Na ATHNATH MKIRAMWENI
JUMLA ya watahiniwa 937,581 sawa na asilimia 81.80 ya watahiniwa 1,146,164 katika matokeo ya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi mwaka 2025, wamefaulu kwa kupata daraja A, B na C.
Akitangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Profesa Said Mohamed, amesema mwaka 2024 watahiniwa waliofaulu walikuwa asilimia 80.87.
“Ufaulu umeongezeka kwa asilimia 0.93. Kati ya watahiniwa 937,581 waliofaulu, wavulana ni 429,104 sawa na asilimia 82.51 na wasichana ni 508,477, sawa na asilimia 81.21.
“Mwaka 2024 wasichana waliofaulu walikuwa asilimia 80.05 na wavulana waliofaulu walikuwa asilimia 81.85. Hivyo, ufaulu wa wasichana umeongezeka kwa asilimia 1.16 na ufaulu wa wavulana umeongezeka kwa asilimia 0.66,”amesema.
Kuhusu ubora wa ufaulu, watahiniwa 422,923 sawa na asilimia 36.90, wamepata daraja ya A na B, ikiwa ni ongezeko la asilimia 1.07 ikilinganishwa na mwaka 2024.




