Na MWANDISHI WETU
KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda, amewahakikishia wafanyabiashara wa soko la Kimataifa la Kariakoo usalama wa biashara zao.
Mwenda aliyekutana na viongozi wa wafanyabiashara hao, wamachinga na wafanyabiashara wenyewe, aliwapa pole kutokana na kufunga biashara zao katika kipindi cha uchaguzi pamoja na madhara waliyopata katika kipindi hicho.
“Nimekuja kuona shughuli mnazofanya, pia kuwapa pole kwa changamoto zilizotokea, nimekuja kuona biashara zinaendeleaje na nimefurahi kuona biashara zinaendelea kama kawaida na nimethibitishiwa na wauzaji nilizungumza nao kuwa, wanauza kama kawaida na wateja wanakuja,”alisema Mwenda.
Pia, kamishna huyo alishuhudia shughuli za biashara zikiendelea kama kawaida katika soko la Kariakoo hali ikiwa shwari na kuwahakikishia wafanyabiashara TRA itaendelea kulinda ustawi wa biashara zao kwa kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili.
“Biashara zenu binafsi ni biashara za umma, na sisi ni wabia wa biashara hizo, hivyo tuna wajibu wa kuzilinda na kuhakikisha zinastawi,” alisema Mwenda.
Alisema kuimarika biashara katika soko la Kariakoo kunahakikisha kufunguka biashara katika maeneo mengine ya nje ya jiji la Dar es Salaam na nchi jirani na kuwataka viongozi wa wafanyabiashara wafanye tathmini ya athari zilizotokana na changamoto zilizojitokeza kipindi cha uchaguzi mkuu katika biashara zao kushauri hatua zinazopaswa kuchukuliwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa Kariakoo, Severin Mushi, alisema hali ya biashara katika soko la Kariakoo imeimarika na kueleza wateja na wafanyabiashara wapo salama, huku akitoa wito kwa wananchi kwenda kufanya manunuzi.
Naye, Mwenyekiti wa Wamachinga, Stephen Lusinde, alisema biashara zao ndani ya soko la Kariakoo na nyingine zililindwa na vijana takriban 150 katika kipindi chote cha changamoto na kuwahakikishia usalama wananchi wanaotaka kwenda Kariakoo kununua bidhaa.




