, Dikson Job, alisema huo ni mchezo muhimu kwao kuhakikisha wanapata ushindi hivyo mashabiki wana mchango mkubwa katika mchezo huo.
“Uzuri mchezo wetu ni bure, mashabiki na wapenzi wa timu yetu wanatakiwa kujaa kwa wingi uwanjani ili waweze kutupa sapoti ya kutosha kwani sapoti yao nduo itatuongezea morari kubwa ya kupata ushindi,” alisema Job.




